Advertisements

Saturday, November 5, 2016

Lissu asubiri barua ya Mahakama kujisalimisha

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu
By Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

Dodoma. Siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuagiza Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema hana taarifa iwapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeagiza akamatwe kwa kushindwa kuhudhuria kortini.

Lissu ambaye pia ni mwanasheria maarufu nchini, amedai kutokana na kutokuwa na taarifa hizo hawezi kujisalimisha popote.

Lissu ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, amedai atajisalimisha kwenye vyombo vya dola au kwenda mahakamani ikiwa atapelekewa barua aliyoandikiwa na Mahakama na kutiwa saini na kugongwa muhuri na hakimu.

“Kaka, mimi siwezi kufanyia kazi za magazeti katika masuala ya kisheria, nipo hapa ninaendelea na shughuli zangu kama kawaida na kama mnavyoniona niko katika kuwawakilisha wananchi wa jimbo langu,” ameeleza Lissu.

Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema ametoa maelezo hayo alipohojiwa kuhusiana na habari zilizoandikwa na vyombo vya habari kwamba, Mahakama ya Kisutu juzi iliagiza mbunge huyo akamatwe baada ya kushindwa kuhudhuria katika kesi inayomkabili.

Mbali ya Mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa kwa Lissu, pia imeagiza iandaliwe hati ya kuitwa mahakamani kwa wadhamini wake ili wajieleze kwa nini wasilipe fungu la dhamana walilotia saini ambalo ni Sh10 milioni.

Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi wa Kisutu, Thomas Simba, Lissu amekuwa hahudhurii kortini kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14 mwaka huu, Dar es Salaam, Lissu na wenzake walikula njama za kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari: “Machafuko yaja Zanzibar”.

No comments: