ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 20, 2016

SERIKALI YAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUJENGA VIWANDA VYA MIFUGO.

Na Ismail Ngayonga MAELEZO

SERIKALI imewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujitokeza na kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya malighafi ya mazao ya mifugo nchini ili kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati.

Hayo yamebanishwa (jana) leo Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Maria Mashingo wakati wa mahojiano maalum ya kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na kurushwa hewani na Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC).

Dkt. Mashingo alisema Serikali ya Awamu ya tano imekusudia kuifanyia mageuzi makubwa sekta ya mifugo nchini ili kuhakikisha kuwa sekta hiyo italeta tija na kuongeza mchango wake katika pato la taifa kutoka kiwango cha asilimia saba iliyopo sasa.

“Tumepanga kuhakikisha kuwa mazao ya mifugo yanatumika kikamilifu katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda vidogo vidogo na vya kati, kwa kuwa Tanzania imebahatika kuwa na wanyama na ndege aina zote” alisema Dkt. Mashingo.

Kwa mujibu wa Dkt. Mashingo alisema Serikali imeendelea kuwasiliana na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo na kutengeneza mazingira bora zaidi ya kuwekeza katika viwanda vya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya mifugo ikiwemo nyama, maziwa, mayai pamoja ngozi.


Aliongeza kuwa katika kutekeleza adhma hiyo, Serikali imendaa mpango mkakati wa miaka mitano wa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ikiwemo maziwa, ambapo imepanga kuongeza idadi ya uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka 800,000 iliyopo sasa hadi kufikia Milioni 4.

“Kiasi hicho cha ng’ombe kitasaidia kuongeza idadi ya uzalishaji wa lita za maziwa kutoka lita Milioni 2  hadi kufikia lita Milioni 4-6, na ziada hiyo itaweza kusambazwa katika shule kwa kuwa wanafunzi wengi wanahitaji kiasi kikubwa cha jibini na vitamin katika ukuaji wao” alisema Dkt. Mashingo.

Aidha Dkt. Mashingo alisema mkakati huo wa Serikali umelenga katika kuhamasisha wananchi na wadau wa mifugo kuweza kuboresha rasilimali za mifugo ili ziweze kuzalisha bidhaa bora zenye uwezo wa kumudu ushindani wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Akifafanua zaidi alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kuvutia wawekezaji ikiwemo kuongeza ubunifu katika tafiti mbalimbali za mazao ya mifugo nchini ikiwemo uzalishaji wa mbegu bora za mifugo, hatua inayolenga kuongeza thamani ya rasilimali hizo.

No comments: