ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 2, 2016

YANGA KUTUMIA UWANJA WA TAIFA KWA MICHEZO YA LIGI KUU NA KIMATAIFA

 Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akisaini Mkataba kwa niaba ya Serikali na Klabu ya Yanga ya jijini Dar es salaam ambayo iliwakilishwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu hiyo Baraka Deusdedit (kulia) leo jijini Dar es salaam. Mkataba huo unahusu Klabu ya Yanga kutumia Uwanja Mkuu wa Taifa na Uwanja wa Uhuru katika mechi za Kimataifa na Ligi Kuu. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Evordy Kyando. 
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akibadilishana Mkataba waliosaini na Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga Baraka Deusdedit leo jijini Dar es salaam.  Mkataba huo unahusu Kalabu ya Yanga kutumia Uwanja Mkuu wa Taifa na Uwanja wa Uhuru, Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Alex Nkenyenge.
Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) mara baada ya kusaini Mkataba na Klabu ya Yanga leo jijini Dar es salaam. Wa pili kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga Baraka Deusdedit.

Na Eleuteri Mangi – WHUSM
Serikali imesaini Mkataba na Klabu ya Yanga kutumia Uwanja Mkuu wa Taifa pamoja na Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya michezo yote ya Kimataifa pamoja na michezo ya Ligi Kuu ya ndani.
Mkataba huo umesainiwa leo jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya Serikali na Kaimu Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga Baraka Deusdedit kwa niaba ya Klabu ya Yanga.
Katika Mkataba huo, Klabu ya Yanga imeruhusiwa kutumia viwanja hivyo kama viwanja vyake vya nyumbani kwa sharti la kuvitunza viwanja hivyo wakati wote wanapovitumia.
Miongoni mwa masharti hayo ni kutunza viwanja, mali na vifaa vyote vilivyopo katika viwanja hivyo, na endapo kutatokea uharibifu wowote utakaofanywa na wachezaji ama mashabiki, Klabu hiyo itawajibika kubeba gharama za matengenezo yote yatakayotokana na uharibifu huo.
Aidha, Klabu ya Yanga inaweza kutumia viwanja hivyo kwa mazoezi ya kujianadaa na mechi zinazowakabili.

No comments: