Advertisements

Friday, October 14, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nje Tanzania's profile photo

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Mfalme wa Morocco nchini Tanzania
Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini kuanzia tarehe 19 hadi 23 Oktoba, 2016.
Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza zaidi uhusiano kati ya Tanzania na Morocco hususan katika masuala ya  kiuchumi na kibiashara kwa faida ya nchi hizi mbili na watu wake.
Vilevile, Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco atatumia fursa ya ziara hiyo kutembelea Zanzibar na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kujionea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Hata hivyo, ziara hiyo ambayo imejikita zaidi katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara haitaathiri msimamo wa Tanzania katika mgogoro unaoendelea kati ya Morocco na Sahara Magharibi.

Msimamo wa Tanzania ambao umekuwa ukisimamiwa na Awamu zote za uongozi zilizopita na Awamu hii, upo sambasamba na ule wa Umoja wa Afrika (AU) unaoutaka Umoja wa Mataifa (UN) ambao ndio wamepewa jukumu la kusimamia mgogoro huo, kuongeza kasi katika kuutatua na kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.
Tarehe 20 Oktoba, 2016 Mhe. Mfalme Mohammed wa VI atakutana kwa mazungumzo ya faragha na Mhe. Rais Magufuli  Ikulu yakifuatiwa na mazungumzo rasmi kati yao na wajumbe waliofuatana nao.
Mhe. Mfalme Mohammed VI pamoja na kutembelea Tanzania, pia atatembelea Rwanda, Ethiopia na Kenya.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 13 Oktoba, 2016.

No comments: