Advertisements

Wednesday, November 23, 2016

Lema akwama jaribio la tatu

By Filbert Rweyemamu ,Zulfa Mussa, mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Arusha. Jaribio la tatu la Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kupata dhamana limegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali maombi ya marejeo ya kesi inayomkabili na kumtaka akate rufaa.

Lema aliomba marejeo ya kesi inayomkabili baada ya kunyimwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. Mahakama Kuu ilifikia hatua hiyo baada ya kukubaliana na hoja zilizowasilishwa na Jamhuri kupinga marejeo kuwa hayana na msingi wowote.

Katika uamuzi wake, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi alisema baada ya kusikiliza hoja za pande za mawakili waandamizi wa Jamhuri, Matenus Marando na Paul Kadushi na upande wa Lema, amejiridhisha kuwa hoja mbili zilizowasilishwa kupinga marejeo zilikuwa na mantiki ya kisheria.

Jaji Moshi alisema maombi ya Lema kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala yalitaka Mahakama Kuu itumie Kifungu cha 372(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kinaipa uwezo wa kufanya marejeo ya mashauri ya kesi za mahakama za chini wakati kesi ikiendelea.

Alisema msingi wa maombi yake unatokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kutoa dhamana na baadaye Jamhuri kuipinga kuwa ilitokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi kushindwa kutafsiri uamuzi wa dhamana iliyotolewa katika kesi mbili za jinai zinazomkabili. Jaji Moshi alisema Lema alipewa dhamana lakini Jamhuri ilipinga hatua iliyosababisha kusitishwa kusikilizwa kwa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi baada ya notisi ya maneno kutolewa na upande wa mawakili wa Jamhuri.

Alisema msingi wa uamuzi wake unatokana na hoja zilizowasilishwa na mawakili wa Jamhuri chini ya kifungu cha 43(2) kinachohusu Sheria ya Mahakimu, kuzuia marejeo kwa sababu inataka mlalamikaji kukata rufaa na kama anataka ifanye marejeo, aeleze kwa kina kwa nini anataka marejeo badala ya rufaa.

Alisema vifungu vya 148 hadi 160 vinatoa haki ya dhamana lakini kifungu cha 161 kinaeleza namna utaratibu huo unavyoweza kufuatwa bila kuathiri masharti ya kisheria. Baada ya uamuzi huo, mawakili wa Lema walikata rufaa chini ya hati ya dharura.

Wakati Lema akirejeshwa mahabusu aliwataka wafuasi wake waliokuwa mahakamani hapo wawe na moyo mkuu.

Kabla ya kuanza kusikilizwa kesi hiyo, wananchi, wabunge kadhaa na madiwani wa Chadema walikuwa na wakati mgumu kuifuatilia baada ya kuelezwa kuwa itasikilizwa katika chumba kidogo cha Jaji. Hatua hiyo ilisababisha kila aliyehudhuria kutaka kuingia katika chumba hicho. Hata hivyo, baadaye kesi hiyo ilisikilizwa katika mahakama ya wazi.

No comments: