NA MWANDISHI WETU
Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) imezindua MPANGO Mkakati wa miaka mitano 2016 – 2020 ambao umeainisha vipaumbele saba kwa kufanyia Utafiti katika masuala mbalimbali ya Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania. Uzinduzi huo ulifanyika katika Ofisi za Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shabani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo Doto M James.
Mpango Mkakati huo 2016 – 2020 ambao ni wa sita tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo,umeainisha maeneo makuu saba ambayo ndani ya maeneo hayo kuna maeneo mengine madogo madogo ishirini na sita ambayo kwa pamoja yatatiliwa mkazo katika kipindi hicho cha miaka mitano.
Maeneo hayo makuu ni; Kukuza Uchumi, Ajira na Viwanda; Utawala na Uwajibikaji; Utandawazi na Ushirikiano wa kikanda; Utoaji wa huduma na ulinzi wa kijamii; Mali asili na Usimamizi wa Mazingira; Usimamizi wa Maarifa na Ubunifu pamoja na Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Endelevu.
Bi. Amina alisema kwamba serikali imefurahishwa sana na juhudi kubwa zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF)
kusaidia serikali kusukuma mbele huduma zake kwa jamii na kupanua uwezo wa kutengeneza Taifa linalotekeleza sera za ukuaji wa uchumi.
Aliwapongeza waandaaji wa Mpango Mkakati huo na kusema Wizara yaFedha na Mipango inafurahishwa sana na namna Taasisi hiyo kama chombo cha Utafiti kinavyosaidia kuonyesha njia na kutoa mwelekeo kwa masuala mbalimbali ya kisera na utekelezaji.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema kutokana na Mpango Mkakati huo, serikali imefurahishwa kuona kuwa taasisi hiyo pia imejikita katika kusaidia kuona serikali inafanikisha utekelezaji wa maendeleo endelevu nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF Dkt. Tausi Kida akizungumza kabla ya kumkarisbisha mgeni rasmi Bi. Amina kuzindua Mpango Mkakati huo pamoja na mambo mengine alisema kwamba Taasisi yake imejikita katika kufanya tafiti maeneo saba ambayo yamo katika mpango wa pili wa maendeleo.
Wadau katika kujadili Mkakati huo wameiomba Serikali kufanikisha Tafiti zote zilizokusudiwa kufanywa zinatekelezwa kwa kuisaidia Taasisi.
No comments:
Post a Comment