ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 11, 2016

POLISI DAR WANASA MTANDAO WA ‘SCORPION’

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro akionesha bunduki aina ya Mark IV waliyoikamata kwa watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi wakati wa majibizano ya risasi na polisi, katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. (Picha na Fadhili Akida).

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imefanya operesheni katika maeneo ya katikati na pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam na kuwakamata watuhumiwa 87 wa makosa mbalimbali, wakiwemo waliokuwa kwenye mtandao wa uhalifu wa mkazi wa Machimbo Yombo jijini Dar es Salaam, Salum Njwele (34) maarufu kama ‘Scorpion’.
Njwele alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mwishoni mwa wiki, kujibu mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumtoboa macho yote mawili Said Mrisho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi Simon Sirro alisema watuhumiwa wengine wanadaiwa kuvunja nyumba na kuiba na wengine walipatikana na gongo lita 148, bangi kete 95 na puli 48.
Alisema watuhumiwa hao, wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Mbagala, Buguruni, Kiluvya, Gongo la Mboto, Tandika, Ukonga, Banana, Kunduchi, Keko, Kawe.
“Watuhumiwa hao walipatikana na makosa mbalimbali yakiwemo kuvunja nyumba usiku na kuiba maarufu 10 ndani 10 nje, kuvuta na kuuza bhangi, kuuza na kunywa gongo,
kupiga debe, uzembe na uzururaji,” alisema Kamanda Sirro.
Katika tukio lingine, watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamekamatwa wakiwa na silaha aina ya MARK IV ikiwa imekatwa kitako chake.
Watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 10 mwaka huu saa 3:30 asubuhi huko maeneo ya Vingunguti wakiwa na pikipiki yenye namba MC 787 BEP aina ya Boxer ikiwa kwenye jaribio la kufanya tukio la ujambazi katika eneo la viwandani.
Alisema Kikosi Maalumu cha Kupambana na ujambazi wa kutumia silaha kiliwafuatilia na watuhumiwa hao baada ya kuona hivyo walianza kufyatua risasi hovyo kuelekea kwa askari na ndipo askari walijibu mashambulizi na kuwajeruhi wote wawili na kuchukua silaha hiyo, ikiwa na risasi tano kwenye magazine moja tayari kwa kufyatuliwa.
Alisema taarifa za awali zimebaini kwamba watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi, walikuwa wamejipanga kuvamia kiwanda kimojawapo maeneo ya Vingunguti. Alisema watuhumiwa hao walikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu hali zao zikiwa mbaya kutokana na majeraha ya risasi.
Alisema upelelezi zaidi wa tukio hilo unaendelea.

CHANZO: HABARI LEO

No comments: