Advertisements

Friday, January 20, 2017

Mfanyabiashara ahojiwa kifo cha mteja

MFANYABIASHARA mmiliki wa hoteli na duka la vinywaji vyenye kilevi katika mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara, Emmanuel Makamba (32) anashikiliwa na Polisi katika Kituo cha Sirari kwa mahojiano kutokana na tuhuma za mauaji ya mteja wake.

Ilielezwa kuwa mfanyabiashara huyo na wenzake wanatuhumiwa kusababisha kifo cha Baraka Thomas, mkazi wa kijiji cha Gwitiryo aliyekuwa akinywa pombe katika duka hilo.

Taarifa zinasema kuwa Thomas aliuawa baada ya kuzuka ugomvi kwenye duka hilo la vinywaji la Makamba.

Diwani wa Sirari, Nyangoko Paulo, alisema kuwa mauaji hayo yalitokea mwishoni mwa wiki iliyopita nyakati za usiku, ambapo ilidaiwa kulitokea ugomvi kati ya wateja akiwemo Thomas, wakati wakinywa pombe.

Kwa maelezo ya Diwani huyo, Thomas alipigwa na kitu kizito kama gongo la mti kichwani.

"Kupigwa huko kulisababisha kutokwa damu nyingi na kukimbizwa katika Kituo cha Polisi na kupatiwa fomu ya PF 3 ya kutibiwa, ambapo alikimbizwa hospitali ya Wilaya ya Tarime lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya baada ya kushindwa kuongea na kupelekwa nchini Kenya kwa matibabu ambapo Januari 17, mwaka huu alifariki akipatiwa matibabu nchini humo," Paulo alisema.

Aliongeza kuwa mwili wa merehemu ulileta kijijini kwao Gwitiryo ukitokea Kenya na kuzikwa. Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Andrew Satta alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema kuwa Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu mauaji hao na kwamba inaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine.

HABARI LEO

No comments: