Advertisements

Wednesday, October 12, 2016

UMMILIKI: Hatima ukodishwaji Yanga Okt 23

Image result for YANGA
By Imani Makongoro, Fredrick Nwaka, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati mjadala wa kukodishwa Yanga kwa miaka 10 ukishika kasi, uongozi wa klabu hiyo umesema uamuzi wa mwisho utatolewa kwenye mkutano mkuu wa Oktoba 23.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit alisema mkutano mkuu wa Oktoba 23 ndiyo utaamua hatima ya kukodishwa kwa klabu hiyo au la.

“Ajenda ya kukodisha klabu itapitishwa na mkutano mkuu ujao, akidi ikitimia kwa mujibu wa katiba yetu zoezi hilo litafanyika,” alisema Baraka na kufafanua.

“Yanga ‘inadili’ na wanachama wanaolipia kadi zao, wapo wenye kadi, lakini hawazilipii hao siwezi kuwazungumzia kwa sababu si wanachama hai.

“Ukizungumzia wanachama wa Yanga kiukweli ni wengi, ni zaidi ya 10,000, lakini wote hao si ‘active’ (hai).

Katibu huyo alisema mkutano mkuu wa dharura uliopita ulikuwa na wanachama 1,800 wanaolipia ada ya kadi zao za uanachama.

“Mambo mengine ni ya kiofisi, hayapaswi kutangazwa, lakini mkutano wetu mkuu wa dharura uliopita ulikuwa na wanachama 1,800 waliokuwa hai,” aliongeza Baraka.

TFF yaingilia kati

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeibuka na kusema haliutambui mkataba wa ukodishwaji wa klabu kutokana na vipengele vitano vitakavyokuwa msingi wa kukodishwa kwa klabu hiyo iliyosajiliwa mwaka 1935.

Katibu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema mchakato wa uwekezaji unaofanywa na klabu za Simba na Yanga, huku akijikita zaidi kuzungumzia suala la Yanga, ambayo mkataba wa kukodishwa umeshatangazwa.

Mwesigwa alisema baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari, TFF ilipokea malalamiko kutoka kwa wanachama na wazee wa Yanga wakilalamikia uamuzi uliofanywa na kikao cha dharura kilichofanyika Agosti 6.

“Mfumo wa uendeshaji wa timu na uongozi hali iliyoifanya TFF kutokaa kimya katika jambo linalohusu mwanachama wake na kuutaka uongozi wa Yanga kuwasilisha nakala ya barua kuthibitisha kukodishwa klabu hiyo.

“Mchezo wa soka unabadilika kila siku na uwekezaji ni matokeo ya taratibu zinazowekwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu.

“Tuliposikia Simba na Yanga zinataka kubadilisha mfumo wao wa uendeshaji, tukaziandikia barua ili tukutane na kuzungumza, Simba walikubali, lakini Yanga hawakutujibu.

“Muda umekwenda na sasa tunasikia Yanga wamesaini mkataba wa kukodishwa. Suala la umiliki na uendeshaji wa klabu lipo katika kanuni za leseni za klabu na linatambuliwa kuanzia Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa), CAF (Shirikisho la Soka Afrika) na TFF. Ni lazima uwepo utaratibu ulio wazi juu mchakato huu,” alisema Mwesigwa.

“Shirikisho limepokea malalamiko na tumemwandikia barua kaimu katibu mkuu wa Yanga kuomba nakala ya mkataba wa klabu hiyo kukodishwa.

“Hatupingi mfumo wa uwekezaji, lakini mchakato huo uende sambamba na taratibu za soka. TFF bado inaitambua klabu ya Yanga yenye mwenyekiti, katibu na sekretarieti yake, lakini haitambui mkataba huo,” alisema Mwesigwa.

Wadau wanasemaje?

Mchezaji wa zamani wa mwanachama wa klabu hiyo, Ramadhan Kampira alisema TFF imechukua msimamo sahihi unaozingatia masilahi ya soka na siyo ya mtu binafsi.

“Naipongeza TFF wamechukua msimamo sahihi kwa kuzingatia kanuni na taratibu, masilahi ya kikundi cha watu yasitumike kuiletea matatizo klabu ya Yanga. Kuna watu wengi wenye mtazamo hasi na jambo hili,” alisema Kampila.

Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Ayoub Nyenzi, ambaye alivuliwa wadhifa wake na kufukuzwa uanachama katika kikao cha dharura cha Agosti 6, alisema TFF inatakiwa kutambua mkutano ule kama ulikuwa halali au la kabla ya kuendelea na mambo mengine.

“Hayo mambo yanayoendelea yametoka kwenye mkutano wa dharura ulioitishwa Agosti 6. Mimi na wenzangu (Salum Mkemi na Hashim Abdallah) tunapinga mkutano ule na uamuzi ulioafikiwa kwa kuwa mkutano ulikuwa batili. TFF ingesikiliza kwanza malalamiko yetu,” alisema Nyenzi.

No comments: