Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akipokewa na Rais wa Jumuiya ya Ismailia Tanzania Bwana Amin Lakhani kwenye Maulidi ya Uzawa wa Mtume Mhammad (SAW) yaliyoandaliwa na Jumuiya hiyo hapo Upanga Mjini Dar es salaam. Kati kati yao ni Mwakilishi wa Agakhan upande wa Zanzibar Bwana Mohame Bhaloo.
Mkurugenzi wa masuala ya Taaluma na Dini ya Kiislamu na Historia wa Jumuiya ya Isimailia Tanzania Dr. Amin Rehmani akichambua masuala mbali mbali ya Dini ya Kiislamu kwenye muhadhara huo wa Maulidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akihutubia kwenye hafla ya Maulid ya Uzawa wa Mtume Muhammad (SAW) ya Jumuiya ya Ismailia Jijini Dar es salaam.
Maustadhi wa Madrassah Shahdiliyah ya Jijini Dar wakiongoza waumini wa Dini ya Kiislamu Kwenye Mlango wa Nne wa Maulidi ya Barzanji ambapo waislamu hunyanyuka kutoa heshima ya kisimamo katika kumtukuza Kiongozi wa Dini hiyo Nabii Muhammad (SAW).
Waumini wa Dini ya Kiislamu wakipakwa mafuta mazuri ya maradhi katika kisimamo cha mlango wa Nne wa Maulid ya Barzanji ya kumtukuza Mtume Muhammad (SAW) hapo Upanga Jijini Dar es salaam.
Rais wa Jumuiya ya Ismailia Tanzania Bwana Amin Lakhani Kulia akimzawadia Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi kwa ushiriki wake wa Maulidi yaliyoandaliwa na Jumuiya hiyo.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Sheikh Alhadi Mussa Salum (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Rais wa Jumuiya ya Ismailia Tanzania Bwana Amin Lakhani kutokana na kuthaminiwa kwa mchango wake uliofanikisha kufanyika kwa Maulidi hayo.
Mwenyekiti wa Baraza la Kiislamu Tanzania (BAKWATA) upande wa Wanawake Bibi Shamim Khan naye akipokea zawadi katika hafla hiyo ya Maulid.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Maulidi ya Uzawa Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Ismailia Upanga Mjini Da es salaam.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Maulidi ya Uzawa Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Ismailia Upanga Mjini Da es salaam.
Sheikh wa Jumuiya ya Darkhana Jamat Alfaran Dewji akisoma fatha ya kufunga hafla ya Maulidi ya Uzawa wa Mtume Muhammad (SAW) ya Jumuiya hiyo.
Viongozi Wakuu pamoja na waumini wa Dini ya Kiislamu wakiitikia dua ya kufunga rasmi kwa hafla hiyo ya Maulidi hapo Upanga Mjini Dar es salaam.
Balozi Seif pamoja na Viongozi mbali mbali wakiangalia machapisho mbali mbali vya Dini ya Kiislamu na Historia yake vilivyoandaliwa na Jumuiya Ismailia katika monyesho maalum yaliyofanyika katika hafla hiyo ya Maulid. Picha na OMPR, ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini kuendelea kumpenda Kiongozi wao Mtume Muhammad { SAW } ili wapate fadhila zilizo bora zaidi kwao zitakazowajengea hatma njema ya maisha yao ya sasa na yale ya baada ya ufufuo.
Alisema amri ya kuwataka waumini wa Dini ya Kiislamu ya kumpenda Kiongozi wao imo ndani ya Kitabu Kitukufu cha Quran ambacho kinavunja hoja ya baadhi ya watu wanaopinga mikusanyiko ya Maulid ya Uzawa wake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo katika sherehe ya Maulidi ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad { SAW } yaliyoandaliwa na Baraza la Agakhan na kufanyika katika Ukumbi wa Prince Agakhan Shia Imami Ismaili Jamati Khana Bara bara ya Ali Hassan Mwinti Upanga Jijini Dar es salaam.
Alisema zipo aya tofauti za Quran zinazoonyesha amri ya Mwenyezi Muungu inayowataka Waumini wa Dini ya Kiislamu kumfurahia Kionghozi huyo kwa sababu imethibiti ndani ya Kitabu hicho kwamba Mtume Muhammad {SAW} ni rehma kwa viumbe vyote.
Balozi Seif aliweka wazi kwamba mikusanyiko hiyo ya hafla za Maulidi ya Mtume Muhammad {SAW} ni nafasi nzuri ya kutekeleza agizo la Mwenyezi Muungu Mola wa Viumbe vyote katika kuenzi na kuzitukuza ishara za Dini ya Kiislamu.
Alisema inashangaza kuona baadhi ya watu wanamkejeli na kumdhihaki Mtume Muhammad { SAW} na kudiriki kusema kwamba haistahiki Waislamu kukusanyika katika hafla za Maulidi kwa ksingizio cha kuwa yeye ni sawa na binaadamu yeyote yule.
Alisisitiza kwamba waumini wa Dini nyengine pamoja na wanyama wanauelewa utukufu, hadhi, Heshima pamoja na Daraja aliyobarikiwa Kiongozi huyo akatolea mfano wa utukufu huo ni kisa cha ngamia aliyekasirika na kuamua kushtaki kwa Mtume Muhammad {SAW} visa anavyofanywa na Bwana wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa wito kwa Waumini wa Dini ya Kislamu pamoja na Wananchi wote kuendelea kushikamana, kupendana lakini la muhimu zaidi ni kudumisha Amani na Utulivu kama alivyokuwa akipenda Kiongozi huyo.
Alisema amani na utuilivu wa Taifa ndio kila kitu katika kudumisha furaha, kuondoa umaskini kwa kushiriki katika harakati za maendeleo kupitia hali ya utulivu ambayo ni jukumu la kila mwa Jamii wa Taifa hili la Tanzania.
Balozi Seif aliishukuru na kuipongeza Agakhan kupitia Jumuiya ya Ismailia kwa mpango wake wa kuendeleza kuunga mkono Serikali zote mbili Nchini Tanzania katika uwekezaji wa Miradi mbali mbali ya Maendeleo bara na Zanzibar.
Alisema matengenezo ya baadhi ya majengo yaliyofanywa na Agakhan ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar yamekuwa kivutio kizuri kinachosaidia kuongeza mapato ya Taifa kutokana na ongezeko kubwa la watalii na wageni wanaoingiza Zanzibar kupitia sekta ya Utalii.
Mapema Rais wa Jumuiya ya Ismailia Bwana Amin Lakhani alisema Agakhan itaendelea kuimarisha miradi ya Uwekezaji katika Sekta ya Afya, Elimu, Biashara pamoja na Utalii ndani ya Ukanda wote wa Afrika Mashariki.
Bwana Amin alisema zaidi ya miaka 50 sasa Jumuiya hiyo imekuwa ikitoa huduma katika sekta hizo katika Mataifa 25 Ulimwenguni zikiwemo pia nchi za Bara la Afrika ambazo kwa wakati huu zinasaidia kutoa ajira hasa kwa makundi ya Vijana wa Mataifa hayo.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika hafla hiyo Makamu wa Rais wa Jumuiya ya Ismailia Tanzania Bwana Kamal Khimji alisema Jumuiya ya Ismailia huandaa Maulidi ya Uzawa wa Nabii Muhammad {SAW} kwa lengo la kutekeleza Sera alizoziacha Kiongozi huyo ili waziendeleze katika kipindi chote cha maisha yao.
Bwana Kamal alisema Mtume Muhammad {SAW} ni kigezo cha tabia njema kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu wanachopaswa kukitumia katika mafunzo yao ya Dini pamoja na mfumo wao wa kimaisha.
Maulidi hayo ya uzawa wa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Duniani Mtume Muhammad { SAW } yaliyoandaliwa na Baraza la Agakhan Tanzania yaliambatana pia na maonyesho ya Vitabu mbali mbali vya Dini ya Kiislamu ambapo washiriki hao walipata fursa ya kuviangalia.
Mkurugenzi wa Taaluma ya masuala ya Dini ya Kiislamu na Historia wa Jumuiya hiyo Dr. Amin Rehmani aliwaeleza washiriki wa maonyesho hayo kwamba utaratibu huo wa maonyesho umeandaliwa kuwapa picha na njia waumini wa Dini hiyo kujenga tabia ya kupenda kujifunza Dini yao.
Dr. Amin alisema hatua hiyo itawapa uelewa na fursa nzuri Waumini wa Dini ya Kiisalamu kujenga hoja dhidi ya wapinzani wao wanaojaribu kuzitumia kinyume aya za Quran katika azma ya kuwapotosha Waumini wa Dini hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
21/1/2017.
No comments:
Post a Comment