Advertisements

Wednesday, October 12, 2016

MASHAHIDI KESI YA ESTER BULAYA WAPUNGUZWA

Mashahidi wa pande zote mbili katika kesi ya kupinga ushindi wa Ester Bulaya katika uchaguzi wa mbunge wa Jimbo la Bunda wamepunguzwa na kuweka mazingira ya shauri hilo kutolewa uamuzi mapema.

Katika kesi hiyo iliyo Mahakama Kuu, Bulaya ataanza kujitetea kwa kuita shahidi mmoja baada ya shahidi wa tatu wa upande wa wawasilisha maombi, Steven Wasira kumaliza kutoa ushahidi juzi.

Upande wa Bulaya, ambaye aligombea kwa tiketi ya Chadema na kumbwaga mwanasiasa mzoefu, Steven Wasira, umedai kuwa umeamua kubakia na shahidi mmoja kutokana na waliowasilisha maombi kuwa na ushahidi dhaifu.

Wakati wajibu maombi wakisema hayo, upande wa wanaopinga ushindi wa Bulaya wametangaza kufunga ushahidi baada ya kuita mahakamani mashahidi watatu pekee tofauti na maelezo ya awali kuwa wangeita watu 15.

Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu anayemwakilisha Bulaya ambaye ni mdaiwa wa kwanza katika shauri hilo namba moja la mwaka 2015, aliieleza mahakama kuwa anakusudia kuita mahakamani shahidi mmoja.

“Ingawa ushahidi uliowasilishwa mahakamani na upande wa waleta maombi ni dhaifu na hauna nguvu kisheria kiasi cha awali tufikiria kutoita shahidi, tumeona ni vyema kuita shahidi mmoja kujenga hoja zetu za kuishawishi mahakama kutupilia mbali shauri hili,” alisema Lissu.

Maelezo hayo ya Lissu ni tofauti na yale aliyoyatoa juzi wakati shauri hilo lilipoahirishwa kwamba asingeita shahidi yeyote kutokana na ushahidi wa wadai kuwa dhaifu na kukosa mashiko mbele ya macho ya sheria.

Waliowasilisha maombi ya kutaka matokeo hayo ya ubunge yatenguliwe ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila ambao ni wapigakura wa Bunda.

Wakili anayewakilisha waliowasilisha maombi hayo, Constantine Mutalemwa amesema wameamua kufunga ushahidi baada ya kuridhika na ushahidi ambao umeshatolewa na mashahidi watatu. 

Awali, wakili huyo aliieleza mahakama kuwa upande huo ungeita mashahidi 15 kabla ya kurekebisha orodha hiyo na kubakiza 12.

Wakili Angela Kushagala anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na msimamizi wa uchaguzi ambao ni wajibu maombi namba mbili na tatu, aliieleza mahakama kuwa wanakusudia kuita mashahidi wawili.

Wakati huohuo, Lissu ameiomba mahakama kuondoa ombi lao la awali la kutoendelea na usikilizwaji wa shauri hilo tofauti na awali walipotaka ilitupilie mbali kwa madai kuwa hakuna kesi ya kujibu. 

Lissu alisema upande wa utetezi umepitia upya maombi yao na kugundua kuwa upo uwezekano wa shauri hilo kuchukua muda mrefu iwapo wataendelea kushikilia msimamo wao wa kutaka litupwe.

No comments: