Advertisements

Tuesday, September 27, 2016

TANZANIA YATAKA USHIRIKIANO KATIKAA VITA DHIDI YA RUSHWA NA UKWEPAJI KODI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ,Dkt. Augustine Mahiga anayemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli katika Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akiwasilisha mbele ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo ( hawapo pichani) vipaumbele vya Tanzania.
Balozi wa Tanzania nchi Marekani Wilson Masilingi akimpa mkono wa pongezi Waziri Mahiga baada kumaliza hotuba yake mbele ya wajumbe wa mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mhe. Anna Lupembe Mbunge wa Viti Maalum (CCM) naye akimpongeza Mhe, Waziri kwa hotuba yake iliyopokelewa vizuri.
Dk. Tausi Kida Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF naye akimpongeza Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakiwa katika mstari tayari kumpa mkono Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Augustine Mahiga mara baada ya kumalia hotuba yake

Na Mwandishi Maalum, New York 
Tanzania imeeleza kwamba juhudi za serikali ya awamu ya Tano za kukabiliana na vitendo vya rushwa hazitaweza kufanikiwa kama havita ungwa mkono na jumuiya ya kimataita.

Ni kwa sababu hiyo, Tanzania, inazitaka nchi zilizoendelea kuwawajibisha wawekezaji wao na makampuni yao ili yalipe kodi.

Hayo yameelezwa jana jumatatu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Agustine Mahiga ( Mb) wakati alipolihutubia Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa na kutumia fursa hiyo kuelezea vipaumbele vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mahinga akafafanua kwamba, lengo namba kumi na sita la maendeleo endelevu linatambua kuwa, rushwa inakandamiza juhudi za kumbana na umaskini na usawa wa jinsia, inazuia fursa na inakuwa na kama kodi kwa familia maskini pale wanapotafuta haki.

Ni katika muktadha huo, akasema, serikali ya Tanzania imeamua kuanzisha vita dhidi ya rushwa kwa kuhuisha uwazi, uwajibikani na usahihi katika utoaji wa huduma kwenye taasisi za umma.

Akasisitiza kwamba serikali imeweka misingi mizuri ya uwajibikaji inayomtaka mtumishi wa umma kutambua kwamba wajibu wake wa kwanza ni kutoa huduma bora na kwa wakati kwa umma.

“Juhudi hizi za serikali za kupambana na rushwa hazitaweza kuzaa matunda bila ya kuungwa mkono wa jumuiya ya kimataifa. Nchi zilizoendelea zinatakiwa kuwawajibisha wawekezaji wao pamoja na makampuni yao ili waweze kulipa kodi stahiki.” Akaeleza zaidi Waziri Mahinga

Na kuongeza. “Ni lazima wawe tayari kurudisha mali na fedha zilizoibwa kutoka nchi zinazoendelea na kuzificha katika nchi zao ili mali na fedha hizo ziweze kusaidia maendeleo yetu”.

Kuhusu fursa za jinsia na uwezeshwaji wa wanawake, Waziri Mahinga ameelezea juhudi mbalimbali ambazo zimefanywa na serikali katika kuwawezesha wawanake ikiwamo kushika ngazi za juu za maamuzi kuanzia serikali kuu hadi bunge na uwezeshwaji wa kiuchumi.

katika kudhibitisha kuwa Tanzania inazingatia usawa wa jinsia katika uteuzi wa ngazi mbalimbali za maamuzi, Waziri Mahinga ameeleza kwamba kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Rais John Pombe Magufuli alimchangua mwanamke kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Uteuzi huu unathibitisha nia ya nchi yangu ya kuona wanawake wengi zaidi wanakuwa katika nafasi za ngazi za juu za maamuzi. Na ajenda hii ya uwezeshwaji wa wanawake wa Tanzania sasa inamilikiwa na wanawake wenyewe” akasisitiza Waziri

Kwa upande wa vijana, Kiongozi huyu wa Ujumbe wa Tanzania ambaye amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema. Vijana ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote lile, siyo tu kwamba ni viongozi wa kesho lakini pia ni viongozi wa sasa.

Akatahadharisha kwamba kwa kutowapa kiupaumbele vijana ni kujitafutia matatizo makubwa kutokana na kile alichosema ni rahisi kurubuniwa na makundi ambayo ni hatari kwa ustawi wa jamii na taifa .

“ Kutoka na kwamba idadi ya vijana ni kubwa, serikali inachukua hatua mbalimbali za kuliwezesha kundi hili la jamii ambalo ni muhimu katika utekelezaji wa ajenda 2030. Na ili vijana waweze kutekeleza jukumu hilo serikali imeanzisha mfuko wa maendeleo wa vijana mfuko ambao hadi mwezi March mwaka huu jumla ya shiling 1.6 bilioni zilipelekwa kwa vikundi 284 ya vijana”.

Kuhusu elimu, eneo ambalo ni kipaumbele kingine cha Tanzania, Waziri ameeleza kuwa upatikanaji wa elimu jumuishi na ya viwango ndicho kipaumbele cha serikali kwa kuwa Serikali inaamini kuwa, elimu ni ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu

Akafafanua kwamba serikali inatekeleza bila kuchoka kuhakikisha kwamba watoto wote wa kike na wa kiume wanapata elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Pamoja na kutoka elimu bure, serikali imeboresha mitaala yake kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.

“Alipoingia madarakani, Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitangaza kwamba kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari itakuwa bure. Serikali imetenga zaidi ya shilingi 263 bilioni ili kuhakikisha elimu inakuwa bure kwa wote.

Vipaumbele vingine vya Tanzania ambavyo Mhe. Waziri amevianisha katika hotuba yake ni pamoja na mikakati ambayo serikali imejiwekea katika utekelezaji wa mkataba wa mabadiliano ya tabia nchi ( Paris Agreement), utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu ( agenda 2030), mapambano dhidi ya dawa haramu za kulevya, na kukabiliana na ugaidi ambao amesema ni tatizo ambalo linaendelea kukua na kuwa tishio hata kwa nchi za Afrika Mashariki.

Kwa upande wa utekelezaji wa agenda 2030, Waziri amesema agenda hiyo imeanishwa katika mipango ya kitaifa ya miaka mitano ya maendeleo kwa pande zote za muungano. Hata hivyo amesema kuwa Tanzania imebaini kwamba haitaweza kukamilisha kwa wakati agenda 2030 pasipo kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo. 

Kuhusu migogoro inayoendelea katika nchi za Burundi na Sudani ya Kusini, Waziri Mahiga amezitaka pande zote zinazopingana nchi Burundi kutambua kwamba majadiliano ambayo ni jumuishi kwa pande zote ndiyo njia sahihi ya kutatua matatizo ya nchi yao.

Kwa upande wa Sudani ya Kusini, Waziri amesema Tanzania inaungana na nchi nyingine kulaani matukio ya hivi karibuni ya kujirudia kwa machafuko nchini humo.

Na kuongeza, Tanzania ambaye ni Mwenye -Kiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliitisha kikao kisicho cha kawaida ili kuzungumzia hali ya kisiasa ya Burundi na Sudani ya Kusini. “ Tunatumaini kwamba nchi zote mbili zitaweka maslahi ya wananchi wao mbele ili kumaliza machafuko”.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pia aligusia kuhusu marekebisho ya mfumo wa Baraza Usalama la Umoja wa Mataifa, ili liwe jumuishi. 

Kwa upande wa Uchaguzi wa Katibu Mkuu, Waziri amesema, Tanzania inaunga mkono hoja ya kuendelea kuheshimu utaratibu wa kupokezana nafasi ya Katibu Mkuu kwa kuzingatia mzugunko wa kijiographia.

No comments: