Advertisements

Tuesday, September 13, 2016

WASOMI CUF WAMJIA JUU PROFESA LIPUMBA

JUMUIYA ya Vyuo Vikuu ya Chama cha Wananchi (CUF) tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imemshauri aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba kuachana na chama hicho.
Taarifa iliyotolewa leo na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Jidawi Chande imesema kuna mpango wa kuvuruga chama hicho unaofanywa na Profesa Lipumba na kumuonya kuacha kujidhalilisha na kujishushia heshima aliyojijengea miaka mingi katika jamii ya ndani na nje ya nchi.
Iliongeza kuwa anachokifanya Profesa Lipumba, si tu kwamba anajidhalilisha au kujifedhehesha tu, bali anaidhalilisha jamii nzima ya wasomi wenye hadhi kama yeye.
“Inasikitisha sana kuona mtu kama Profesa Lipumba aliyewahi kushika wadhifa wa uenyekiti wa chama Taifa, leo anakuwa mstari wa mbele kukivuruga na kukigawa chama.Tunamtaka Lipumba aheshimu maamuzi halali ya chama na afuate Katiba kwa maslahi ya chama na si kwa maslahi yake binafsi,” amesema.

Taarifa hiyo pia imelaani fujo na kauli za kibaguzi, zinazoendelea kutolewa na Profesa Lipumba na baadhi ya wafuasi wake, kama ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Magdalena Sakaya kuwa chama kina mpasuko wa Bara na Visiwani.
Taarifa hiyo pia imeliomba Baraza Kuu na mamlaka nyingine za chama hicho, kuendelea kufanya uamuzi mgumu ya kukijenga chama pale inapobidi, kwani misingi na taratibu za chama lazima zifuatwe.

No comments: