Advertisements

Saturday, November 5, 2016

RAIS WA ICC AISHUKURU TANZANIA


Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akiwa katika mazungumzo na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) Jaji Slivia Fernandez de Gumendi. Katika mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ubalozi wa Tanzania, Rais wa ICC alitumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa Tanzania kwa hotuba ambayo si tu ilikuwa na ushauri wa namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya Mahakama hiyo na Wanachama wa Mkataba wa Roma hususani kutoka nchi za Afrika lakini pia kwamba ilikuwa ni hotuba ya uwiano. Jumatatu wiki hii Tanzania ilikuwa kati ya nchi zilizozungumza wakati Ripoti ya utendaji kazi ya ICC ilipowasilishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Balozi Tuvako Manongi na Rais wa ICC Jaji Gumendi mara baada ya kumaliza mazungumzo yao ambayo yaligusia masuala mbalimbali kuhusu Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC)


Na  Mwandishi Maalum, New  York
Rais wa  Mahakama ya   Kimataifa ya  Makosa ya Jinai ( ICC) Jaji Slivia Fernandez de  Gumendi,  jana  (Ijumaa),  amekutana na kufanya  mazungumzo na  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Matiafa,  Balozi Tuvako Manongi
Katika  Mazungumzo  hayo baina ya   Jaji  Gumendi na  Balozi  Manongi  yaliyofanyika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania,   Rais wa ICC aliishukuru Tanzania kwa hotuba yake   iliyotolewa na Balozi  siku ya Jumatatu wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  lilipopokea na  kujadilia Ripoti ya  ICC.

Kwa  mujibu wa  Rais wa ICC Jaji Slivia Fernandez  de Gumendi  hotuba  ya    hiyo ya  Tanzania  ilikuwa   yenye uwiano (balanced)  na pia  ilitoa  ushauri au mapendekezo ya namna gani  Mahakama hiyo  inavyoweza kuboresha uhusiano  na  wanachama wake  kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.
“  Nilikusikiliza  kwa makini sana  wakati  ulipokuwa unatoa hotuba  yako,   nilinukuu  kila  hoja   ulizokuwa unazizungumza . Hotuba   ya  Tanzania ilikuwa yenye  uwiano    (balanced) na ningependa  kuitumia   fursa hii kuishukuru   Tanzania kwa hilo.
Rais   huyo wa ICC amekiri kwamba anadhani ni wakati  muafaka  kwa wadau wa pande  mbili  kukaa na kuzungumza  kama ambayo  Tanzania  na wanachama  wengine wameshauri hasa kutokana na kile  alichosema, kwamba, kila nchi imekuwa na  tafsri  tofauti  na  uelewa tofauti  kuhusu baadhi  ya  vipengere  (articles) zinazohusu Mkataba wa Roma  unaounda  Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.
Kwa upande wake Balozi Manongi amesema,   ushauri na mapendekezo ambayo  yametolewa  na Tanzania pamoja na nchi nyingine hayalengi katika  kutaka  kubadili  Mkataba  wa Roma  au kuipunguzia  nguvu ya  kiutendaji  Mahakama hiyo.
“Tungependa sana  ieleweke kwamba tunaposhauri kukaa na kuzugumza  kusitafsiriwe kana kwamba tunataka kupunguza nguvu ya utendaji wa  chombo hiki ambacho  wote tunaamini kwamba  kinastahili kuwapo. Tunashosema na kusisitiza, kwamba   kila  upande unahoja  za msingi basi tuzijadili kwa kuzungumza” akasisitiza  Balozi  Manongi.
Rais wa  ICC na  Balozi Manongi  walibadilishana mawazo juu  na masuala mbalimbali kuhusu utendaji kazi wa Mahakama ya  ICC ikiwa ni pamoja na  kuangalia ni maeneo gani ambayo   Mahakama na wanachama  wake  wanaweza kujadiliana . 

No comments: