Advertisements

Monday, November 28, 2016

NAIBU MEYA MANISPAA YA SHINYANGA AJIUZULU KISA UFISADI

SHINYANGA: Naibu Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Mathew Nkulila (CCM) ametangaza kujiuzuru ujumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala wa manispaa hiyo ili kufikisha ujumbe kwa umma kwamba hakubaliani vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma unaofanyika katika manispaa ya Shinyanga.
Amejiuzulu kwa kudai kuwa Manispaa hiyo imejaa ufisadi mkubwa sana akiwatuhumu Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi na Watendaji wote kushiriki kwenye shughuli za kifisadi.
Akiongea Leo na waandishi wa habari mkoani Shinyanga, Nkulila amesema hawezi kuendelea kulea ufisadi unaofanywa na viongozi wa CCM kwenye mkoa huo na nje ya mkoa ambao unaligharimu taifa mpaka sasa.

Miongoni mwa hoja zilizomfanya ajiuzuru ni sakata la Greda aina TEREX T180 mali ya Halmashauri Manispaa ya Shinyanga,hoja za barabara za lami mjini Shinyanga,hoja kuhusu JASCO,udanganyifu wa Bajeti 2016/17 ulioanzishwa na Baraza la madiwani na uliowasilishwa wizarani sambamba na ujenzi wa nyumba za ghorofa mjini kati na usimamizi wake.

Hii hapa ni taarifa aliyoitoa leo Jumatatu,Novemba 28,2016 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu wanahabari, leo tarehe 28/11/2016 nimeona ni vema kuwaita mimi kama Diwani wa Kata ya Ndembezi, Mjumbe wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga na mtumishi wa umma kwa ujumla ili nizungumze nanyi /baada ya kujiuliza maswali mengi sana, na kuyatafakari juu ya utata wa mambo kadhaa yanayojitokeza manispaa na yenye athari kwa wakazi walionipa dhamana ya udiwani kwa uaminifu. Tarehe 10/12/215, katika baraza la kwanza niliapishwa kwa maneno haya na ninanukuu.

“Mimi Nkulila David Mathew naapa kwa dhati kwamba; nitaitumikia Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kwa wadhifa wangu wa UDIWANI na kwamba NITAHIFADHI, NITALINDA na KUTETEA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA sheria za Tanzania, maadili ya madiwani na kanuni za kudumu za halmashauri, kama zilivyowekwa kwa mujibu wa sheria, na kwamba nitaitumikia Halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kwa waminifu na moyo wangu wote (Ee Mwenyezi Mungu nisaidie)”

Pengine ni vema kueleza wazi kwamba nimeamua kujiuzuru ujumbe wa KAMATI YA FEDHA NA UTAWALA ili kufikisha ujumbe kwa umma kwamba sikubaliani hata kidogo na baadhi ya mambo yanavyoamuliwa katika kamati na kisha Baraza.
Kwa kuzingatia yote hayo nikiongozwa na kiapo naomba nianze kwa kutaja mambo nitakayozungumza nanyi, yaliyonisukuma kuwaita ili kuweka uwazi huu kwa wakazi wa Shinyanga na wakazi wa Ndembezi. Mambo hayo yatahusu:-
Greda aina TEREX T180 mali ya Halmashauri Manispaa ya Shinyanga.
Hoja za barabara za lami mjini.
Hoja kuhusu JASCO.
Udanganyifu wa Bajeti 2016/17 ulioanzishwa na Baraza la madiwani na uliowasilishwa wizarani.
Ujenzi wa nyumba za ghorofa mjini kati na usimamizi wake.
Hoja kuhusu Greda.

Mnamo tarehe 15/06/2016 katika kikao cha kamati ya fedha nilianza kuhoji mambo muhimu kuhusiana na suala zima la maamuzi kuhusu Greda la Halmashauri aina ya TEREX ambalo limeonesha uwezo mdogo wa kutenda kazi tangu lifike manispaa tarehe 20/03/2016. Nilijenga hoja za kina baada ya kupokea taarifa za ukaguzi CAG (Exit Meet ya mwezi May 2016).

Katika kikao hicho kilipelekea kikao cha kamati ya fedha kilichofuatia kutoa hoja ya kuunda kamati ndogo ya wataalamu na madiwani nikiongozwa na barua iliyosomwa kwetu na mtunza hazina wa manispaa ikinukuu barua toka kwa RAS (Katibu Tawala Mkoa) yenye Kumb. Na. AD25/290/01A/49 ikiwa na rejea yenye Kumb. Na. AG.26/522/01/81 ya tarehe 25/04/2016 toka OR.TAMISEMI ikitoa maelekezo saba (Rejea maelekezo hayo).

Nilitafakari maelekezo hayo ya msingi yenye lengo la kujenga nidhamu katika halmashauri katika utendaji kazi, ili kutimiza maelekezo hayo nilianza kufuatilia hoja za ukaguzi kwa kina na nikataka kujua yafuatayo:-
Kwa nini TEMESA walikagua Greda hilo lilipofika na kuliona lina vigezo vyote (Specifications) vya kitaalamu na baada ya kulifanyia majaribio kwa vitendo likabainika halina nguvu na uwezo wa kufanya kazi” (Hoja ukaguzi) na kisha baadae kupelekea kutofanya kazi kabisa tangu lilipofanyiwa majaribio, ingawa mratibu wa mradi wa ULGSP na mwendeshaji wa mtambo huu, walitoa maelezo kwa wakaguzi kwamba kifaa cha utambuzi wa mafuta (Fuel Sensor) hakifanyi kazi vizuri.
Nilitaka kujua kwa nini wahusika (wasimamizi) wamueleze mkaguzi kwamba mtambo upo ndani ya muda wa matazamia kwa rejea kiambatisho na 04 (sikukiona) na bado hawawajibiki kumtaarifu mzabuni kulitengeneza mpaka linakutwa na hoja za ukaguzi?
Nilitaka kujua Ndugu Razaro Madanka na Martin Musa ambao tayari wameshalipiwa gharama ya mafunzo na Halmashauri ya kuendesha Greda hilo Tshs. 1,050,000/= kwa hati ya malipo Na. 4/3 ya tarehe 02/03/2016 walienda kusoma au la?
Nilitaka kujua mkataba unasemaje wa manunuzi ya Greda hilo.

Lakini nilitoa hoja ya Greda kurudishwa kwa kuzingatia Greda limo ndani ya muda wa matazamio na wakati huohuo kuendelea na uchunguzi wa yote hayo baada ya kuunda kamati.

Mkurugenzi alipinga na kushawishi kikao kikubali kazi ya uchunguzi wapelekewe TAKUKURU, alisisitiza wao wana wataalamu wote wakiwemo manunuzi, wahandisi wanasheria na wengineo, hivyo uchunguzi utakuwa na ufanisi mkubwa kwa TAKUKURU.

Taarifa ya TAKUKURU iliyokuja ilionesha mtambo umeharibiwa na operator na hivyo litengenezwe tu. Halmashauri nayo ikasimamia hapo bila kuangalia maeneo mengine, ambayo yanadosari zinazopaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kama barua toka OR TAMISEMI inavyoelekeza.

Mfano :- katika kikao kimoja cha kamati ya fedha –mratibu wa mradi wa ULAGSP alileta hoja akiomba idhini ya kukodi wataalamu waendeshe mitambo ili huyu wakwetu apate uzoefu na sio kumkabidhi kuliendesha ,kikao kilimruhusu na akawaleta na wakawa wanalipwa posho hadi kuliharibu na kupaki kabisa.Swali ni kweli hao walikuwa wataalamu au alikidanganya kikao na kama ndiyo nani kaisababishia na hasara hiyo Halimashauri? (payment voucher ni ushahidi wa kukodi ina OPARATOR) kama si muhitasari alitoa hoja ya kuhusu kulikodisha na tulikataa
Haitoshi katika matengenezo yamekua yamekuwa yakifanyika bila kuzingatia taratibu za TEMESA

Mfano: Kubadili wembe wa pili tangu lije, ulifanyika kienyeji tu na kibaya zaidi spare zinazotolewa (chakavu) hazipelekwi stoo ambako ndipo mahala zinazopaswa kutunzwa hadi halmashauri itakapoamua vinginevyo, ( DISPORSAL).
Utata mwingine nilioubaini ni malipo yaliyofanyika tarehe 18/03/2016 ya Ths. 1,275,580 kwa L.P.O No 2015/108 iliolipwa na Halmashauri ndani ya muda wa matazamio. Sielewi idhini ilitoka wapi ya kukiuka mkataba na kuitia hasara Halmashauri bila sababu bali UZEMBE.

Ndugu wana habari mimi niliona vyema nikamuona DC na kumueleza utata huu na nikafanya hivyo siku ya tarehe 20/11/2016. Tarehe 21 kulikuwa na baraza maalumu la kujadili hatma ya Greda, mimi sikwenda kwa makusudi kwani nilijua uamuzi utakaotolewa ni tofauti na ninavyoelewa ukweli ulivyo,na ikawa hivyo hoja ikafungwa na baraza hilo bila hatua yeyote dhidi ya yeyote tofauti na barua toka OR-TAMISEMI iliyoeleza.

Hoja ikasimamiwa ya ushauri wa TAKUKURU tu litengenezwe na kwa kuwa limetengenezwa likathibitishwa linafanya kazi na madiwani kupitia kazi zililizofayika katika kata zao kwa upande wangu bado naamini hoja za CAG kwa uthibitisho wa taarifa hizi za kazi baada ya matengenezo kuelekea mapokezi ya mwenge, (rejea taarifa) greda siku 4 kuchonga Km 4.3 si sawa na ni dalili tosha ya kwamba bado greda halina uwezo wa kufanya kazi IPASAVYO, liko (very slow) taratibu sana, sielewi kwa nini linatetewa, kata ya NDEMBEZI na kwingineko kabla ya mwenge kuja limefanya kazi inayothibitisha na kutokuwa na uwezo bado.

Binafsi bado naona GIZA juu ya TIJA ILIOTARAJIWA na wakazi wa manispaa ya Shinyanga katika utendaji kazi wa mtambo huo, siungi mkono maamuzi baridi ya baraza la tarehe 21/11/2016 japo taratibu za vikao tayari zimefanyika na muamuliwa na wengi na LIMEPITA.
Hoja kuhusu barabara za lami mjini
a) ONION ROAD kudaiwa inaurefu wa Km 1.6 wakati halisi ni Km 0.3, Boma road Km 1.6 halisi ni Km 0.3, gorverment Km 4 wakati hasi ni Km 0.7, Nyerere Km 1.1 wakati halisi ni Km 0.3 na kipande kingine kujengwa na mkandarasi tofauti, Kenyata Road Km 2 halisi ni Km 1.75 na Swyneton Km 2.2 halisi ni Km 1.9 ni hoja ambayo ni ya udanganyifu mkubwa ambao niliubaini katika mkataba mmoja wa kazi aliopewa kampuni ya STEGILE kutengeneza barabarara hizo na nikagoma kusaini mkataba mpaka nilipoomba msaada kwa katibu tawala wakati huo (Mzee Talimo, sasa ni mstaafu) ambae alitumia wahandisi wake kufuatilia nami nilishiriki kuwaonesha. Yalitoka maelekezo ya nini kifanyike ikiwa ni pamoja na kuacha kuripoti udanganyifu huo.
b) Inasikitisha kuona bado udanganyifu unaendelea kwa ushahidi wa majibu ya ofisi ya mhandisi wa manispaa (rejea taarifa yao). Msimamizi mkuu wa udanganyifu huu anapaswa kuchunguzwa ajulikane achukuliwe hatua ili kujenga nidhamu katika utendaji kazi za halmashauri.
Hoja kuhusu JASCO.

Mkandarasi anaejenga barabara za lami Km. 13 Manispaa, hapa kuna tatizo kubwa la mkataba kufungwa bila kuzingatia memoranda World Bank ambayo flow ya kuletewa hela itazingatia (performance Base) hali ya ufanisi katika utendaji kazi ajabu mkataba ukafungwa wa mwaka 1 (mmoja) wakati mleta fedha hajui hilo. Dosari zipo za kizembe ambazo nazo zinanipa giza pamoja na jitihada zinazoendelea kuweka mambo sawa.
Udanganyifu wa Bajeti 2016/27 upande wa ujenzi – Barabara.

Tulipokea mrejesho wa bajeti ya 2016/17 na nilipoipitia kwa kina nikagundua kilichowasilishwa ni tofauti na baraza lilivyopitisha kupitia mkutano wake. Mfano barabara ya Boma, Onion, Government, Nyerere, Swyneton hatukuzipitisha lakini zimekuja katika utekelezaji wa kazi. Inaonesha ipo hujuma ya kuwasilisha bajeti tofauti kwa matakwa ya mtu na sio baraza jambo ambalo si jema kwa maendeleo ya halmashauri.
Ujenzi wa nyumba za ghorofa mjini kati.

Sheria hii haitekelezeki na itakapo kuja kusimamiwa basi athari zake ni kubwa sana. Ni sheria ambayo nimekua nikiifuatilia nikiwa Naibu Meya na sikufanikiwa kwa kukosa ushirikiano. Mtazamo wangu ni vema zikaachwa kabisa kwa eneo la mjini kati ili kutoa uonevu vinginevyo ili haki ya sheria itendeke, nyumba za kubomoa ni nyingi sana. Hili ni la mbunge au wabunge kusaidia kuweka sawa sheria hii isiotekelezeka kwa baadhi ya miji hasa Shinyanga manispaa ili watu wote wajenge nyumba imara na si maghorofa na mbadala wake maghorofa yaanze kujengwa sehemu nyingine ambako kuna maeneo yaliyo wazi.

Ndugu zangu wanahabari, nieleweke mimi ni kiongozi mwakilishi wa wananchi walionituma kusimamia maendeleo yao, hivyo na wao kupata habari ni haki yao na wajibu kama ilivyo na inavyosisitizwa katika kufanya mikutano ya wananchi ili kiongozi kuzungumza nao yanayohusu maendeleo yao. Kumbe kuongea nanyi nimewatendea haki kuwaeleza ukweli niujuavyo kuhusu nambo yote niliyoyataja. Cheo ni dhamana, naheshimu kiapo changu, hivyo kujiuzuru ujumbe wa kamati ya fedha si kosa bali ni njia ya kufikisha ujumbe kwa mambo ambayo sikubaliani nayo, na ambayo bila kufanya hivi nami nitasomeka naunga mkono kwa mujibu wa taraibu za uendeshaji wa vikao.

Ahsanteni kwa kunisikikiliza.


DAVID M. NKULILA
DIWANI KATA YA NDEMBEZI
MANISPAA YA SHINYANGA.

No comments: