ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 12, 2017

Kesi ya Mke wa Bilonea Msuya Yaahirishwa Tena

DAR ES SALAAM: MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajiwa kutoa uamuzi wa kumwachia  ama kutomwachia huru mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya aitwaye Miriam Mrita (41) na mwenzake ambaye ni mfanyabiashara, Revocatus  Muyela (40), wanaotetewa na mawakili Peter Kibatala na John Mallya  ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 23 mwaka huu.

Uamuzi huo ulitolewa leo mahakamani hapo kutokana na upande wa serikali kushindwa kubadilisha hati ya mashtaka ya kesi hiyo ndani ya siku mbili kama ilivyoamliwa Januari 9, mwaka huu.
 Januari 9, 2017 Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa, aliuamuru upande wa serikali kubadilisha hati ya mashitaka ndani ya siku mbili ambapo   alisema uamuzi huo  unatokana na kupitia hoja za pande zote mbili na kubaini kuwa hati ya mashitaka ilikuwa na mapungufu mawili likiwemo la kutoonyesha kama kuna mtu ambaye amesababisha kifo kwa mtu mwingine.

Pia alisema hati hiyo haionyeshi mtu aliyesababisha kifo kwa mtu mwingine kama alikuwa na nia ovu ya kutenda kosa hilo.
 Akizungumza mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mwambapa, wakili upande wa serikali, Kishenyi Mutalemwa, alidai kuwa muda waliopewa kuwasilisha hati hiyo ni mdogo kwa hiyo hawajaweza kutekeleza oda waliyopewa hivyo wanaiomba mahakama iwapatie tarehe nyingine.
 Mutalemwa alidai kuwa suala la hati linahitaji umakini hivyo waliomba kupewa muda mwingine kukamilisha jambo hilo.
 Wakili wa utetezi, John Mallya,  alidai amri iliyotolewa mahakamani hapo ni ya kisheria hivyo  upande wa jamhuri ulitakiwa kutekeleza ama kukata rufaa lakini umeshindwa kufanya hivyo.
 Mallya alidai kutokana na upande wa serikali kushindwa kutekeleza amri hiyo  aliiomba mahakama iwaachie huru washitakiwa kwa sababu hakuna hati sahihi ya mashtaka inayowafanya waendelee kushitakiwa.
Akijibu hoja hiyo,  Wakili Mutalemwa alidai hawajashindwa kuleta hati hiyo lakini kama alivyosema awali, alikuwa anaomba kuongezewa muda zaidi wa kukamilisha suala hilo  ambapo wataweza kuieleza mahakama kama watakata rufaa au la.
 Aidha wakili Mutalemwa alidai ombi la kuachiwa huru washitakiwa si jambo zuri na kama litakuwa sahihi basi wataendelea kushikiliwa kwa kisheria.
 Hata hivyo,  Hakimu Mwambapa alisema amesikiliza kila upande  na hajakubali wala kukataa yale yaliyozungumza lakini Januari 23 mwaka huu atatoa uamuzi wa hoja hizo zilizotolewa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa Miriam na Revocatus wanadaiwa kumuua kwa makusudi Anethe Msuya, dada wa bilionea, Erasto Msuya, kwa kumchinja nyumbani kwake eneo la  Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam Mei 25, mwaka jana
GPL

No comments: