MKAZI wa Mtaa wa Migombani, Kata ya Kaloleni, Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Edmound Josephat (30), amekutwa akiwa amefariki dunia nyumbani kwake baada ya kudaiwa kunywa pombe akiwa hajala.
Wakizungumza na MTANZANIA jana, wakazi wa eneo hilo walisema Josephat alifariki juzi baada ya kunywa pombe bila kula.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Songwe, Mathius Nyange, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema alipata taarifa kutoka kwa wananchi kijijini hapo.
“Nilipata taarifa kutoka kwa wananchi wa mtaa huo ambao baadaye waliuchukua mwili wa marehemu kwa uchunguzi.
“Baadaye waliuchukua mwili huo na kuupeleka hospitalini ambako iligundulika marehemu alikuwa amekunywa pombe kali bila kula ingawa haikujulikana ni pombe ya aina gani,” alisema Kamanda Nyange.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Nyange aliwataka wananchi kuacha tabia ya kunywa pombe kali bila kula kwa kuwa kufanya hivyo wanahatarisha maisha yao.
“Pamoja na hayo, tunaangalia namna ya kuanza kufanya operesheni ili kuwabaini wanaokunywa pombe wakati wa kazi na wale wanaokunywa pombe haramu zilizopigwa marufuku,” alisema.
Pia, alisema wataanza kuwabana wanaoingiza pombe kutoka nchini Zambia na Malawi kwa kuwa zimekuwa zikiua watu mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment