ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 27, 2016

Mtoto wa miaka 11 atunukiwa PhD kwa niaba ya marehemu mama yake

WAHITIMU, viongozi na wageni waliohudhuria Mahafali ya 32 ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro, waliingiwa na simanzi wakati mtoto, Tamar Aaron Mbogho (11), alipojitokeza na kupokea Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD), akimwakilisha mama yake Swai Sophia Faustin ambaye alifariki dunia miezi sita kabla ya kufika siku ya mahafali.

Tamar, mtoto pekee wa marehemu, ambaye baba yake mzazi ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Aaron Mbogho alifika katika hafla hiyo akiwa ameambatana na ndugu zake kadhaa, tayari kwa ajili ya kupokea heshima hiyo kwa niaba ya mama yake.

Gazeti hili liliweza kuwasiliana kwa njia ya simu na Mbogho akiwa katika kituo chake cha kazi Mwanga ambapo alisema Tamar alifika katika hafla hiyo kupokea shahada hiyo kwa niaba ya mama yake.

Kwa mujibu wa Mbogho, mkewe Dk Sophia alifariki dunia Mei 21, 2016, wakati huo akiwa ameshahitimu masomo yake kikamilifu na alisema Tamar ni mtoto wa pekee wa Sophia.

"Alikuwa ni mmoja wa wahitimu waliopaswa kutunukiwa shahada hiyo kwa sababu tayari alishahitimu na kubakia muda wa mahafali, lakini bahati mbaya akafariki dunia kabla ya muda kuwadia,” alisema na kuongeza.

"Binti yetu alipenda kwenda kuchukua shahada ya mama yake na alisindikizwa na ndugu zake wa familia. Ameniambia malengo yake ni kusoma kwa bidii ili aweze kupata Shahada ya Udaktari wa Falsafa kama mama yake, " alisema Mbogho.

Katika mahafali hayo yaliyofanyika juzi katika Kampasi ya Solomon Mahlangu, Mazimbu, wahitimu 61 walifuzu na kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Naibu Makamu Mkuu Taaluma wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Peter Gilla, alisoma orodha ya watunukiwa ambapo pia alitaja jina la mwanafunzi asiyekuwapo ambaye alifariki dunia, lakini akiwa amefuzu na anastahili kupata Shahada ya PhD ya Chuo Kikuu hicho ambaye ni Sophia.

Hivyo, Mwenyekiti wa Mahafali hayo, Dk Benno Mrembuka, alimwongoza mtoto Tamar kwenda kupokea shahada hiyo kutoka kwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha na Utawala, Profesa Yonika Ngaga, hali iliyoleta simanzi na huzuni kwa washiriki waliokuwepo katika mahafali hiyo.

Baadaye Tamar alielekezwa kufika mbele ya meza kuu ili kuwapa mkono wageni mbalimbali ambao walitumia nafasi hiyo kumfariji kutokana na kumpoteza mama yake mzazi ambaye alikuwa ni mhitimu.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Gerald Monela, alisema SUA imeendelea kutoa wahitimu wa Shahada ya Sayansi na Ualimu katika masomo ya sayansi kwa ajili ya kukidhi mahitaji makubwa ya walimu wa kufundisha shule za sekondari nchini.

CHANZO: Habari Leo

No comments: