Advertisements

Monday, November 14, 2016

KESI YA AKINA ZOMBE: MRAKIBU WA POLISI (SP) BAGENI APINGA HUKUMU YA KUNYONGWA HADI KUFA

Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP),Christopher Bageni amewasilisha maombi Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

SP Bageni alihukumiwa adhabu hiyo baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kwamba aliwaua kwa kukusudia wafanyabiashara wanne wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi mkazi wa Manzese, Dar es Salaam,  katika Msitu wa Pande.

Bageni kupitia Wakili wake, Gaudioz Ishengoma,  aliwasilisha maombi hayo mwishoni mwa wiki yaliyoambatana na hati ya kiapo iliyoapwa na wakili huyo.

Muwasilisha maombi anaomba mahakama hiyo kuifanyia marejeo hukumu dhidi yake iliyotolewa Septemba 13 na kusomwa  Septemba 16 mwaka huu na Msajili wa Mahakama hiyo, John Kahyoza.


Akitoa sababu kuomba marejeo, anadai  alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa wakati wa kutathmini ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama kwa kuegemea kwenye ushahidi wa upande wa mashtaka.

Alidai katika kuchanganua ushahidi ambao uamuzi wa mahakama uliegemea, mahakama ilishughulika na ushahidi wa msingi (Exam in Chief) wa upande wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu tu ushahidi wa utetezi hususan wa Bageni au haikuutazama kabisa.

“Kuna kukinzana kwa haki kwa maana ya kwamba mtoa maombi alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa, kwa mahakama kuchagua na kuegemea   upande wa mashtaka pekee na kushindwa kuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi, hasa wa mtoa maombi.

“Uamuzi wa mahakama umetolewa katika msingi wa makosa ya dhahiri kwenye kumbukumbu za mahakama, hivyo kusababisha upotoshaji wa haki, kushindwa kuzingatia mwongozo wa kanuni katika asili, thamani na matumizi ya ushahidi wa kuungwa mkono,” ilisema sehemu ya maombi hayo.

Alidai kuwa kwa kushindwa kuchanganua na kutathmini  ushahidi kwa umakini kwenye kumbukumbu, mahakama ilishindwa kuainisha ushahidi wa mjibu rufaa wa nne (Bageni)  kimazingira kama ilivyo ni dhahiri unakosa thamani ya kuhitaji ushahidi wa kuunga mkono na hivyo si salama kuegemea katika kumtia hatiani.

“Kwa kushindwa kuona na kuzingatia ushahidi uliokusudiwa kuwa na ushahidi wa kuunga mkono, siyo ushahidi huru na hauna mashiko kuthibitishwa (PW27) na haupo (PW36).

“Kwa kushindwa kufanya uchambuzi wa ushahidi kwenye kumbukumbu kwa umakini wenye manufaa, vinginevyo mahakama ilipaswa kuona wajibu wa kuthibitisha shtaka kwenye jinai haukufikiwa,”anasema Wakili Ishengoma.

Anadai mahakama katika kuamua, kama ilivyofanya katika uhalisia wake, kuhusu ushiriki wa mtoa maombi katika eneo la tukio la uhalifu, ilishindwa kubaini katika ujumla wake ushahidi wa upande wa mashtaka ambao haukuweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.

Ishengoma alidai mahakama haikuuchukulia ushahidi kwenye kumbukumbu katika ujumla wake hivyo kutengua uamuzi wa kuachiwa huru kwa mtoa maombi na kumtia hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kusimamia ushahidi ambao haupo na uvumi pamoja na ushahidi wa mashaka makubwa.

Alidai kutokana na hukumu ya mahakama, haikuwa bayana ni kwa ushahidi wa nani ulithibisha mtoa maombi Bageni alimwezesha au kumsaidia nani katika mauaji ya marehemu hao.

Katika hati ya kiapo iliyoapwa na Wakili Ishengoma, Bageni anadai yeye na wengine wanane ambao hawako katika maombi hayo walishtakiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa makosa ya mauaji ya watu wanne katika Kesi ya jinai namba 26 ya mwaka 2006.

Bageni alikuwa mshtakiwa wa pili na katika hukumu iliyotolewa na Jaji Salum Massati, amnayo  wote waliachiwa huru, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo hivyo alikata rufaa namba 358 ya mwaka 2013.

Kabla ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, DPP aliwaondolea rufaa wajibu rufaa watano na kubaki wajibu rufani wanne ambao waliachiwa huru pia Septemba 16, mwaka huu.

Walioachiwa huru ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na maofisa wengine wawili baada ya mahakama kuona hakuna ushahidi wa wazi ama mazingira kuwatia hatiani.

Katika kesi ya msingi, Bageni alidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese , Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande, Mbezi Luis, Dar es Salaam.

No comments: