ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, October 30, 2016

SIMBA MWENDO KASI

Kikosi cha Simba
SIMBA imezidi kujikita kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga Mwadui ya Shinyanga mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage.

Ushindi huo unaifanya timu ya kocha Joseph Omog ifikishe pointi 32 baada ya kushuka dimbani mara 12. Timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi imeshinda mechi 12 na kutoka sare mara mbili bila ya kupoteza mchezo hata mmoja hadi sasa.

Aidha, matokeo hayo yanaifanya Simba ijinafasi kileleni mwa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 32, mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 24 za mechi 11.

Yanga wenyewe leo wanashuka kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuikaribisha Mbao FC ya Mwanza katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo wa jana, hadi mapumziko, Simba walikuwa wanaongoza kwa mabao 2-0, yote yakifungwa na viungo wapya waliosajiliwa kutoka Mtibwa Sugar. Mohammed ‘Mo’ Ibrahim alianza kufunga dakika ya 32 baada ya kumtoka beki wa Mwadui kufuatia pasi safi ya kiungo mwenzake, Mwinyi Kazimoto.

Mo Ibrahim alimtengenezea Kichuya aliyeifungia Simba bao la pili katika dakika ya 45, hilo likiwa bao lake la nane msimu huu katika Ligi Kuu.

Kipindi cha pili, Simba walirudi na moto ule ule na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 50 lililowekwa kimiani na Mo Ibrahim tena akimalizia pasi ya mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Ame Ali.

Kikosi cha Simba: Vincent Angban, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Method Mwanjali, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Muzamil Yassin, Mwinyi Kazimoto/Ibrahim Hajib (dk46), Laudit Mavugo, Shizza Kichuya/ Said Ndemla (dk66) na Mohamed ‘Mo’ Ibrahim.

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara, Toto Africans ya Mwanza jana iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Mabao ya Toto yalifungwa na Waziri Junior, Hamim Abdul, Omege Seme huku yale ya Mtibwa Sugar yalipachikwa na Kelvin Friday.

Kutoka Mbeya, timu ya Mbeya City imefanya kweli baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Majimaji ya Songea katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Yanga wenyewe leo watakuwa na kibarua kigumu wakati watakapokuwa wakisaka pointi tatu kutoka kwa Mbao FC ambao waliitoa jasho Simba na kuambulia bao 1-0 kwenye uwanja huo huo wa Uhuru.

Yanga wenyewe wana pointi 24 baada ya kucheza mechi 11, hivyo wanahitaji pointi tatu ili waweze kuisogelea Simba, ambayo msimu huu inaonekana kama ya mwendo kasi, ambayo kuishika ni shida.

Katika mechi zingine; JKT Ruvu iliutumia vizuri uwanja wao baada ya kuifunga Ndanda FC kwa bao 1-0 huku bao hilo pekee likifungwa na Atupele Green, na African Lyon ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Prisons.

HABARI LEO

No comments: