Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa Mradi wa Umeme wa Maji wa Kilowati 430 katika Kata ya Ikondo mkoani Njombe. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi (wa kwanza kushoto), Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli (wa pili kushoto), Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Jane Nunes (wa Tatu kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt Gideon Kaunda (wa pili kulia) na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni (wa Nne kulia).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kutoka kulia) akipiga makofi mara baada ya uzinduzi rasmi wa Mradi wa Umeme wa Maji wa Kilowati 430 katika Kata ya Ikondo mkoani Njombe. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi (wa kwanza kushoto), Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli (wa Tatu kushoto), Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Jane Nunes (wa Nne kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt Gideon Kaunda (wa pili kushoto).
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kushoto) akiangalia moja
ya mitambo ya kuzalisha umeme Umeme wa
Maji wa Kilowati 430 katika Kata ya Ikondo mkoani Njombe. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe,
Rehema na wa kwanza kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini,
Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.
Na Teresia
Mhagama
Naibu Waziri
wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amezindua mradi wa umeme wa Kilowati
430 unaotokana na maporomoko ya maji katika Kata ya Ikondo mkoani Njombe ambapo
mpaka sasa zaidi ya wateja 1140 wameunganishiwa umeme huku zoezi hilo likiwa ni
endelevu.
Uzinduzi huo
uliofanyika katika Kata hiyo ulihudhuriwa na Balozi wa Italia nchini
Tanzania, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa
wilaya ya Njombe, wananchi wa Kata ya Ikondo, Shirika lililotekeleza mradi huo
la CEFA, watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) na Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO).
Dkt. Kalemani
alisema kuwa mradi huo umetekelezwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya
CEFA kutoka Italia na kugharamiwa kwa pamoja kati
ya Jumuiya ya Ulaya na Serikali ya Tanzania kwa jumla ya Dola za Marekani
110,209.
Aliongeza kuwa
mradi huo wa umeme utasambazwa katika vijiji vilivyoko kata za Ikondo, Matembwe
na Lupembe na ziada itakayobaki inaingizwa kwenye gridi ya Taifa.
" Habari
njema ni kuwa tayari vijiji Saba vimeunganishiwa umeme kupitia mradi huu, hii
inatimiza moja ya malengo ya Serikali ya kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji
wa nishati bora katika maeneo ya vijijini kupitia asasi za kiraia,"
alisema Dkt. Kalemani.
Alisema kuwa,
hadi kufikia mwezi Juni, 2016 idadi ya wananchi wanaopata huduma ya umeme
imefikia asilimia 40 huku vijijini ikiwa ni asilimia 24 na kueleza
kuwa juhudi zaidi zinafanyika ili kufikia lengo la kuunganisha umeme kwa
asilimia 75 ya wananchi ifikapo mwaka 2025.
Aidha, Dkt.
Kalemani aliwasisitiza wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji,
kuhakikisha kuwa wanavitunza vyanzo hivyo na mazingira kwa ujumla ili kuweza
kuwa na miradi ya mafanikio kama huo wa Ikondo.
Awali Meneja
Mradi kutoka CEFA, Jacopo Pendezza alisema kuwa Taasisi hiyo ipo nchini kutoka
mwaka 1976 na imejikita katika miradi ya umeme vijijini na ina miradi mbali
mbali ya umeme inayofanya kazi katika Kata ya Matembwe, Boma la Ng'ombe na
Ikondo mkoani Njombe.
Alisema kuwa
awali mradi huo wa umeme wa Ikondo ulikuwa unazalisha Kilowati 80 za umeme lakini
kutokana na mahitaji ya wananchi kuongezeka, CEFA kwa kushirikiana na kampuni
ya kijiji cha Matembwe (MVP) inayosimamia mradi huo, waliamua kuongeza mtambo
wa Kilowati 350 na hivyo kupelekea mradi huo kuzalisha jumla ya kilowati 430 za
umeme.
Alisema kuwa
umeme huo umeleta faida mbalimbali ikiwemo uanzishwaji wa miradi mbalimbali
ambayo inawaletea wananchi kipato ikiwemo kiwanda cha kutengeneza chakula cha
mifugo, soseji, mafuta ya kupikia, na kutumika katika shughuli za useremala na
ushonaji wa nguo.
Kwa upande
wake, Mwakilishi wa EU katika uzinduzi huo, Jenny Nunes alisema kuwa
mradi huo utakuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kuboresha maisha ya wananchi
kiuchumi, kusaidia wanafunzi katika masomo na huduma nyingine muhimu za
kijamii, na kusaidia juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema kuwa
EU itaendelea kusaidia miradi ya umeme nchini ili wananchi wengi wapate nishati
hiyo muhimu na kwamba zaidi ya shilingi bilioni 400 zitatumika kwa ajili ya
sekta husika.
Aidha, Mkuu wa
Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi alisema kuwa makao makuu ya wilaya zote mkoani
Njombe, yameunganishwa na huduma ya
umeme na kwamba vijiji 250 kati ya 384 katika Mkoa huo tayari vinapata huduma
ya umeme.
Alisema kuwa
mkoa huo unazalisha mazao mbalimbali ikiwemo Chai, ambapo ili kuongezea thamani
ya mazao hayo, lazima kuwe na umeme wa uhakika utakaosambazwa katika vijiji
vyote vya Mkoa husika.
No comments:
Post a Comment