Advertisements

Wednesday, November 2, 2016

MAONI KUHUSU UCHAGUZI WA MAREKANI WA MWAKA 2016

Image result for usa flag
Ubalozi wa Marekani
Dar es Salaam
TANZANIA
Mawazo machache wakati Watu wa Marekani tukielekea katika
uchaguzi wa Rais wetu ajaye

Na Virginia Blaser – Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania
2 Novemba 2016

Katika miezi michache iliyopita, nimeona ongezeko kubwa la hamasa nchini Tanzania ya kufuatilia uchaguzi nchini Marekani na Mfumo wetu wa kipekee wa uchaguzi.  Tunapokaribia Siku ya Uchaguzi hapo tarehe 8 Novemba, tunasherehekea sio tu utamaduni wa kuwa na chaguzi zilizo huru na wazi ambazo ndizo zimekuwa zikitupatia marais wetu toka mwaka 1789, bali pia amali zilizokita mizizi zinazowapa raia wote nafasi ya kuamua kuhusu serikali yao. 

Bila kujali matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Mwaka 2016, mchakato wa kidemokrasia uliodumu kwa muda mrefu tunaoutumia kuchagua rais mpya, unadhihirisha wazi amali na maadili ambayo sisi, kama Wamarekani tunayaenzi na kujivunia: uhuru wa kujieleza, uhuru wa habari na vyombo vya habari, taasisi huru na utawala wa sheria.  Maadili haya ndiyo nguzo ya demokrasia yetu. Kutokana nayo, raia wa Marekani wanaweza kushiriki kwa uhuru na uwazi kabisa katika mijadala ya kijamii huku wakihakikishiwa kuwa ushiriki wao kamilifu sio tu unakaribishwa, bali ni sehemu muhimu ya kuendeleza na kuimarisha nchi yetu.

Waasisi wa taifa letu walihakikisha maadili haya yanajumuishwa katika Katiba ya Marekani pale walipoanzisha mfumo wa uchaguzi wa Kura za Majimbo (Electoral College). Japokuwa mfumo wa awali wa uchaguzi umebadilika kidogo toka kuasisiwa kwa taifa letu, bado tunaendelea kuutumia mfumo huu wa kura za majimbo ambao hulipa kila jimbo idadi mahsusi ya kura kulingana na idadi ya watu wake. Ili kushinda uchaguzi kwa kupata kura za kutosha kuwa rais – angalau kura 270 kati ya kura zote 538 za majimbo, ni lazima wagombea wajinadi katika masuala mbalimbali yanayowagusa wapiga kura katika kila jimbo nchi nzima, iwe ni katika majimbo makubwa na hata yale madogo.

Wakati wapiga kura wanakwenda kupiga kura zao, wanachagua mgombea atakayepata kura nyingi zaidi katika kura za jimbo lao. Waasisi wa taifa letu waliona kuwa mchakato huu ndio ambao ungehakikisha kuwa sauti za watu zinasikika na kero zao zinashughulikiwa. Tunaendeleza mchakato huu kutokana na fursa unaowapatia Wamarekani kujadili maoni na mitazamo yao mbalimbali kuhusu masuala yanayowagusa.


Kwa kawaida chaguzi za Marekani hujumuisha kipengele muhimu cha midahalo mikali ya wazi. Kwa hakika, kama Wamarekani tunathamini sana kuwa na mfumo unaowezesha na kupanua nafasi ya demokrasia, unaoviwezesha vyama vya siasa kuelezea misimamo na mitazamo yao inayotofautiana na kuwezesha uhuru wa vyombo vya habari. Mfumo huu ndio unaotuwezesha kushiriki katika majadiliano makali na ya kina kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa yanayojenga jamii yetu na mstakabali wetu wa pamoja – wakati wa uchaguzi na katika maisha yetu ya kila siku. 

No comments: