Diwani wa Kata ya Kaloleni eilayani Kiteto mkoani Manyara, Christopher Parmet amenusurika kufa baada ya kuchomwa mkuki na wafugaji wa eneo hilo wakati akifukuza mifugo iliyovamia shamba lake.
Diwani huyo ambaye ni katibu mwenezi wa CCM wilayani Kiteto na katibu wa mbunge wa jimbo hilo, Emmanuel Papian na hivi sasa amelazwa kwenye hospitali ya wilaya hiyo akipatiwa matibabu.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Papian alisema afya ya Parmet inaendelea vizuri baada ya kuongezewa damu kwani alivuja damu nyingi baada ya kuchomwa mkuki kiganjani.
Papian alisema diwani huyo alijeruhiwa jana jioni alipofika shambani kwake kwa ajili ya kuwalipa vibarua wake watatu ambao pia walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alisema yupo nje ya nchi hivyo asingeweza kuzungumza tukio hilo.
Mganga mkuu wa wilaya hiyo Dk Lupembe alithibitisha majeruhi hao kulazwa kwenye hospitali ya wilaya hiyo na kuwa wanaendelea kupata matibabu.
No comments:
Post a Comment