Advertisements

Sunday, September 4, 2016

MJANE AUAWA, ANYOFOLEWA VIUNGO MKOANI TABORA

MJANE mwenye umri wa miaka 46, Veronica Dala ameuawa na watu wasiofahamika kwa kukatwa na mapanga mwilini. Aidha mjane huyo amenyofolewa baadhi ya viungo vya mwili wake.
Tukio hilo limetokea alfajiri ya Septemba Mosi mwaka huu katika kijiji cha Ilagaja, kata ya Mwangoye wilayani Nzega mkoani Tabora baada ya wahalifu hao kuvamia nyumba ya mjane huyo kisha kuanza kumshambulia kwa mapanga.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya majirani na ndugu wa mjane huyo walisema walipata taarifa ya kuwa ameuawa na watu wasiofahamika asubuhi ya tukio hilo.
Luhaga Jilala ambaye ni ndugu wa mjane huyo, alisema taarifa hizo alizipata asubuhi kuwa ndugu yake ameuawa. Hata hivyo, chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Juma Seleli alisema tukio hilo ni la pili kutokea miaka kadhaa iliyopita alivamiwa na wahalifu na kumjeruhi vibaya.
Alisema kijiji hicho kimejipanga kuhakikisha wanafanya doria za mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi wa kijiji na wananchi wake.

Diwani wa kata hiyo, Henerico Kanoga alisema atahakikisha wananchi wanafanya uchunguzi kwa kupiga kura za maoni ili kuwapata watu wanaoshiriki kufanya uhalifu huo wa kikatili.
Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla alisema Serikali ya Wilaya imeandaa mpango mkakati wa kuhakikisha wananchi wanatoa ushirikiano wa kutosha ili kukomesha mauaji.
Alisema wilaya ina mpango wa kuanza kupiga kura za maoni kwa wananchi ili kuwabaini wote wanaoshirikiana na wahalifu hao na kuongeza kuwa mwananchi atakayetoa taarifa dhidi ya wahalifu hao, siri zote zitatunzwa ili kulinda usalama wake.
Polisi mkoani Tabora imekiri mauaji hayo na kuahidi kufanya msako mkali kwa ajili ya kuwakamata na inawashikilia watu wawili kwa ajili ya mahojiano.

CHANZO: HABARI LEO

No comments: