Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) Dk Albina Chuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam. (Picha na Mroki Mroki)
OFISI ya Taifa ya Takwimu(NBS) imebainisha kuwa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, Pato la Taifa limeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 7.9 ikilinganishwa na asilimia 5.8 ya robo ya pili ya mwaka jana.
Aidha, imetaja sekta zilizochangia kukua kwa kasi kwa pato hilo kuwa ni kilimo, viwanda, uchukuzi, ujenzi, madini na umeme kupitia gesi asilia.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu taarifa hiyo ya uchumi kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema kutokana na kasi ya uchumi inavyokwenda kwa sasa, huenda ifikapo Desemba mwaka huu, kwenye taarifa ya robo ya tatu ya mwaka pato hilo likaongezeka zaidi.
Dk Chuwa alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo pato hilo la taifa lime fikia jumla ya thamani ya Sh trilioni 11.7 ikilinganishwa na Sh trilioni 10.9 katika kipindi kama hicho cha mwaka jana. “Imekadiriwa kuwa pato la taifa mwaka huu kwa bei ya mwaka wa kizio 2007 litakuwa Sh trilioni 47.2 ikilinganishwa na Sh trilioni 44.1 iliyopatikana mwaka jana,” alisisitiza.
Dk Chuwa alisema pato hilo kwa bei za soko katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu ni Sh trilioni 26.7, ikilinganishwa na Sh trilioni 23 kwenye kipindi kama hicho mwaka jana. Makadirio ya pato hilo la taifa kwa bei za soko za mwaka huu ni Sh trilioni 104.4 ikilinganishwa na Sh trilioni 90.8 za mwaka jana.
Alisema ukuaji wa pato hilo la taifa limechangiwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambapo kwa upande wa sekta ya kilimo inayojumuisha mifugo, misitu na uvuvi ilikuwa kwa kasi ya asilimia 3.2 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji ya asilimia 1.9 ya robo ya pili ya mwaka jana.
Alisema katika kilimo cha mazao kilikua kwa asilimia 3.4 ikilinganishwa na asilimia 5.2 ya mwaka jana, ufugaji uliongezeka kwa asilimia 2.5 mwaka huu, ikilinganishwa na asilimia 2.3 mwaka jana, misitu ilikua kwa asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 3.7 ya mwaka jana wakati uvuvi kasi yake ilipungua kwa asilimia 3.6 mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 3.7 ya mwaka jana.
Alisema kwa upande wa shughuli za uchumi, viwanda na ujenzi, shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto ziliongezeka kwa kasi ya asilimia 20.5 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu ikilinganishwa na kasi ya asilimia 11.2 ya kipindi kama hicho mwaka jana.
Alisema kasi ya ukuaji wa madini na mawe, ilichangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia, almasi, tanzanite, chumvi, dhahabu, shaba na madini ya fedha.
“Uzalishaji wa gesi asilia ulikuwa ni futi za ujazo 11,267 mwaka huu ikilinganishwa na futi za ujazo 7,793 zilizozalishwa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka jana na uzalishaji wa dhahabu mwaka huu ulikuwa ni kilogramu 11,577 ikilinganishwa na kiligramu 10,682 zilizozalishwa mwaka jana."
Kwa upande wa almasi, alisema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu ilikuwa karati 58,068 ikilinganishwa na karati 52,928 zilizozalishwa mwaka jana na madini ya tanzanite yaliyozalishwa mwaka huu yalikuwa kilogramu 4,110 ikilinganishwa na kilogramu 3,110.
Aidha, katika eneo la shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani, mkurugenzi huyo alisema katika robo hiyo ya pili ya mwaka huu, shughuli hizo zilikua kwa kasi ya asilimia 9.1 ikilinganishwa na asilimia 5.2 iliyozalishwa mwaka jana.
“Kasi ya ukuaji wa shughuli hizi ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa za vyakula, tumbaku, nguo, saruji, dawa, uchapaji na utengenezaji wa samani,” alisisitiza Dk Chuwa.
Alisema kwa upande wa shughuli za uzalishaji nishati ya umeme, zilikua kwa kasi ya asilimia 7.1 na kuongeza kuwa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu kiasi cha kilowati za umeme milioni 1,751 zilizalishwa ikilinganishwa na kilowati za umeme milioni 1,559 za mwaka jana.
“Kasi ya ukuaji wa shughuli za uzalishaji nishati ya umeme ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi asilimia,” alifafanua.
Kuhusu eneo la ujenzi linalojumuisha nyumba za makazi na zisizo za makazi, barabara na madaraja na shughuli za uhandisi lilikuwa kwa kasi ya asilimia tisa mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 13.2 mwaka jana.
Halikadhalika, Dk Chuwa alizitaja shughuli za uchumi za utoaji huduma kuwa katika kipindi hicho cha robo ya pili ya mwaka huu zilikua kwa kasi ndogo ya asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 9.5 katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Alisema kupungua kwa kasi ya ukuaji ya shughuli hizo zinazojumuisha biashara za jumla na rejareja, ukarabati wa magari na pikipi na vifaa vingine vya nyumbani kulitokana na kupungua kwa asilimia 22.8 ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi.
Akizungumzia upande wa shughuli za uchukuzi na uhifadhi, alisema zilikua kwa kasi ya asilimia 30.6 mwaka huu ikilinganishwa na kasi ya asilimia 9.4 ya mwaka jana. Ukuaji wa kasi hiyo ulitokana na kuongezeka kwa shughuli za usafirishaji abiria kwa njia ya reli na barabara ukiwemo usafiri wa mabasi yaendayo haraka (DART) na gesi asilia.
Hata hivyo, alifafanua kuwa pamoja na kwamba shughuli za bandari nazo zilichagia katika ukuaji wa eneo hilo, lakini kutokana na tatizo la mdororo wa usafirishaji mizigo duniani ulioathiri nchi nyingi, hata bandari ya Tanzania nayo iliathirika na kupungua kwa usafirishaji wa mizigo hiyo.
“Nawaomba wachumi wetu wasikae tu kukosoa, waisaidie serikali kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na hali hii. Kwani nchi yenye bandari kubwa duniani Singapore ambayo nayo imeathirika, imeanza kuchukua hatua kwa kupunguza bei za mizigo inayoingizwa nchini humo,” alifafanua.
Dk Chuwa alisema kiujumla tathmini ya ukuaji wa pato la taifa kwa kipindi hicho cha robo ya pili ya mwaka huu, inaonesha kuwa uchumi unakua kwa kasi ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Alitoa mfano wa nchi ya Rwanda ambayo ndio nchi pekee katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokwishatoa taarifa yake ya uchumi kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, ambayo inaonesha pato lake limekua kwa asilimia 5.4 mwaka huu, ikilinganishwa na asilimia 7.2 ya mwaka jana.
Aidha, ripoti ya Benki ya Dunia imebainisha kuwa wakati uchumi wa nchi nyingi za Jangwa la Sahara ukibainika kushuka kwa kasi, nchi ya Tanzania, Senegal, Ivory Coast, Ethiopia na Rwanda uchumi wake umeonekana kukua.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo, jana nchi nyingi za Jangwa la Sahara uchumi wake unatarajiwa kushuka na kufikia kiwango cha asilimia 1.6 kutokana na changamoto za kiuchumi zilizojitokeza katika mataifa yake makubwa yanayokua kiuchumi na yanayojishughulisha na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.
Taarifa hiyo, ilifafanua kuwa nchi hizo nyingi kwa sasa zinakabiliwa na matatizo hayo kutokana na kushuka kwa kasi kwa bei ya mafuta na kukabiliwa na mazingira magumu ya kifedha.
Mkuu wa Kitengo cha Uchumi cha benki hiyo, Albert Zeufack alisema wachambuzi wa benki hiyo wamebainisha kuwa nchi hizo zinaweza kunyanyuka kiuchumi endapo zitakuwa na sera za uhakika za kiuchumi na kujiwekea mazingira mazuri ya kibiashara.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kutokana na jitihada zinazooneshwa na nchi nyingi katika Jangwa la Sahara Pato la Taifa la nchi hizo linatarajiwa kukua na kufikia asilimia 2.9 mwakani ambapo kwa mwaka 2018 inakadiriwa kufikia asilimia 3.6.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment