ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 5, 2016

WAZAZI WATAKAOWAOZESHA WATOTO WAO BADALA YA KUWAPELEKA SHULE WILAYANI NZEGA KUKIONA CHA MTEMAKUNDE

 Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe Gedfrey Ngupula

Na Mathias Canal, Tabora

Tatizo la Mimba za utotoni na kuozesha wanafunzi katika umri mdogo limetajwa kuwa ni kikwazo kikubwa katika jamii kwani watoto wa kike wananyimwa haki ya kupata elimu ili kujikwamua na fikra mpya katika uchumi na namna ya kuwa na familia bora na endelevu katika kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe Gedfrey Ngupula Ameyabainisha hayo katika mahojiano maalumu na Mwandishi wa Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com kuhusu mikakati ya kukabiliana na mimba za utotoni pamoja na wazazi kuwaachisha masomo watoto wao wa kike ili kuwaozesha kwa fikra potofu za kupata mali zikiwemo Ng'ombe na fedha.

Dc Ngulupa amesema kuwa jambo hilo limepigwa marufuku na serikali lakini bado linafanyika kimya kimya katika maeneo mbalimbali nchini hivyo endapo atabaini wazazi wanaofanya hivyo kuanzia sasa watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania.

Amewataka wananchi kuachana na dhana hiyo potofu ya kujipatia mali kupitia watoto wao wa kike badala yake wahakikishe wanafanya kazi kwa bidii ikiwemo kuwekeza zaidi katika elimu, kilimo na ufugaji kwani ndio njia nyepesi katika mafanikio kuliko kuwa na mtazamo hasi.

Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo walimu katika utendaji wao ikiwa ni pamoja na uduni wa mishahara, Kitolipwa stahiki zao baada ya kupandishwa madaraja Dc Ngupula alisema kuwa serikali kuu kupitia Mhe Rais Dkt John Magufuli aliahidi neema kwa watumishi wote ikiwemo sekta ya afya na elimu hivyo amewataka walimu kuwa wavumilivu katika kipindi hiki Rais anapopitia ripoti ya watumishi hewa aliyokabidhiwa hivi karibuni ili kujiridhisha na kuruhusu kuajiriwa kwa watumishi wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipa madai ya walimu ambayo yana haki kimsingi na yamekuwa ya muda mrefu.

Hata hivyo Dc Ngupula amesema kuwa walimu wakuu wanapaswa kuendelea kutoa taarifa za ukweli kuhusiana na upungufu wa madawati ili kukabiliana na kadhia hiyo ambayo imekuwa ni tatizo kubwa katika shule mbalimbali nchini.

Alisema kuwa endapo uchunguzi anaoendelea kuufanya utabaini kuwa kuna upungufu wa madawati ilihali tayari awali walishatoa taarifa kuwa hakuna kadhia hiyo watachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo ili kutoa fundishi kwa watumishi wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega wanaishi kwa mazoea pasina utendaji yakinifu.

Dc Ngupula amesema kuwa kumekuwa na udanganyifu mkubwa katika utoaji wa takwimu za wanafunzi hewa kwani taarifa za awali zilieleza kuwa kuna wanafunzi hewa Wilayani Nzega zaidi ya 4000 lakini amesema kuna uwezekana wa kuwapo na wanafunzi wengine wengi hivyo endapo kama jambo hilo litabainika wale wote walioshiriki katika udanganyifu huo watachukuliwa hatua za haraka kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kazi.

Ili kuelekea kwenye uchumi wa Taifa la kati kuna kila sababu ya kuwa na Taifa imara lenye wasomi wa kutosha lisiwe Taifa la watu wajinga hivyo ni lazima kuhakikisha wanafunzi wengi wanapata elimu kwani ndio njia pekee ya kujikwamua na umasikini uliokithiri nchini Tanzanaia.

No comments: