Advertisements

Friday, December 9, 2016

SAKATA LA KUUAWA KWA FARU JOHN LACHUKUA SURA MPYA, WATUMISHI WATANO WATIWA MBARONI

Maofisa watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wanaotuhumiwa kushiriki kumwondoa faru John kutoka katika Creta hiyo walikamatwa juzi kwa mahojiano ili kujua ukweli kuhusu mazingira ya kupotea kwake. 

Hatua ya maofisa hao kukamatwa imekuja siku tatu baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuituhumu menejimenti, wafanyakazi wa NCAA na Baraza la Wafugaji (NPC) kuwa imejaa vitendo vya rushwa na wizi na asingeweza kuvumilia sakata la faru John ambaye alisema kuwa aliuzwa kwa Sh200 milioni kwenye Hoteli ya Grumet iliyo Hifadhi ya Serengeti na kuwa walipokea fedha za awali Sh100 milioni. 

Waziri Mkuu alisema anataka kumwona faru huyo, nyaraka za kumhamisha na kama amekufa basi apelekewe hata pembe ofisini kwa kuwa anajua pa kuzipeleka. 

Alisisitiza kuwa ikibainika kuna ambao wamekiuka taratibu watawajibika. 


Habari za uhakika kutoka Ngorongoro, ambazo zimethibitishwa na Jeshi la Polisi zinasema kuwa maofisa hao watano wanashikiliwa katika kituo chao cha Ngorongoro kutokana na ushiriki wao kwa njia moja au nyingine. 

Wanaoshikiliwa ni pamoja na Israel Naman ambaye alikuwa Kaimu mkuu wa idara ya uhifadhi wakati faru huyo akiondolewa. 

Wengine ni Cuthbert Lemanya, ambaye alikuwa Mkuu wa Kanda ya Creta, Dk Athanas Nyaki ambaye anadaiwa kumdunga sindano ya usingizi ili aweze kubebwa. 

Maofisa wengine waliokamatwa ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka ya Ngorongoro, Kuya Sayaleli na aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Ikolojia, Patrice Mattey. 

Ofisa mmoja wa NCAA, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake jana alisema maofisa hao walikamatwa juzi jioni na jana walikuwa wanaendelea kuhojiwa. 

“Tuiache serikali ifanye kazi kwani ni muhimu sana kujulikana ukweli wa tukio hili,” alisema ofisa huyo. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo hakupatikana jana kuelezea tukio la kukamatwa maofisa hao, baada ya simu yake kupokelewa na msaidizi wake ambaye alieleza yupo kwenye kikao. 

Lakini, ofisa wa mmoja wa polisi, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina kwa kuwa si msemaji alikiri kukamatwa maofisa hao kwa mahojiano. 

Chanzo cha sakata 
Akiwa katika ziara ya kikazi Ngorongoro, Waziri Majaliwa aliibua sakata la kuhamishwa kinyemela faru huyo na kudaiwa kupelekwa Grumet. 

Waziri mkuu alitaka ukweli kuhusu upotevu wa John aliyeondolewa Creta na kupelekwa Grumet na kudaiwa kufa huku taarifa za kifo hicho zikifanywa siri. 

Waziri Mkuu alitaka kupewa nyaraka zote zilizotumika kujadili kumuondoa faru na kuamua kumpeleka Grumet. 

Waziri Mkuu alitoa hadi Desemba 8 (jana) awe amepata taarifa zote, ikiwamo ya daktari inayothibitisha kifo hicho na kwamba pembe za faru huyo zifikishwe ofisini kwake. Pia, Majaliwa alisema ikibainika wapo waliokiuka taratibu watawajibika. 
 

No comments: