Advertisements

Thursday, November 10, 2016

MWILI WA MAREHEMU JOSEPH MUNGAI KUWAGWA LEO DAR

Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai unatarajiwa kuagwa   Dar es Salaam leo katika viwanja vya Karimjee.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mtoto wa marehemu, William Mungai alisema ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja hivyo saa 5.00 asubuhi.

Hata hivyo mtoto huyo wa marehemu hakutaka kuingia kwa undani kuhusu chanzo cha kifo cha baba yake, badala yake alisema familia iachwe iendelee kushauriana na daktari.

Alisema pamoja na hayo, kifo hicho kimewashtua kwa vile  kimetokea ghafla na kwamba baada ya kuisha kwa ibada ya kuaga mwili huo, utasafirishwa hadi Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kwa mazishi.


“Hadi sasa familia tunajua kwamba marehemu aliugua tumbo la kawaida na tulimpeleka hospitalini ambako alifariki dunia, tunaomba familia iachwe, kwa sababu  bado tunashauriana na daktari wake.

“Tumekubaliana mwili wake uagwe kesho (leo) saa tano Viwanja vya Karimjee ambako pia historia yake yote na familia itasomwa,” alisema William.

Kifo cha Mungai kilitokea juzi jioni katika kile kilichoelezwa kuwa   alianza kujisikia vibaya baada ya kunywa kiywaji katika   hoteli moja iliyopo Msasani, ambayo aliizoea.

Mmoja wa waombelezaji waliofika nyumbani kwa marehemu jana ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Zanzibar, Salum Mwalimu ambaye alimwelezea Mungai kuwa aliunga mkono  mabadiliko ya siasa.

“Hakuwa na kadi ya Chadema lakini alipenda mabadiliko, mwanaye William aligombea ubunge wa Mafinga kupitia  Chadema na baba yake alimuunga mkono,” alisema.

Mbunge wa zamani wa Kwela, Chrisant Mzindakaya alisema amesikitishwa na kifo hicho ikizingatiwa wiki iliyopita walikuwa pamoja na walizungumza mambo mengi ya siasa.

“Hakuwa na kesho katika maisha yake, alilokuwa na uwezo wa kulifanya alilifanya siku hiyo hiyo, alikuwa na msimamo, hakukubali kuyumbishwa,” alisema Mzindakaya.

No comments: