Advertisements

Friday, October 28, 2016

RC TABORA ATANGAZA VITA KWA WATUMIAJI WA DAWA ZA KULEVYA ZIKIWEMO HABARI NYINGINE KUTOKA TABORA

Image result for MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri

Na Mussa Mbeho,Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameonya watu wote wanaojihusisha na uuzaji au utumiaji wa madawa ya kulevya mkoani humo na kuahidi kuwa kiama chao kimefika.

Mwanri ametoa onyo hilo katika mikutano mbalimbali ya hadhara aliyoifanya wiki hii katika kata za Isevya, Gongoni, Misha, Ndevelwa na katika mkutano wake na Wenyeviti na Watendaji wote serikali za mitaa zilizoko katika manispaa ya Tabora.

Alisema kitendo cha kuongezeka kwa watumiaji wa madawa hayo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo na hususani maeneo ya Isevya, Ipuli, Chemchem na Mwinyi katika manispaa hiyo kinahatarisha sana maisha ya vijana walio wengi kwani wataendelea kuambukizana tabia hiyo.

Alisema vijana wengi wanashindwa kutumia nguvu zao katika uzalishaji ili kujipatia kipato na badala yake kujihusisha na vitendo visivyofaa vya uvutaji wa bangi, mirungi, kokein na madawa mengine yanayoathiri maisha yao.


Aliongeza kuwa msako wa kuwabaini wanaojihusha na biashara hiyo haramu katika mkoa huo utaanza mara moja.

Alimwagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa ACP Hamis Issa kuanza kuwasaka wahusika wote wa vitendo hivyo haraka iwezekanavyo sambamba na kukomesha kabisa biashara hiyo.

Mwanri alisema vita hiyo itasaidia kuokoa maisha ya watu wengi kwani wengi wao kwa sasa wamekuwa kama mazuzu, wasioweza kufanya jambo lolote za uzalishaji hivyo akatoa agizo kwa madiwani, wenyeviti na watendaji wa mitaa, vijiji na kata kutoa ushirikiano wa hali ya juu
ili kufankisha mikakati hiyo.

Alibainisha kuwa vita hiyo itaenda sambamba na kuwasaka wahalifu wote wanaojihusisha na ujambazi,wizi wa kutumia silaha,utapeli,rushwa,wanaowapa ujauzito
watoto wa shule pamoja na wale wanaomiliki sihaha kinyume cha taratibu.

Aidha aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakisha vinaimarisha doria katika maeneo mbalimbali ya manispaa ya Tabora hiyo ili kukabiliana na vitendo hivyo ikiwemo kuwakamata watumiaji wote wa madawa ya kulevya na kuwaburuza mahakani watakaobainika.

Kamanda Seleman aliwaambia wananchi wa kata hizo kuwa utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa unaanza mara moja na kuwataka wahusika wote kuacha mara moja kujihusisha na vitendo hivyo kwani siku zao zinahesabika.

Aidha aliwataka madiwani, watendaji na wenyeviti wa mitaa kutoa ushirikano kwa jeshi hilo ili liweze kufanikisha zoezi la kuwatia hatiani wahusika wote katika maeneo yao kwani wasipotoa ushirikiano wananchi wao wataendelea kuteseka.

JPM AIBUKIA SEMINA YA MADIWANI TABORA.

Na Mussa Mbeho,Tabora.

KAULI ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dr.John Pombe Magufuli ya kudai risti unaponunua au kuuza kitu chochote
imechukua sura mpya baada ya madiwani wa manispaa ya Tabora kuhoji
sababu zinazokwamisha halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo ya
ukusanyaji mapato.

Akitoa mada juu ya ukusanyaji mapato Mratibu wa semina hiyo
iliyohusisha madiwani na wakuu wote wa idara katika halmashauri hiyo
Hamis Mjanja alisema bila kudai risiti halmashauri hiyo haiwezi kupata
mapato ya kutosha kwani mapato yao mengi yanaishia mifukoni mwa watu.

Alisema suala la kuongeza mapato na ufanisi wa zoezi zima la
ukusanyaji mapato linategemea weledi watendaji wa halmashauri na
umakini wa madiwani katika kusimamia shughuli hiyo hivyo akawataka
madiwani kuamka usingizini na kuisimamia halmashauri yao.

Mkuu wa Mkoa huo Aggrey Mwanry alisema wajibu wa madiwani na wakuu wa
idara ni kutoa elimu na kuhimiza wananchi kudai risiti na kutoa risiti
wanapofanya
biashara zao ili kuwezesha halmashauri hiyo kukusanya mapato kwa asilimia 100.

'Ninyi madiwani mna dhamana kubwa sana katika suala zima la ukusanyaji
mapato, na hili mnapaswa kulisimamia ipasavyo ili kutekeleza kwa
vitendo dhamira ya Rais wetu Dr John Pombe Magufuli', aliongeza.

Hoja hiyo ilionekana kuwagusa madiwani hao huku baadhi wakiapa
kuchukua hatua na kuwa wakali sana kwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo na
watendaji wake wote katika halmashauri hiyo ikiwemo wahusika wote wa
kukusanya ushuru katika vyanzo mbalimbali vya mapato ya halmashauri
hiyo.

Akizungumzia namna madiwani wanavyoweza kuchochea ukusanyaji wa
mapato Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mwl.Queen Mlozi alisema madiwani
wana nafasi kubwa ya kufanikisha zoezi hilo kwa kuwa muda mwingi wapo
karibu na wananchi.

Alisema kama madiwani watatambua wajibu wao na kusimamia shughuli zote
za maendeleo katika kata zao halmashauri itakusanya mapato kwa
asilimia pasipo shaka ya upotevu wa mapato.

Aliongeza kuwa suala la kupaisha uchumi katika kata zao ni kutoa hamasa
kwa wananchi wao kuchangia huduma mbalimbali za kijamii na kuomba
risti wakati wanapo nunua bidhaa mbalimbali kutoka madukani na
gulioni.

RC TABORA ASIKITISHWA WAJAWAZITO KULALA 4 KITANDA KIMOJA

Na Mussa Mbeho, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametembelea wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa Kitete mkoani Tabora na kukuta hali ya kusikitisha
sana kwa wajawazito na wazazi waliojifungua kulala watatu au wanne
katika kitanda kimoja.

Akionesha kusononeshwa na hali hiyo, alieleza kuwa kitendo cha
wajawazito au wazazi kulala mzungu wanne tena watatu watatu au wanne
ni hatari sana kwa afya ya mama na mtoto.

‘Hii hali haikubaliki, ni lazima jitihada za makusudi zifanyike ili
kuwasaidia mama zetu hawa na watoto’, aliongeza.

Alimwagiza Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dr.Nasoro Kaponta
kwa kushirikiana na Uongozi wa Hospitali hiyo kufanya kila
liwezekanalo ili kutatua changamoto hiyo kwani ni hatari kwa afya ya
mama na mtoto.

Aidha aliuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha akinamama
wajawazito wote wanaoenda kujifungua hospitalini hapo hawadaiwi fedha
za vifaa vya kujifugulia kwa kuwa serikali ilishaagiza wasitozwe
gharama yoyote.

Dr Nasoro alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa msongamano huo unatokana na
ufinyu wa nafasi katika wodi hiyo ndio maana wanashindwa kuongeza
vitanda na kuongeza kuwa uchache wa zahanati na hospitali za wilaya
pia unachangia kero hiyo.

Msimamizi wa huduma za akinamama katika wodi hiyo Bi.Eliwampuka Mbwana
alieleza kuwa kwa wastani akinamama 25-30 huja kujifungulia
hospitalini hapo kila siku kutokana na ukosefu wa hospitali za wilaya
ndio maana kuna msongamano huo.

Ili kupunguza msonganano huo, Mhudumu wa wodi hiyo Eva Isaya alishauri
zahanati na vituo vya afya vilivyopo katika manispaa ya Tabora
vitumike kujifungulia na hopsitali ya Kitete ihudumie wale watakaopewa
rufaa tu.

Katika ziara hiyo Mwanri alikabidhi mashuka 38 yenye thamani ya sh
500,000/- katika wodi hiyo yaliyotolewa na wanafunzi wa Chuo cha
Utumishi wa Umma tawi la Tabora ambapo pia walitoa msaada wa chakula,
mavazi na vitu vinginevyo vyote vikiwa na thamani ya sh mil 1.5 kwa
kituo cha kulea wazee kilichoko Ipuli.
.
Mkuu wa wilaya ya Tabora Mwalimu Queen Mlozi alipongeza uongozi na
wanafunzi wa Chuo hicho kwa moyo wao wa kizalendo wa kuunga mkono
jitihada zinazofanywa na serikali katika kusaidia jamii kwa kuwa
serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu.


RC TABORA AAGIZA MLINZI ALIPWE MISHAHARA YAKE YA MIEZI 22

Na Mussa Mbeho,Tabora

MKUU wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri ya Manispaa ya Tabora Bosco Ndunguru kulipa malimbikizo
yote ya mishahara ya miezi 22 kiasi cha sh 660,000/- ya mlinzi wa
shule ya msingi Ndevelwa, Agustin Paul (58), badala ya kuendelea
kumpiga dana dana.

Agizo hilo limetolewa juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika kata ya Ndevelwa iliyopo katika manispaa hiyo baada ya Mkuu wa
Mkoa kuhutubia wananchi na kutoa nafasi ya kuuliza maswali au kueleza
kero zao.

Baada ya mlinzi huyo kutoa malalamiko yake, Mkuu wa Mkoa alimwita
Mtendaji wa Kata hiyo Hamis Kasonta ili kutoa ufafanuzi wa madai hayo
ambapo alikiri mlinzi huyo kutolipwa mishahara yake na uongozi wa
shule hiyo ya serikali kwa miezi 22.

Diwani wa kata hiyo Seleman Maganga alieleza kuwa awali mlinzi huyo
alikuwa anapata mshahara wake kama kawaida, wakati mwingine analipwa
kidogo kidogo lakini baadae wakaacha kumlipa kwa kisingizio cha
serikali ya kijiji kutopokea fedha yoyote ya uwezeshwaji kutoka
halmashauri ya manispaa.

Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo Chatta Lukela alipoitwa kutoa
ufafanuzi alisema suala hilo lipo chini ya uongozi wa shule na
serikali ya kijiji ndio inayopaswa kumlipa mishahara yake yote mlinzi
huyo.

Baada ya maelezo hayo Mwanri alisema kwa kuwa serikali ya kijiji
haijapata mgao wa fedha za uwezeshwaji kutoka halmashauri ya
manispaa, deni hilo lilipwe moja kwa moja kutoka Ofisi ya Mkurugenzi
wa manispaa na utaratibu wa malipo uanze mara moja hata kama ni kidogo
kidogo.
Ili kuhakikisha deni hilo linalipwa, RC alimwagiza Mkuu wa wilaya ya
Tabora Mwalimu Queen Mlozi kulisimamia na kumpa mrejesho wa kufanyika
kwa malipo hayo.

Akiongea kwa masikitiko mlinzi huyo Agustino Paul (58) mwenye watoto 2
alieleza kuwa alianza kazi hiyo mwaka 2014 kwa makubaliano ya kulipwa
sh 30,000/- kwa mwezi, alilipwa miezi kadhaa lakini baada ya hapo
hakulipwa tena ila aliambiwa avumilie hela zikipatikana atalipwa.

‘Baada ya kukaa miezi kumi bila kulipwa niliamua kuacha kazi lakini
baadae wakanirudisha tena huku wakiahidi kunilipa kidogo kidogo mpaka
deni liishe, ahadi hiyo haijatekelezwa hadi leo na bado niko kazini’,
aliongeza.

No comments: