Advertisements

Thursday, November 3, 2016

Wapakistani watupwa jela miaka minne

Raia wa Pakistani ambao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya shughuli za mawasiliano bila kuwa na kibali maalumu cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TCRA), wakiongozwa na askari Magereza baada ya kesi yao kutolewa hukumu katika Mahakam ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana. (Picha na Mroki Mroki).
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu raia watatu wa Pakistan, kifungo cha miaka minne jela au kulipa faini ya Sh milioni 125 baada ya kupatikana na hatia ya kuingilia mtandao wa mawasiliano na kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 145.

Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, alitoa hukumu hiyo baada ya washtakiwa, Hafees Irfan, Mirza Irfan Baig na Mirza Rizwani Baig, kukiri makosa yao.

Akitoa adhabu hiyo, Hakimu Mwijage alisema, washtakiwa wamepatikana na hatia ya makosa manne na katika kila kosa watalipa faini ya Sh milioni tano au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, ambayo ni sawa na faini ya Sh milioni 20 au kifungo cha miaka minne jela.

Aidha, alisema kwa sababu mashtaka yanahusisha kuisababishia hasara Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), kila mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 35, pia washtakiwa wakimaliza kutumikia vifungo vyao, warud ishwe nchini kwao na vifaa walivyokutwa navyo vitakuwa mali ya serikali.

Awali, kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Esther Martin aliwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali na kudai kuwa katika tarehe tofauti, Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa na vifaa vya kuunganishia mawasiliano ya kimataifa bila kuwa na kibali cha TCRA.

Alidai, washtakiwa walitoka Pakistan na kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo Arab Emirates, Malaysia, Msumbiji kwa ajili ya kutumia vifaa hivyo, pia waliingia nchini katika tarehe tofauti na kufikia kwenye chumba namba 905 katika Hoteli ya Butterfly iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam.

Inadaiwa wakiwa kwenye chumba hicho, waliunganisha mawasiliano kwa kutumia vifaa vya kimataifa bila kuwa na kibali cha TCRA, lakini wakati wakiendelea na kazi zao ilibainika kuwa, kuna watu katika maeneo hayo wanatoa huduma ya mawasiliano, kinyume cha sheria.

Aliendelea kudai kuwa, Oktoba 5, mwaka jana, maofisa wa Polisi wakiambatana na TCRA walifika maeneo hayo na kufanya upelelezi, kisha wakawakamata washtakiwa hao katika hoteli wakiwa na vifaa mbalimbali vya mawasiliano, ambavyo ni kadi za simu 273, CPU 18, Laptop saba, Moderm ya Huawei na vocha zilizokwishatumika.

Washtakiwa walifikishwa kituo cha Polisi Kijitonyama na baada ya kufanya upelelezi, ilibainika kuwa wameisababishia serikali na TCRA hasara ya Sh milioni 140.

Baada ya kusomewa maelezo yao, washtakiwa walikiri makosa. Wakili Esther aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine na makosa hayo, yasiwe yanajirudia rudia, adhabu itolewe kwa kuzingatia hasara walioisababisha washtakiwa, pia alidai makosa hayo yanahatarisha usalama wa taifa.

Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Shadrack Ishengoma aliiomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu hiyo washtakiwa kwa sababu wamekiri makosa yao, pia wanategemewa na familia zao, na kuongeza kuwa washtakiwa wameshakaa rumande kwa miezi 13 yaani zaidi ya mwaka mmoja.

Hakimu Mwijage alisema ametoa adhabu hiyo kwa kuzingatia hoja za pande zote mbili na washtakiwa walilipa faini na kuachiwa

HABARI LEO

No comments: