ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 27, 2016

BODABODA WAFUNZWA KUNYWA POMBE KISTAARABU

KATIKA kuunga mkono jitihada za serikali za kupunguza ajali za barabarani nchini, Kampuni ya TBL Group imedhamini mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha bajaji na bodaboda wanaofanyia kazi zao katika kituo cha Ubungo Maji, Dar es Salaam yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Madereva pia walipata fursa ya kupata mafunzo ya unywaji wa kistaarabu ambayo yanaelekeza kutumia vinywaji vyenye kilevi kistaarabu na kuhakikisha utumiaji wake hauleti athari yoyote. Walikumbushwa kutoendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia vinywaji vyenye kilevi.
Meneja wa Masuala Endelevu wa TBL Group, Irene Mutiganzi alisema kampuni imedhamini mafunzo hayo yaliyotolewa na maofisa kutoka Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani ukiwa ni mwendelezo wa kampuni hiyo kuendesha kampeni za usalama barabarani.
“Tukiwa kampuni inayotengeneza vinywaji vya aina mbalimbali vyenye kilevi tunalo jukumu pia kuunga mkono jitihada za serikali kupunguza matukio ya ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikisababisha vifo vya watu wengi na
hasara kubwa, Hivyo tunatoa mwito kwa madereva wote hususani wa vyombo vya moto katika msimu huu wa sikukuu kuwa makini kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazotokana na uzembe wa kutozingatia sheria na kanuni za usalama barabarani,” alisema.
Aliongeza kuwa, kampuni itaendelea kuunga mkono jitihada za serikali na wadau wengine wa masuala ya usalama barabarani ili kutokomeza matukio ya ajali nchini.
Alisema hivi sasa kampuni inaendesha mafunzo ya unywaji wa kistaarabu kwa makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya madereva.
Alisema elimu hiyo itaendelea kutolewa katika kipindi cha mwaka ujao ili iwafikie Watanzania wengi na kubadilisha jamii kuwa na utamaduni wa utumiaji wa vinywaji vyenye kilevi bila kusababisha athari zozote kutokana na utumiaji huo.
“Kampuni pia imekuja na mkakati wa kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inawafikia wanafunzi wa shule za msingi ili wakue wakiwa na uelewa wa umuhimu wa kuzingatia kanuni za usalama barabarani.
Alisema kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imeanza kuendesha mafunzo kwa wanafunzi wa shule za msingi katika mikoa mbalimbali nchini.

No comments: