Advertisements

Wednesday, October 26, 2016

Askari ‘fake’ anaswa akitapeli

pg-1-3
Na JUDITH NYANGE-MWANZA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Ahmed Gabo mkazi wa Bugarika, Kata ya Pamba wilayani Nyamagana, kwa tuhuma za kuiba, kuvaa sare za jeshi hilo pamoja na kujifanya askari.

Akizungumzia tukio hilo juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 20, mwaka huu saa 5:30 asubuhi baada ya askari Issa Masoud, aliyekuwa doria kupokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu uwepo wa askari wanayemtilia mashaka.

Alisema wananchi hao walimtilia mashaka askari huyo kutokana na namna alivyokuwa amevalia sare za Jeshi la Polisi, hali aliyokuwa nayo pamoja na vitendo vya ubabaishaji walivyookuwa akivifanya kuwa si vya kimaadili kinyume na maadili ya jeshi hilo.

“Huyo kijana hata ukimwangalia jinsi alivyovaa kofia yake, filimbi hana, mkanda ameugeuza, viatu alivyovaa si vya kiaskari na ndani ya suruali alikuwa amevalia nguo nyingine.

“Tulipomhoji alisema ni kweli hizo sare si zake, yeye si askari wa Jeshi la Polisi wala hajawahi kupita katika mafunzo ya jeshi lolote lile hapa nchini bali hizo nguo alizikuta katika begi la muumini aliloliiba msikitini alipokuwa akisali.

“Yule muumini aliyeibiwa begi lake msikitini ni askari wa hapa hapa mkoani na aliibiwa siku nne zilizopita, huyu ni miongoni mwa wale vijana wenye tabia za udokozi katika nyumba za ibada,” alisema Msangi.

Kamanda Msangi alisema baada ya kukamilika kwa taratibu za jeshi hilo, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani na amewataka wananchi kuwa makini na watu wote na pindi watakapoona askari anayefanya vitendo vilivyo kinyume na maadili ya jeshi hilo watoe taarifa na watachukuliwa hatua zinazostahili.

Mtanzania

No comments: