Monday, December 26, 2016

Taarifa ya kusikitisha kutoka kata ya masanze jimbo la mikumi.

 OFISI YA MBUNGE Jimbo La Mikumi inalaani sana kitendo cha kinyama kilichofanywa na Ndugu zetu wa jamii ya wafugaji kwa kujichukulia sheria mkononi na kumjeruhi vibaya Ndugu Augustino Mtitu mkulima wa kitongoji cha Upangwani, Kijiji cha Dodoma Isanga, Kata Ya Masanze Jimbo la Mikumi ambapo leo tarehe 25 Desemba majira ya Mchana amechomwa mkuki mdomoni na kutokezea nyuma ya shingo yake, ambapo alipelekwa hospitali ya wilayani Kilosa na baadae amekimbizwa hospitali ya mkoa Morogoro  ili kufanyiwa operesheni ya kuondoa mkuki huo na kwa matibabu zaidi.

Augustino Mtitu alishambuliwa na wafugaji wa kimasai alipokuwa akimsaidia jirani yake kufukuza Ng'ombe wasiharibu mazao shambani kwake, Kipande cha mti kinachoonekana hapo mdomoni ndiyo mkuki uliokatwa ili kupunguza urefu wa mkuki huo wakati wakimkimbiza hospitali,  Inasemekana MwenyeKiti wa kijiji na MwenyeKiti wa kitongoji hicho nao wamejeruhiwa.


WITO KWA SERIKALI.
Ofisi Ya Mbunge Mikumi inatoa wito kwa Serikali  kuwabaini wale wote waliofanya kitendo hiki cha kinyama kuhakikisha wanachukuliwa hatua kali za kisheria  ili kuweza kukomesha vitendo hivi vya kujichukulia sheria mkononi inayopelekea kuongezeka kwa uvunjifu mkubwa wa Amani na migogoro isiyokwisha kati ya wakulima na wafugaji wilayani KILOSA.

Imetolewa na:-
Robert A. Galamona
Katibu Ofisi Ya Mbunge
Mikumi.

1 comment:

Anonymous said...

Kwa kweli jambo hili ni hatari sana kwa usalama vijijini ambako ndiko kwenye matumaini. Kwanini uvunjifu wa amani huu haukomeshwi kwa kuwataifisha ng'ombe na kumfunga mchungaju na mwenye ng'ombe kifungo cha miaka 30. Mara kadhaa ng'ombe wameingia shambani kwangu na dadab yangu aliogopa na wakaharibu mazao yangu walivyotaka. Hata ukienda police, wakifikishwa huko inakuwa hatari kwa maisha ya mkulima! Watakuja kundi na kukushambulia! Ni hatari! Ni hatari! Ni hatari! Ulinzi wa nchi ni pamoja na kukomesha mambo HATARI kama haya.