Advertisements

Monday, November 14, 2016

SAKATA LA KATIBA PENDEKEZWA, MPYA YAIBUKA, NI ALIKUWA MWANASHERIA MKUU ZANZBAR


Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Z’bar Mh. Otmani Massoud, akisindikizwa na walinzi wa bunge alipokuwa akitoka nje ya bunge maalum la katiba 2014

Othman, ambaye alijiondoa kwenye Kamati ya Uandishi wa Bunge la Katiba, aliibua mshangao Oktoba Mosi, 2014 wakati alipopiga kura ya kukataa baadhi ya vipengele vya Rasimu ya Katiba ambayo ilikuwa imeshasusiwa na vyama vya upinzani.

Zanzibar. Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ameeleza sababu zilizomfanya atoe msimamo binafsi kwenye Bunge la Katiba uliosababisha aachishwe kazi na Rais Ali Mohamed Shein.
Othman, ambaye alijiondoa kwenye Kamati ya Uandishi wa Bunge la Katiba, aliibua mshangao Oktoba Mosi, 2014 wakati alipopiga kura ya kukataa baadhi ya vipengele vya Rasimu ya Katiba ambayo ilikuwa imeshasusiwa na vyama vya upinzani.
Siku hiyo, Othman, ambaye hakuwa ameonekana kwenye Bunge hilo kwa muda mrefu, alipiga kura ya wazi akieleza kuwa anakataa ibara ya pili, tisa, 86, ibara za sura ya saba, 128 na 129.
Ibara hizo zinazungumzia Muungano, ukuu na utii wa Katiba na utaratibu wa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Wajumbe wa Bunge hilo walipotaka kujadili suala hilo, Spika Samuel Sitta (sasa marehemu) alikataa kuruhusu hoja hizo akisema haiwezekani kujadili kura ya mjumbe kwa kuwa ni kinyume cha Katiba. Baada ya uamuzi huo, Dk Shein alitangaza Mwanasheria Mkuu mpya.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wetu mjini Zanzibar hivi karibuni, Othman alisema Zanzibar haikwenda kwenye Bunge la Katiba ikiwa na msimamo wake na kwamba Dk Shein alishindwa kutetea visiwa hivyo.
Alisema wakati wa mchakato wa Katiba, wajumbe kutoka Zanzibar hawakuwahi kukutana na kujadiliana kwa pamoja jinsi ya kutetea masilahi yao, licha ya Rais Shein kushauriwa kuwakutanisha.
“Kosa la kwanza lililotokea kama Zanzibar, hata watu wengi walishauri kwamba tukae tuamue mambo yetu. Wakati ule kulikuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ya vyama viwili. Lakini hata siku moja haikutokea na wala mimi sikuwahi kupewa maelekezo ya kuitetea Serikali (ya Zanzibar) katika Bunge la Katiba.
“Kila mtu alikwenda kivyake kwenye Bunge la Katiba. Walikwenda na misimamo yao ya vyama. Kwa bahati mbaya mimi sifungwi na misimamo ya vyama hivyo viwili. Watu waliomba si mara moja si mara mbili kwa Rais kwamba tukae. Makamu wa Kwanza (wakati huo Maalim Seif Sharif Hamad) alikwenda kumuomba, mawaziri walikwenda kumuomba kwamba tukae tujadili masilahi ya Zanzibar, lakini hatukukutana,” alisema.
Alisema kilichomkera zaidi ni kuwekwa kwenye Kamati ya Uandishi wa Katiba ambayo alisema ilipewa maelekezo ya nini cha kuandika.
“Nakumbuka kanuni ya 35 inasema kazi ya Kamati ya Uandishi ni kukusanya yale yaliyotoka kwenye Kamati za Bunge. Sasa ugomvi wangu ulikuwa ni mambo yaliyojadiliwa kwenye hizo kamati, yalitokana na waraka wa CCM uliotoa maelekezo ya mambo yaliyotakiwa kuandaliwa,” alisema na kuongeza:
“Kwanza nilikuwa sikubaliani na mambo mengi yaliyojadiliwa kwenye hizo kamati. Pili, kwenye kuandaa hiyo ripoti ya chama, mimi sikushiriki ingawa kwa upande mwingine, Mwanasheria Mkuu wa wakati huo na wanasheria wengine walishirikishwa, akiwemo Jaji Fredrick Werema,” alisema.
“Ni sawa na kitu kimeshapikwa, sisi tunakwenda kupakua. Nikawaambia wenzangu kama mliona mimi ni mpishi mzuri, basi msingeniweka kwenye kupakua. Isije ikaonekana kuwa nilishiriki kwenye kuandaa haya mambo wakati hakuna kitu nitakachoongeza wala nitakachopunguza.”
Alitaja sababu nyingine kuwa ni wajumbe walioteuliwa kuandika Katiba Inayopendekezwa kuandaliwa kila kitu na mchakato kukosa misingi ya uandishi.
“Kwa hiyo sikutaka jina langu liwemo kwenye rasimu ambayo sikuiandaa, ndiyo maana nikajiondoa. Uzuri ni kwamba sikuteuliwa kwenye ile kamati kama Mwanasheria Mkuu (wa Zanzibar), bali niliteuliwa kama Othman, mjumbe wa Bunge la Katiba,” alisema.
Kabla ya kujitoa Kamati ya Uandishi , Othman alisema wajumbe wenzake kutoka Zanzibar, wakiwamo mawaziri wa Zanzibar walikutana na kuweka msimamo wa mambo manane kati ya 17 waliyotaka yaingizwe kwenye Katiba hiyo, lakini baadaye yalikataliwa.
“Yale mambo 17 yaliandaliwa na baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar na yakaletwa kwenye kamati ya mawaziri kutoka Zanzibar iliyokuwa ikiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais (Balozi Seif Ali Iddi) na mawaziri wengine waliokuwa Zanzibar na mimi wakanialika,” alisema.
“Niliwaambia kwamba hayo mambo 17 yote ni ya msingi, lakini kwa hapa tulipofika ni vizuri tuchague mambo ambayo wote tutakubaliana. Wenzetu wakiyakataa basi sisi hatuna haja ya kuendelea.”
Aliyataja mambo waliyoyachagua kuwa ni pamoja na uwezo wa Rais wa Muungano kugawa mipaka ya Zanzibar, akisema walitaka Rais wa Zanzibar awe na mamlaka hayo kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1982.
“Tulisema hivyo kwa sababu ukishampa Rais wa Muungano kugawa mipaka na wilaya, hujui atakuja rais wa aina gani. Kwa nini asiseme Zanzibar ni mkoa au wilaya au shehia? Tukasema hapana,” alisema.
Alitaja jambo la pili kuwa ni ukuu wa Katiba, akisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano isiguse mambo yasiyo ya Muungano ambayo yatakuwa chini ya Katiba ya Zanzibar.
Alitaja pia suala la ardhi ambalo awali lilikuwa chini ya Muungano, akisema lilipaswa kuwa chini ya Zanzibar. Alisema suala jingine ni jinsi ya kumpata Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kutumia wingi wa kura, jambo ambalo alisema haliwezekani, akipendekeza Rais apate japo asilimia 20 ya kura za Wazanzibari ndipo ahesabike kuwa mshindi.
“Unaweza ukafika mahali, Rais wa Muungano akachaguliwa lakini Zanzibar asipate kura hata moja. Au chama cha Rais wa Muungano kikapata kura Bara lakini Zanzibar kisipate hata kura moja. Sasa unajiuliza huyo ni Rais wa Muungano kwa uhalali upi?” alihoji.
“Wenzetu Kenya wana utaratibu kwamba Rais akichaguliwa kuna majimbo lazima akubalike. Marekani pia wana utaratibu kwamba zile ‘collegiate’ lazima Rais apate zote. Kwa mfano ukichukua jimbo la California lina watu kama milioni 34, lakini kuna majimbo kama Maine lina watu kama milioni moja kama Zanzibar.”
Aliyataja mambo mengine kuwa ni mfumo wa kodi, suala la kupiga kura ndani ya Bunge na kubadilisha mfumo wa Serikali. Alitaja pia kero ya wabunge wa Zanzibar kutokuwa na nguvu ya uamuzi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, akisema ndiyo kubwa aliyoipigania.
“Kwa mfano ukiangalia tatizo kubwa lililopo ni wale wabunge wa Zanzibar wanaokwenda Bunge la Muungano, wakifika kwenye mambo ya Muungano, hawana sauti ya kuamua. Inaweza ikapitishwa Sheria ya Muungano na wabunge wa Zanzibar wakakubali au wasikubali, uamuzi unafanywa kwa wingi wa kura za Bara,” alisema.
“Sisi tunajiuliza, wabunge wa Zanzibar kama hawana sauti kwenye mambo ya Muungano, wanakwenda kufanya nini pale? Kuna haja ya kuwa na wabunge wa Zanzibar kama hawana sauti?
“Hiyo ni kero ya muda mrefu. Kwa mfano kuna Sheria ya Uvuvi imepitishwa miaka 10 iliyopita, lakini haitekelezeki. Kwa sababu imepitishwa kwa utaratibu huu wa ajabu, Zanzibar imekataa kuitekeleza.”
Alisema waliyajadili mambo hayo wakiwa na mawaziri wa Zanzibar, lakini baadaye wakabadilika.
“Baadaye wakasema jamani tumeshakaa hapa tumekula pesa ya watu, tupitisheni tu kwa sababu hayataingia kwenye Rasimu ya Katiba. Waliponifuata nilikataa kwa sababu kumbukumbu inayobaki hapo ni Katiba Inayopendekezwa,” alisema.
Alisema baada ya uamuzi wake wa kujitoa Bunge Maalumu la Katiba, Rais alimuita na kumtaka ajiuzulu, lakini akakataa.
“Aliniita akaniambia kwa jinsi mambo yalivyokwenda, itabidi huu mzigo nikutue. Nikasema kwa sababu wewe ndiye uliyenitwika, una haki ya kunitua. Katika uamuzi huo aliniambia ama nijiuzulu au anifukuze,” alisema na kuongeza:
“Kubwa nililouliza, what is my offence (kosa langu nini)? Maana mimi sijatofautiana na Serikali, sijatofautiana na wenzangu, sijatofautiana na wewe Rais kwamba ulinipa maagizo sikuyafanya, badala yake ninyi ndiyo mmegeuka. Nieleze, tatizo, nimefanya nini? Kama sikufanya kosa basi bora unifukuze ili iwekwe kwenye kumbukumbu kwamba ulinifukuza.”
Akieleza zaidi kuhusu hatua hiyo ya kufukuzwa, Othman alidai kwamba ilikuwa ni kwa shinikizo la CCM Bara japo aliteuliwa na Rais wa Zanzibar.
“Mimi naamini niliteuliwa na Rais wa Zanzibar na nikatolewa na makamu mwenyekiti wa chama, yaani ananihukumu kwa msimamo wa chama, si kama Rais ambaye anakubali kwa msimamo wake nifanye na mimi sikufuata.
“Ni shinikizo alilolipata kutoka chama chake ndiyo lililomfanya anifukuze, lakini kama Rais wa Zanzibar. Hatukuwa na tofauti, maana yote tuliyomshauri, mawaziri wake waliyakubali na hata Makamu wa Pili wa Rais alikubali. Sasa hapa kilitokea nini, hilo anajua mwenyewe,” alisema.

Chanzo
By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

No comments: