Advertisements

Monday, September 12, 2016

TETEMEKO LAFUTA ZIARA YA JPM ZAMBIA

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar/Dodoma. Rais John Magufuli ameahirisha ziara ya siku tatu nchini Zambia ambako alikuwa ahudhurie sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo, Edgar Lungu ili kushughulikia tatizo la tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya watu 16 mkoani Kagera.

Taarifa ya iliyotolewa na Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Jaffar Haniu jana usiku ilisema badala yake, Dk Magufuli amemtuma Makamu wake, Samia Suluhu Hassan kumuwakilisha katika sherehe hizo. Sherehe za kumwapisha Rais Lungu zinatarajiwa kufanyika kesho Lusaka.

Taarifa hiyo ilikuwa inafuta nyingine iliyotolewa awali na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa iliyosema Rais Magufuli alitarajiwa kuwasili Lusaka leo kwa shughuli hiyo.

Ilisema Rais Magufuli anafanya ziara ya kwanza Zambia akiwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) inayojulikana kwa jina la SADC-Troika wadhifa alioupokea kutoka kwa Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi katika Mkutano wa 36 wa SADC uliofanyika katika Mbabane Swaziland Septemba 1, 2016.

Wafiwa wasimulia

Wakati vifo vya watu waliopoteza maisha kutokana na tetemeko la ardhi lililoikumba baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa juzi iliongezeka na kufikia 16, kijana mmoja Edson Simon, mkazi wa Mtaa wa Kashenye Manispaa ya Bukoba amebaki mjane baada ya kufiwa na mkewe, Verdina Simon aliyekuwa na ujauzito wa miezi minane.

Akizungumza jana katika ibada ya kuaga miili ya watu hao iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini hapa, Simon alisema: “Nilimwacha mke wangu amelala kutokana na kujisikia vibaya tangu usiku wa kuamkia juzi. Nilienda kijiweni kutafuta hela ya kumpeleka hospitali lakini nikaishia kumpeleka chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema Simon huku akibubujikwa machozi katika ibada hiyo ambayo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Vifo vyaongezeka

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema hadi kufikia jana mchana, watu 16 walithibitika kupoteza maisha huku nyumba 840 zikiwa zimeporomoka. Hadi juzi jioni watu 11 walikuwa wameripotiwa kupoteza maisha.

“Nyumba 1,264 zimeharibika kwa kupata nyufa huku watu 253 wakijeruhiwa. Watu 83 walitibiwa na kuruhusiwa baada ya hali zao kutengamaa,” alisema.

Miongoni mwa nyumba zilizoathirika ni pamoja na majengo ya Serikali na taasisi za umma 44.

Waliofiwa wasimulia

“Tetemeko la ardhi limeniacha mjane kwa umri huu mdogo wa miaka 27... ama kweli duniani tunapita,”

Alisema Simon, mkazi wa Mtaa wa Kashenye Manispaa ya Bukoba aliyempoteza mkewe, Verdina Simon aliyekuwa na ujauzito wa miezi minane ambaye ni kati ya watu 16 waliofariki dunia katika tetemeko la ardhi lililotikisa mkoa wa Kagera na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa juzi.

“Tetemeko siyo tu limenidhulumu penzi langu kwa kumchukua mke wangu, bali pia limezima ndoto yangu ya kumpakata mtoto wangu wa kwanza,” aliongeza: “Laiti ningejua nisingemwacha mke wangu nyumbani, ningeondoka naye hata akae na mimi kijiweni nikiendelea kusaka fedha za kumpeleka hospitali.”

Akisimulia siku ya mwisho ya mkewe, kijana huyo alisema usiku wa kuamkia Jumamosi haukuwa mzuri kwa familia yake kwani mkewe alilalamika usiku kucha kuwa anajisikia vibaya na kumwomba ampeleke hospitali.

Alisema kulipopambazuka aliamua kwenda kijiweni kusaka fedha na kurejea nyumbani mchana kwa ajili ya chakula cha mchana na alimkuta mkewe akiwa amejipumzisha.

“Nilijaribu kumshawishi atoke nje ili apunge upepo na kuzungumza na majirani lakini aligoma na kuendelea kuketi kwenye kiti ndani ya nyumba hali iliyozidi kuninyong’onyeza kwa sababu hadi wakati huo sikuwa nimepata fedha za kutosha kumpeleka hospitali,” alisimulia.

Alisema baada ya kumaliza kula aliagana naye na kurejea kijiweni kutafuta fedha na alipofika eneo la Kilimanjaro, tetemeko lilianza.

“Bila kujua kilichotokea nyumbani kwangu, nililazimika kumpakia mwanamke mmoja niliyemkuta njiani akilia akiomba msaada wa kukimbizwa Hamugembe baada ya kupata taarifa kuwa nyumba yake imeanguka,” alisema Simon na kuongeza:

“Baada ya kumshusha yule abiria, ghafla hofu iliniingia nilivyoona nyumba za Hamugembe zilivyobomoka ndipo nikaanza kupiga simu ya mke wangu aliyoita muda mrefu bila kupokewa.”

Alisema muda mfupi baadaye, alipokea simu kutoka kwa mwenye nyumba wake kuwa mkewe amefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta.

Mwili wa marehemu Verdina ulisafirishwa jana kwenda kijiji cha Ruhanga Kamachumu wilayani Muleba kwa ajili ya mazishi.

Wakati Simon akimlilia mkewe, Justina Justian, mkazi wa Hamugembe alikuwa akimlilia mumewe, Jonas Petro aliyepoteza maisha katika tukio hilo.

Katika janga hilo, Justina alifanikiwa kumwokoa mtoto wake, Judith Jonas (4), aliyejeruhiwa kwa kuangukiwa na ukuta kama ilivyokuwa kwa marehemu babake.

Wilayani Karagwe Anitha Imani (34), alikuwa akimlilia mumewe, Imani Joshua (38), aliyefariki dunia kutokana na mshtuko uliosababishwa na tetemeko hilo.

“Mwezi mmoja uliopita mume wangu aligundulika kuwa na tatizo la shinikizo la damu ambalo limesababisha kifo chake baada ya tetemeko kutokea akiwa dukani. Alianguka na juhudi za kuokoa maisha yake kwa kumpeleka Hospitali ya Kahanga zilishindikana,” alisema Anitha.

Kama ilivyokuwa kwa Simon mkazi mwingine wa Karagwe, Advela Respikius alisema tukio la tetemeko limeacha simanzi na historia isiyofutika kwenye familia yake baada ya kupoteza mtoto na mjukuu aliyekuwa tumboni.

“Tumekabidhi yote mikononi mwa Mungu kwa sababu hatuna la kufanya zaidi ya kushukuru kwa kila jambo,” alisema.

Serikali yatoa ahadi

Akizungumza na waombolezaji waliojitokeza kuwaaga marehemu, Waziri Mkuu Majaliwa aliahidi kuwa Serikali inafanya tathmini kuona namna ya kuwasaidia waathirika wa tukio hilo, huku akiwaomba kuwa watulivu.

Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Saverina Mwijage aliyezungumza kwa niaba ya wabunge alishindwa kuendelea na hotuba yake akiangua kilio akisema tukio hilo limemkumbusha janga la kuzama kwa meli mv Bukoba iliyoua mamia ya Watanzania wengi wao wakiwa wakazi wa Mkoa wa Kagera.

“Nilivyoshuhudia majeneza yalivyojipanga, ghafla kumbukumbu ya vifo vya mv Bukoba imenirejea...” alisema Mwijage na kuangua kilio.

Kikao cha dharura

Meya wa Manispaa ya Bukoba, Adronikus Kalumuna alisema halmashauri hiyo imeitisha kikao cha dharura cha baraza la madiwani kujadili janga hilo na namna ya kuwasaidia waathirika.

Meya huyo alisema hilo ni tukio la kwanza kubwa kulikumba Manispaa ya Bukoba, hivyo halmashauri lazima iangalie namna bora ya kuwasaidia waathirika.

Tetemeko la ardhi lililoukumba Mkoa wa Kagera limekuwa la kwanza nchini kusababisha madhara makubwa kwa watu, nyumba na miundombinu licha ya kwamba si la kwanza kwa ukubwa katika kipimo cha ritcher.

Wakati athari hizo zilitokea, Ofisa Jiolojia Mwandamizi katika Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabrel Mbogoni amesema hadi sasa hakuna teknolojia ya kubaini tetemeko kabla halijatokea, hivyo kinachotakiwa ni wananchi kukaa tayari wakati wote.

Tetemeko hilo la kipimo cha 5.7 ritcher ni la pili baada ya lile lililotokea katika eneo la Oldoinyo Lengai mkoani Arusha mwaka 2007 likiwa na ukubwa wa 5.9 ritcher.

Mbogoni alisema ukubwa wa madhara wa tetemeko unategemea eneo linakopita, kina cha mawimbi kutoka usawa wa ardhi, ugumu wa miamba iliyopo na aina ya nyumba au miundombinu iliyopo.

Mbogoni alisema tetemeko lililotokea Oldoinyo Lengai licha ya kusababisha mpasuko wa mita nne kwenye ardhi, halikuleta athari kubwa kwa binadamu kutokana na aina ya nyumba za miti wanazojenga wenyeji, ambazo huhimili mtikisiko.

Alisema tofauti na matetemeko mengi nchini na duniani, la Kagera mawimbi yamepita umbali wa kilomita 10 tu kutoka usawa wa ardhi, umbali ambao ni mfupi na hivyo kusababisha madhara makubwa.

Tetemeko hilo limeua watu 16, kujeruhi wengine 253 na kuharibu nyumba 840 huku nyingine 1,264 zikipata nyufa.

Mtaalamu huyo alisema mahali ambako tetemeko limetokea siko wanakoweza kupata madhara tu, bali hata maeneo mengine kwa sababu husambaa

dunia nzima kupitia mawimbi chini ya ardhi.

Alisema inapotokea miamba iliyopo eneo fulani ni migumu, mawimbi hupita haraka na madhara huwa kidogo, tofauti na miamba ikiwa laini ambako kukaa na kuitingisha muda mrefu na madhara kuwa makubwa.

Kwa nini hakulitabirika?

“Si hapa tu, chukulia mfano Japan, kule matetemeko yanatokea kila siku na wana teknolojia ya juu kuliko sisi, kwa nini wasiyatabiri mapema na kuepuka?” alihoji Mbogoni.

Alisema taasisi kama Chama cha Msalaba Mwekundu na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, zinaweza kuendesha mafunzo kwa wananchi ya namna ya kujiokoa na kuokoa wengine wakati wa maafa kama hayo.

Wakati Mbogoni akisema hayo, Shirika la Jiolojia la Marekani (USGS) linabainisha uwezekano wa utoaji tahadhari mapema ambao hubaini tetemeko na kudokeza watu wa maeneo yanayoweza kuathirika kabla halijawafikia.

Mtandao wa USGS unabainisha kuwa taarifa zinazotolewa na mtambo wa kuhisi mawimbi hayo, huyawahisha kwenye kituo cha kupokea na kuyatafsiri kabla ya kurushwa mahali yalipo makazi ya watu wanaoweza kuathiriwa kupitia kompyuta au simu.

Jinsi ya kujiokoa

Mbogoni alisema, “Wananchi wachukue tahadhari kwa sababu mara nyingi tetemeko moja linapotokea yanatokea mengine yanayoweza kuwa na ukubwa unaokaribiana na ule wa mwanzo,” alisema.

Aliwataka wananchi kutokimbia ovyo wanaposikia matetemeko ya ardhi, bali wabaki wakiwa wametulia mahali palipo na usalama.

“Kwa mfano, kama uko ndani unaweza ukajificha kwenye uvungu wa meza au kitanda au ukasimama katika makutano ya kuta.

“Baada ya mtikisiko unatakiwa kutoka nje na kukaa mahali ‘peupe’,” alisema.

Aliwaonya watu kutokaa karibu na vitu virefu kama majengo, nguzo za umeme au miti kwa sababu chochote kinachoweza kuanguka.

Alisema endapo mtu ataangukiwa na vitu vizito, asitumie nguvu nyingi kujinasua wala kupiga kelele mfululizo, kwa kuwa anaweza kuishiwa nguvu kabla hajaokolewa.

Mabalozi watuma rambirambi

Mabalozi wa nchi mbalimbali nchini wametoa pole kupitia kurasa zao za Twitter akiwamo wa Norway, Hanne Marie Kaarstad aliyesema, “Pole zangu leo (jana) ni kwa wote walioathiriwa na tetemeko la ardhi huko Bukoba, Tanzania.”

Balozi wa Sweden, Katarina Rangnitt alisema; “Naomba kuwasilisha pole zangu kwa familia na rafiki wa waathirika wa tetemeko hilo Bukoba, Tanzania.”

Mwakilishi wa UN, Alvaro Rodrigues, alisema; “UN inapeleka pole zake kwa watu wote walioathiriwa na tetemeko nchini Tanzania.”

Chadema yatuma rambirambi

Wakati hali ikiwa hivyo, Chadema kimetoa salaamu za pole kwa walioathirika na tetemeko hilo.

Taarifa ya Mkuu wa Idara ya Habari ya chama hicho, Tumaini Makene ilitoa wito kwa Watanzania wote, wakiwamo viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali, wabunge, madiwani, kushirikiana kuwasaidia waathirika wa tukio hilo katika kipindi hiki.

CUF yaguswa

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro alituma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa wa marehemu wa maafa hayo.

“Kwa niaba ya chama natoa pole kwa ndugu wote, jamaa na marafiki, wawe na subira na uvumilivu katika kipindi hiki, majeruhi wote tunawaombea wapone haraka ili warejee katika majukumu yao ya kila siku,” alisema Mtatiro.

No comments: