Advertisements

Wednesday, October 19, 2016

Mchakato wa kuanzisha Viza ya Pamoja ya Utalii katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kaimu Mkurugenzi, Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Bernard Haule (kulia) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkuu, wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Robi Bwiru
Kaimu Mkurugenzi, Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Bw. Bernard Haule akiongea na waandishi
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
 

Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

 

                20 KIVUKONI FRONT,
                           P.O. BOX 9000,
                  11466 DAR ES SALAAM, 
                                    Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mchakato wa kuanzisha Viza ya Pamoja ya Utalii katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ndugu wanahabari:
Wiki iliyopita baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii ya hapa nchini na nje ya nchi iliandika taarifa kuhusu Tanzania kujitoa au kugomea utaratibu wa visa ya pamoja ya utalii (Single Tourist Visa) wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Kufuatia taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekuwa ikipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kutaka kufahamu ukweli wa jambo hilo. Hivyo, Wizara imeona leo itoe taarifa rasmi kufafanua namna ya mchakato wa uanzishwaji wa viza ya pamoja ya utalii ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unavyoendelea.
Suala la Uanzishwaji wa Viza ya Pamoja ya Utalii kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki bado liko katika majadiliano ya Nchi Wanachama kupitia Vikao vya Sekta ya Utalii na Wanyamapori. Katika kufanikisha azma hii,  Baraza la Kisekta la Mawaziri wa  Maliasili na Usimamizi wa Wanyamapori uliofanyika  tarehe 1 Novemba 2008 liliunda Kikosi Kazi kwa ajili ya kufanya  utafiti kwa lengo la kubainisha mahitaji na utayari wa Nchi wanachama juu ya kuanzisha  Viza ya Pamoja ya Utalii.  Utafiti uliofanyika mwaka 2010, ulibainisha masuala muhimu yafuatayo ya kuzingatiwa kabla ya kuanzishwa kwa Viza ya Pamoja ya Utalii:
a)    Kurazinisha  (harmonization) sheria za Viza za Nchi Wanachama;
b)     Idara ya Uhamiaji  kuanzisha Mfumo  wa  kudhibiti Usalama;
c)     Utoaji wa Viza kuwa wa kielektroniki;
d)   Kuwepo kwa mfumo wa ukusanyaji na ugawanyaji wa mapato pamoja na namna ya kulipa;
e)     Kuwepo kwa maafisa uhamiaji katika kila ofisi za ubalozi;
f)      Kujenga uwezo wa watumishi kwenye suala la  mfumo wa kieletroniki  wa utoaji wa viza ya pamoja ya Utalii.
Kufuatia matokeo ya utafiti huo, Mkutano wa 5 wa Baraza  la Kisekta la Mawaziri wa Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori  uliofanyika  mwezi Julai 2013  jijini Bujumbura, Burundi pamoja na mambo mengine uliagiza kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kitajumuisha wataalamu kutoka Taasisi za Uhamiaji, Utalii, Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tehama, Usalama, na Sheria katika nchi wanachama ili  kuandaa mpango kazi  na  kushughulikia masuala yote ambayo  yatajitokeza kuhusiana  na uanzishwaji wa  Viza ya Pamoja ya Utalii. Hata hivyo, kabla ya utekelezaji wa maagizo hayo, Nchi za Uganda, Kenya na Rwanda zilianzisha  Viza ya Pamoja ya Utalii baina yao nje ya vikao vya Jumuiya.
Ni vema ikaeleweka kwa umma wa Watanzania na Afrika Mashariki kwa Ujumla kuwa kwa kuzingatia Mfumo wa Maamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao ni wa kukubaliana kwa pamoja (consensus) hakuna Mfumo wowote wa uanzishwaji wa Visa ya Pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioanzishwa. Hii inamaanisha kuwa hakuna Visa ya Pamoja ya Utalii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokubalika. Kwa mantiki hiyo, taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari hazina ukweli wowote na zilikuwa na lengo la kuichafua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawawahakikishia umma wa Tanzania kuwa itaendelea kuheshimu maamuzi ya vikao halali vya Jumuiya na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha visa ya pamoja ya utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. 
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 18 Oktoba  2016.

1 comment:

Anonymous said...

hapa tutazidiwa kete na wakenya kama kawaida.....