Advertisements

Monday, November 7, 2016

IJUE HISTORIA YA SIASA NA MAENDELEO YA TANZANIA

Image result for ABUBAKAR SALEH MOHAMED TAMBAZA

Kulia ni Abubakar Mohamed Saleh Tambaza 1959 - 2012


Ukitaka kumjua Abubakar itabidi kwanza uanze na wazee wake. Ukoo wa Tambaza historia yao Dar es Salaam inakwenda zaidi ya miaka mia moja na zaidi na hii ni historia ambayo inaweza ikaelezwa na wao wenyewe kwa kukuonyesha yale yalioachwa na wazee wao kuanzia Kariakoo, Kisutu sasa sehemu ya Mtaa wa Bibi Titi, Upanga na Mabibo ambako kwa sasa ndiyo yalipo makaburi yao. Ukianzia eneo la Upanga hodhi yote ile ilikuwa mali yao. Makaburi yao mengine ya wazee wao yapo Upanga ambapo sasa umejengwa Msikiti wa Maamur. Lakini kubwa ni jinsi wao wenyewe wanavyoweza kuhadithia kwa njia ya ajabu sana habari za wazee wao hao kwa uhakika kabisa hadi kuishia kwa Bwana Abdallah aliyekuwa Jumbe wakati wa ukoloni wa Waingereza. Msikiti wa Kisutu maarufu kama Msikiti wa Mwinyi Kheri Akida ambao ulijengwa na Sheikh Mwinyikheri Akida katika miaka ya mwisho ya 1800, ni msikiti wao na hadi sasa uko chini ya uongozi wao. Huyu Sheikh Mwinyikheri Akida ni katika mababu zake Abuu. Kwa uhakika kabisa ni babu wa babake Abuu Marehemu Mzee Mohammed Saleh Abdallah Tambaza.

Historia ina kawaida ya kujirudia. Sheikh Mwinyikheri Akida aliishi Kisutu ambayo ni sehemu ya mwanzo ya makazi Dar es Salaam. Sheikh Mwinyikheri Akida alikuwa katika masheikh wakubwa wa wakati wake na alikuwa na sifa kubwa ya ucha Mungu. Sheikh Mwinyikheri Akida alipofariki miaka ya mwanzo ya 1900, Dar es Salaam ilitaka kumpa maziko makubwa sana. Abuu kama babu yake, ambae kati yao wametenganishwa na zaidi ya miaka mia moja maziko yake yamefuata nyayo zile zile. Dar es Salaam kama ilivyotoka kumzika babu yake mkuu miaka mia iliyopita iliamka kwa kishindo kuja kumzika mwana mji Abubakar Mohamed Saleh, kijana wa Kariakoo, mtu mwema na karim, aliyependa kusaidia aliyemjua na asjiyemjua, msheshi, mtu wa maskhara na aliyejikurubisha kwa kila mtu kwa mapenzi na bashasha bila kujali hali yake.


Dar es Salaam huwa ina kawaida ya kulala usingizi ikawa huisikii kabisa na wakati mwingine ukasema haipo. Lakini Dar es Salaam hiyo hiyo ghafla huzinduka ikaamka kwa kishindo kikubwa na kwa hakika kila mtu akashtuka akasema, “Ala kumbe Mzizima na watu wake bado ipo.” Hali hii hutokea kwa ghafla na bila taarifa pale Dar es Salaam inapompoteza mtu wake. Hapo ndipo utaijua kuwa Dar es Salaam ingalipo na ina watu wake. Achana na maneno kuwa Dar es Salaam hii ya sasa ati haina mwenyewe. Hakuna mali isiyokuwa na mmiliki wake. Utaijua Dar es Salaam ina wenyewe mmoja wa watoto wa Dar es Salaam anapokutwa na fardhi (mauti). Maziko ya Abubakar Mohamed Saleh wa Tambaza, hayajapata kuonekana. Dar es Salaam ina historia ya maziko ya watu wake. Kumbukumbu za mazishi katika historia ya Dar es Salaam zinaonyesha kuwa mazishi ya kwanza makubwa yalikuwa ya Sheikh Idrissa bin Saad. Sheikh Idris alifariki mwanzoni mwa miaka ya 1950 na alizikwa ndani ya msikiti wake Mtaa wa Narung'ombe, Kariakoo. Jeneza lilitoka nyumbani kwake na nyumba yake ikitazamana na msikiti wake lakini ilikuwa kazi kubwa kulifikisha jeneza msikitini jinsi umma ulivyokuwa umejaa. Mkanyagano juu ya mkanyagano. Maziko makubwa mengine yalikuwa ya Sheikh Kaluta Amri Abeid aliekuwa Waziri wa Sheria katika Serikali ya Awamu ya Kwanza. Sheikh Amri Abeid alifia Ujerumani mwaka 1963 na maiti yake ilirudishwa nchini na kuzikwa katika makaburi ya Chang'ombe. Yakafuatia mazishi ya Abdulwahid Sykes mwaka 1968 ambae alizikwa makaburi ya Kisutu. Maziko ya Abdulwahid Sykes yaliacha historia. Ilikuwa nani ni nani katika Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza Nyerere alionekana akitembea kwa miguu nyuma ya jeneza kutoka nyumbani kwa mama yake Abdu Mtaa wa Lindi kuja Msikiti wa Kitumbini. Baada ya hapo yakaja mazishi ya Sheikh Kassim bin Juma mwaka 1993. Umma uliojitoleza kuja kumzika Sheikh Kassim ulitisha.

Dar es Salaam ina historia ya kuwaenzi watu wake maarufu. Sheikh Idrissa alikuwa Khalifa wa Tarika Askariyya aliyoianzisha yeye mwenyewe. Tarika hii ina murid wengi kutoka sehemu za Rufiji na Kilwa. Sheikh Amri Abeid alikuwa katika kundi la Waislam wa mwanzo kushika madaraka ya juu serikalini. Abdulwahid alifahamika zaidi kwanza kutoka kwa sifa aliyokuwa nayo baba yake katika jamii wakati wa ukoloni wa Wajerumani hadi kuingia kwa Waingereza. Lakini kubwa kwa Abdulwahid ni kuwa alikuwa mwanasiasa kijana, muasisi wa TANU na watu wa Dar es Salaam walimjua kama mtu aliyemkaribisha Nyerere mjini na kumwingiza katika harakati za siasa. Sheikh Kassim Juma jinsi vyovyote ingevyotokea, Allah alimpa kipaji cha ajabu akifika mahali hata kama palikuwa pamepooza basi patachangamka. Katika siku za mwisho za uhai wake alitofautiana vibaya sana na serikali. Hii ilimpelekea yeye kukamatwa na kutupwa gerezani na baadae akafa huku kesi yake ikiwa bado ipo mahakamani.

Wote hawa walikuwa na michango yao kwa mji wa Dar es Salaam ingawa kwa viwango tofauti, na watu hawa walipokufa watu wa Dar es Salaam walitoka kuja kuwapa heshima zao walizostahili kama viongozi na mashujaa wa taifa hili. Mazishi ya watu hawa wote waliokuwa na majina makubwa ya kutajika katika vyombo vya habari na wakialikwa katika hafla kubwa kubwa za kitaifa hao wote mazishi yao hayakufikia maziko ya Abubakar Tambaza hata kwa mbali. Yapo maziko mengine makubwa lakini hatuwezi kuyataja yote mathalan maziko ya Rubani wa Ndege za Kivita, Said Karama, maziko ya Mzee Maneno Kilongora, maziko ya hivi karibuni ya baba yetu mrehemu Mzee Kitwana Dau na mengine mengi. Sasa iweje Abuu kijana wa Kariakoo, mtu wa kawaida kabisa, mtu ambae sura yake haikupata hata kutokea katika gazeti wala runinga, apewe maziko makubwa kupita watu hao wote waliokuwa maarufu na wenye majina ya kutajika? Iweje leo Abuu anasomewa visomo leo Msikiti wa Makonde, kesho Msikiti wa Mtoro, nk. Nani huyu Abubakar Tambaza kiasi awe mpenzi wa kila mtu wa kila msikiti?

Lazima nikiri kuwa nilishtuka nilipofungua gazeti la “Mwananchi” na kukuta picha ya Abuu na chini yake ipo taazia iliyoandikwa na Dk. Ramadhani Dau. Haukupita muda napokea ujumbe a simu kuwa ipo taazia nyingine ya Abuu katika “Uhuru” na “Jambo Leo” zote zimeandikwa na Dk. Dau na amenunua ukurusa mzima kuomboleza kifo cha rafiki yake. Kwa hakika nilipigwa na butwaa. Mimi Abuu ni mdogo wangu kwa maana halisi ya neno lenyewe. Kaka yake Abuu, Abdallah Mohamed Tambaza ni rafiki yangu toka utoto na tulisoma sote St. Joseph’s Convent katikati ya miaka 1960 na hadi leo ni rafiki yangu kipenzi. Isitoshe wazee wetu wakijuana. Taazia zile tatu zote zimetoka siku moja tena kwa kurasa ya kulipiwa na ukurusa mzima kwangu mimi kitu hicho kilikuwa jambo geni. Sijapata kuona kitu kama hiki kabla. Kitendo cha Dk. Dau kumlilia rafiki yake kwa namna ile kilinidhihirishia mapenzi ya hali ya juu kati ya watu hawa wawili. Dau aikuwapo hospitali Hindu Mandal wakati rafiki yake yuko katika sakarat maut na bila shaka ninavyomjua Dau pale alipokuwa kwa hakika kabisa Yasin ilikuwa ikimtoka. Watu waliokuwa wakipendana na wakajahitimishana namana hii ni wa kuliliwa ngoa. Fikra zangu zilirudi nyuma mara ya mwisho mimi na Abuu tulipokuwa ofisini kwa Dk. Dau. Baada ya maskhara yao kama kawaida Dau aliagiza na mara sote wawili tukaletewa zawadi za NSSF katika mifuko maridadi. Mimi kama mwandishi kila niwapo huwa na zana zangu za kazi. Niliwaomba niwapige picha na nikawapiga picha pamoja, ndugu wapenzi marafiki wawili. Haukunijia hata kidogo kwa wakati ule kuwa picha ile itakujakuwa kumbukumbu kubwa ya majonzi.

Msomaji wangu ungepata bahati ya kuwakuta watu hawa wawili katika barza wanazungumza wewe usingelitia lako ungekaa kimya usikize. Mimi nikifanya hivyo kila nilipokuwanao pamoja. Kwanza ngoja nikufahamishe kitu. Ikiwa unataka kukisikia Kiswahili cha pwani kwa lafidhi yake halisi ilikuwa umsikize Abuu akizungumza. Mimi kwa vijana wa leo sijapata kumsikia kijana aliye na ulimi aliokuwanao Abuu. Hilo moja. Sasa ngoja nirudi kwa sahib wake Dau. Dk. Dau ana ulimi kama aliokuwanao Abuu lakini hakumshinda na hili naweza kulieleza. Ingawa wote wamekulia katika mazingira sawa ya mjini na kukisema Kiswahili kwa lafidhi ya pwani iliyonogeshwa kwa wao kusoma Qur’an iliyonyoosha matamshi yao, Dk. Dau kwa kiasi kidogo sana kaathirika na kule kusoma Kizungu sana. Matamshi ya Dk. Dau hayatoki na ile ladha unayoisikia kwa Abuu. Sasa wanapopambana katika baraza ilikuwa raha na wote wana barza huwa kimya wakiwasikia wanavyopashana. Raha ilikuwa katika ujuzi wa lugha na pili katika kule kupeana maneno. Dau atamuambia Abuu huku akicheka sana, “Abuu leo sheikh nimekuwa sina maana, ushasahau nilivyokuwa nakuvusha barabara Morogoro Road tunakwenda shule...” Barza itaangua kicheko. Abuu atarudisha mapigo sasa kawageukia wasikizaji, “Jamani hebu semeni wenyewe huyu kwa ukubwa gani aliokuwanao kiasi yeye anivushe mie barabara. Mimi siwezi kuwa mwizi wa fadhila kama yeye leo kasahau kama kuwa mimi ndiye nilkuwa nikiwatisha watoto wa Kihindi shule wasimpige...” Hapo vicheko vinaongozeka. Hapo pembeni yuko mzee wetu mkubwa wa barza na mwenyekiti wa kudumu, Mzee Kissinger, Mohamed Khalil, Jamil Hizam (Denis Law), Panji (mdogo wake Abuu) na jamaa wengine dhumna inakwenda lakini watu wameshikilia mbavu kwa kicheko. Mzee Kissinger ni kamusi inayotembea kuhusu historia ya Dar es Salaam na watu wake. Jamil Hizam alikuwa mcheza kandanda hodari katika miaka ya 1960 hadi 1970 ndiyo watoto wa mwanzo kutoka Dar es Salaam kucheza timu ya taifa ya vijana Tanzania. Jamil katika ujana wake akimuhusudu Denis Law mchezaji wa Uingereza na jina akalipata la shujaa wake. Dau na Abuu wanatazamana kila mmoja anasubiri mashambulizi. Abuu kama vile namuona kaegemea ukuta, kofia yake kaibenjua kwa mbele. Dk. Dau na yeye yuko katika darzi yake na kofia kaiweka upande kwa mvao maarufu wa watu wa Mafia.

Hawa ndiyo marafiki wawili ndugu waliopendana na wakaonyesha mapenzi yao kwa dhati ya nafsi zao na kwa vitendo. Dk. Dau mkurugenzi wa shirika kubwa, alipata kuwa mhadhiri Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam amekaa barazani kwa rafiki yake Abubakar, Kariakoo Mtaa wa Kongo kamfuata kumjulia hali. Kwake yeye Abuu ni yule yule Abuu rafiki yake, cheo chake cha ukurugenzi na kisomo chake hakikuathiri hata chembe uhusiano wao. Wangapi leo wanayaweza haya. Tunayo mifano mingi ya baadhi ya jamaa zetu wakiingia katika nafasi basi husahau rafiki zao wa zamani na kuwanyanyapaa wakajishughulisha na hao ambao wao huwaona ndiyo “stahili” zao kwa kuwa ni “wakubwa” kama wao. Wakawa wao ni watu wa Gymkhana Club na mahoteli makubwa ya fahari.

Katika taazia ya Dk. Dau, Dau amesema Abuu alikuwa na uradi aliodumu nao hadi anakufa nao ni kuandaa chakula asubuhi na jioni kuwakirimu watu. Neno “uradi” alotumia Dau ni neno zito sana na kwa hakika kalitia mahali pake ingawa si kwa kawaida kwa neno hilo kutumika hivyo. Wengi tumezoea neno “uradi” kuwa dua asomayo mja khasa katika kumuhimidi mola wake. Dk. Dau katufahamisha kuwa uradi wa Abuu ulikuwa kutoa sadaka ya chakula asubuhi na jioni. Hakika mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Uradi huu umenikumbusha baba yake mkubwa Abuu, Bwana Yahya Saleh. Mzee Yahya akikaa Mtaa wa Kariakoo na Sikukuu na ilikuwa ada ya akina Tambaza watoto na wazee wao kuswali Ijumaa msikitini kwao, Msikiti wa Mwinyikheri Akida na baada ya sala wote kuongozana hadi nyumbani kwa Mzee Yahya kwa chakula cha mchana. Kama vile ni jana fikra zangu zinanirudisha nyuma. Namuona Mzee Yahya Saleh, mdogo wake Mohamed Saleh, Bwana Mwinyimadi, wametangulia mbele nyuma wanafuatia watoto wao, Abdallah Mohamed Saleh, Saleh Yahya, Abubakar, Mahdi (sasa ni sheikh) na sisi wengine ingawa si akina Tambaza lakini katika ule wali haulizwi mtu ni wa nani unakaa jamvini unanawa unakula. Dua inasomwa kisha mnatawanyika. Uradi huu uliendelea pale Kariakoo nyumbani kwa Mzee Yahya Saleh hata baada ya kifo chake. Niliposoma kuwa Abuu yeye kenda mbele zaidi ya wazee wake kwa ukarimu kuwa yeye kutoa chakula ni uradi wake wa kila siku na kubwa zaidi ulezi wa mayatima, nilishukuru. Abuu aliwachukua watoto wa mitaani akawatia katika timu ya mpira Bom Bom. Watoto hawa kwa kiasi kikubwa walipata malezi na maadili mema. Timu hii ni ya watoto wadogo ni maarufu sana Kariakoo. Ikutoshe tu katika watoto hawa wawili hivi sasa ni wachezaji katika Club ya Simba. Hii leo vijana hawa si watoto wa mtaani tena vijana wanaoendesha maisha yao na kutoa mchango katika taifa. Vilevile kwa miaka kadhaa alikuwa akiliendesha kombe lake la kila mwaka la Tambaza Cup. Mashidano haya yamekuwa maarufu na limetoa msisimko wa pekee kwa vijana wa Kariakoo.

Kwa hakika wasifu wa Abubakar Mohamed Tambaza ni mrefu na siwezi kuumaliza katika siku moja. Abubakar alikuwa mwanasiasa, mwanamichezo mpenzi wa wa Sunderland. NImelitumia neno hili “Sunderland” kwa makusudi sasa ni Simba Sports Club. Abuu na rafiki zake akina Mshike, Matimbwa wengineo hufurahi sana ukiwanasibisha na Sunderland kwa kuwa unawakumbusha mbali. Baba yake Abuu Mzee Mohamed Saleh alikuwa mchezaji wa Sunderland katika ujana wake kasha akaja kuwa kiongozi wa Simba katika miaka ya 1970 akwa Mtunza Fedha. Baba yake mkubwa Bwana Yahya alipata kuwa Mbunge wa Dar es Salaam mkwaka wa 1970 hadi 1975 wakati huo haijagawiwa. Mzee Yahya Saleh alimwangusha Balozi Tatu Nuru (sasa marehemu). Mzee Yahya Saleh alikuwa mmoja wa wanachama shupavu wa TANU Tawi la Mvita wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika. Tawi hili lilikuwa Mtaa wa Mvita Dar es Salaam Kaskazini chini ya uongozi wa Mtoro Kibwana kama mwenyekiti na Sheikh Hadair Mwinyimvua kama katibu. Ilipofika mwaka wa 1957 Yahya Saleh akachaguliwa kuwa mwenyekiti wake. Lakini asili ya tawi hili lilianzia Kisutu kasha likahamia Mtaa wa Mvita. Mtoto wa Sheikh Haidar Mwinyimvua ndiye imam hivi sasa wa Msikiti wa Mwinyikheri Akida. Inasemekana katika Tanganyika nzima hapakuwa na tawi la TANU lililokuwa na nguvu kama tawi hili. Abuu alikujafuata nyayo hizi hizi za wazee wake katika siasa. Alitoa mchango wake katika tawi lake la Jangwani kwa kadri ya uwezo wake akiwa Mwenyekiti Serikali ya Mtaa CCM Kata ya Mtambani B Mtaa wa Kongo kwa vipindi vitatu mfululizo. Vilevile Abuu alikuwa Mwenyekiti CCM Tawi la Jangwani ambalo limejumuisha hata Makao Makuu ya CCM Ofisi Ndogo Mtaa wa Lumumba. Tawi hili la la Jangwani hii leo unaweza kulifananisha na tawi lile la Mvita wakati wa kudai uhuru. Vilevile alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ilala. Hii ni kamati kubwa sana katika CCM.

Naambiwa kwenye mazishi yake waheshimiwa wote walikuwapo wakipigana vikumbo. Mbele ya nyumba yao Mtaa wa Congo No. 1. Kilipokuwa kinara palijaa wanawake ikabidi wanaume wasogee mbele mitaa ya jirani. Hili si jambo la kawaida kwa kuwa kisomo sasa kitasommwa kwa mbali na nyumba ya msiba. Wanasema Dar es Salaam haijapata kushuhudia wanawake wengi kiasi kile katika msiba. Uani kwenye nyumba ya shughuli walijazana wanawake wa kila umri. Sheikh Zuberi alikpokwenda uani kuwafariji alipewa sifa ya Abuu kuwa alikuwa kimbilio lao kila walipokuwa na matatizo na aliwasaidia na kuwawekea heshima zao. Uani kulikuwa vilio na kwiki. Mtaa wa Kongo na mitaa ya jirani ilikuwa haipitiki. Kila utakapoingilia, iwe umeingia kwa Mtaa wa Twiga, au Nyati, Matumbi au kutokea Mtaa wa Msimbazi au Swahili kuingia mitaa ya jirani kama Rufiji ilibidi uishie huko huko haikuwezekana kuifikia nyumba ya shughuli. Sala ya jeneza haikuweza kuswaliwa msikitini kwa kuwa hapakuwa na msikiti ambao ungeliweza kuchukua umati ule wa Waislam waliokuwa pale. Ilibidi sala ile iswaliwe palepale nyumbani kwao mbele ya uwanja wao. Haya yalipataikana kuonekana mara moja tu katika historia ya Dar es Salaam. Kwanza ilikuwa katika maziko ya Prof. Malima na pili maziko ya Abubakar. Msafara wa kuelekea shambani kwao Mabibo ulisindikizwa na askari wa Usalama Barabarani vinginevyo ingelikuwa shida kuupitisha umma ule wa magari Barabara ya Morogoro hadi Port Accees Road na kuingia Mabibo

Mkono wangu wa pole uende kwa mama yetu Biti Selemani Nyaubuguyu ambae kila siku akimtia machoni Abuu. Huyu Bi Mkubwa mimi ni mama yangu. Siku moja nilifika pale nyumbani baada ya miaka mingi na katika mazungumzo akanambia, “Mimi nikimfahamu mama yako pale Kipata. Mimi nilipoolewa na baba yenu nilikuwa nakaa kwa Mama Nambaya.” Mama yangu kafa 1956 na huyu Mama Nambaya alikuwa shoga ya mama yangu. Hadi miaka ya 1970 nilikuwa nikipita kumwamkia Mama Nambaya na alikuwa akifurahi sana na wakati mwingine akinihadithia habari zangu kuwa mama yangu alikuwa akitaka kwenda sokoni alikuwa akiniacha kwake hadi arejee. Mwanae Shabaka alibaki kama kaka yangu mkubwa hadi alipofariki kiasi miaka mitatu iliyopita. Mkono wangu wa pole umfikie Dk Dau. Hapa sitasema mengi. Nampa pole kaka yake Abubakar rafiki yangu, Abdallah Mohamed Saleh wa Tambaza. Hakika tumeondokewa na Dar es Salaam ina haki ya kuwa mkiwa. Mola atupe sote moyo wa subira. Tunamuomba Allah amsamehe Abubakar madhambi yake na amjazie pale palipopungua na amlipe pepo. Amin.

Mohamed Said
15 January 2012

No comments: