WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewashukuru na kuwapongeza madaktari wa Taasisi ya Bilal Muslim Tanzania ambayo imetoa huduma ya matibabu ya macho kwa zaidi ya wananchi 4,000 wa mkoa wa Dodoma
Ametoa pongezi hizo jana usiku (Jumapili , Desemba 11, 2016) wakati akizungumza na madaktari waliotoa huduma hiyo walipomtembelea katika makazi ya Waziri Mkuu mkoani Dodoma
Waziri Mkuu alisema huduma wanayoitoa ni muhimu kwa kuwa imewezesha watu ambao walikata tamaa ya kuona wameona, hivyo aliwaomba waendelee kwenda katika maeneo mengine nchini ili Watanzania wengi zaidi waweze kunufaika.
"Nawashukuru kwa mchango mkubwa mnaoutoa katika kuunga mkono jitihada za Serikali kwenye utoaji wa huduma za matibabu ya macho bure na kuwawezesha hata wale wasiokuwa na uwezo kupata huduma ," alisema .
Serikali ya awamu ya Tano ina dhamira ya dhati kuwatumikia wananchi na kutoa huduma kwa wote , hivyo tuko tayari kushirikiana na taasisi yeyote ambayo inakusudia kuwafikia wananchi.
Waziri Mkuu alisema “katika utoaji huduma za jamii , Serikali inathamini sana mchango wa taasisi binafsi na za dini ambazo ziko mstari wa mbele kushirikiana na jamii kwa ujumla,”.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwakaribisha madaktari hao kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali mkoani Dodoma. “Hapa ndio makao makuu ya Tanzania , hivyo nawakaribisha mje kuwekeza, ardhi ya kutosha ipo . Mnaweza kuja kujenga hospitali kubwa ya macho," alisema .
Naye Naibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Mheshimiwa, Anthony Mavunde alisema jumla ya watoto 250 wamefanyiwa upasuaji wa macho na madaktari hao ambao walianza kutoa huduma hiyo Desemba 8, 2016 na wanatarajiwa kumaliza Desemba 12, 2016
"Nawashukuru kwa moyo wenu wa kujitolea kuja kusaidia watu wenye mahitaji ya matibabu ya macho . Mkoa wa Dodoma una changamoto kubwa ya matatizo ya macho .Nimefarijika sana kuona baadhi ya akinamama waliokuwa wamekata tamaa ya kuona wameweza kuona tena,” alisema.
Naye Mtaribu wa taasisi hiyo, Noorelain Sharrif alimuahidi Waziri Mkuu kwamba wataendelea kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma za matibabu ya macho bure kwa wananchi wenye mahitaji na wako tayari kwenda popote nchini kutoa huduma hiyo
“Tuko tayari kushirikiana na Serikali katika kutimiza wajibu wetu kwa jamii , tutafanya hivyo wakati wowote na kwa wananchi wote,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, DESEMBA 12, 2016.
No comments:
Post a Comment