ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 30, 2017

MWENYEKITI WA KITONGOJI AUAWA KWA PANGA

Image result for panga knife
By Anthony Mayunga, Mwananchi amayunga@mwananchipapers.co.tz

Serengeti. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamakarakara wilayani hapa, Chacha Range(30) anadaiwa kuuawa kwa kukatwa panga na rafiki yake wakitoka kunywa gongo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi alisema mauaji hayo yalitokea saa tisa usiku Januari 27, jirani na nyumbani kwake. Alisema baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa huyo aliipeleka familia ya marehemu eneo la tukio na baadaye alitoweka.

Alisema polisi kwa kushirikiana na wananchi wanamtafuta mtuhumiwa, (jina linahifadhiwa) anayedaiwa kutoroka juzi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kenyamonta, Augustine Baraganza alisema mtuhumiwa baada ya kumkata kwa panga mwenyekiti huyo, alikwenda nyumbani kwa kiongozi huyo na kuwaamsha mkewe na mama yake na kuwataarifu kuwa amemkata kwa panga mwenyekiti na yuko hoi.

“Aliwaambia wasihangaike kuuliza kwa kuwa aliyefanya kitendo hicho ni yeye na aliwapeleka hadi eneo la tukio na kumkuta mwenyekiti huyo akikoroma kwa kuwa alikuwa amekatwa paji la uso, kupasuka pua, kisogo na alijeruhiwa mkono wa kushoto,” alidai ofisa huyo.

Baraganza alidai kuwa walisimama kwa muda na mtuhumiwa huyo na baadaye aliwaaga kuwa amechoka kusimama hivyo anakwenda kwake ambako ni jirani na aliawaacha hapo. Alisema walimpeleka hospitali lakini alikata roho kabla ya kupata huduma.

Habari kutoka kwa baadhi ya wanakijiji zinadai kuwa kabla ya kuuawa, mwenyekiti na mtuhumiwa walikuwa wakinywa gongo pamoja mchana na kulitokea kutoelewana.

Taarifa hizo zilidai baadaye mtuhumiwa alimshambulia mwenyekiti huyo walipokuwa wakirejea nyumbani.

Mauaji hayo yametokea siku chache baada ya kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu aliyoitoa kwenye kikao na watendaji wa vijiji na kata akiwataka kusimamia masuala ya ulinzi na usalama.

“Haiwezekani watu wanafanya mauaji hadharani halafu hawakamatwi, tena kijijini, hatuwezi kuvumilia tabia hiyo,” alisema.

Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Serengeti, Alfred Kyebe hivi karibuni katika mkutano wa wadau wa ulinzi na usalama, alisema wananchi wanathamini mifugo zaidi kuliko watu.

“Akiibiwa ng’ombe mmoja watatoka vijiji vinne kumsaka, lakini mtu akiuawa na mwenzake hakuna anayehangaika na muuaji, utamaduni ambao unatakiwa kuachwa.”

No comments: