Advertisements

Tuesday, January 17, 2017

SABABU ZA EDWARD LOWASSA KUKAMATWA NA POLISI JANA

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana alikamatwa na polisi mkoani Geita akituhumiwa kufanya mkutano bila kibali. 

Lowassa, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alikuwa njiani akitokea mkoani Kagera, ikiwa ni mwendelezo wa ziara za viongozi wa chama hicho katika kanda zake kutekeleza Operesheni Kata Funua inayohusisha mikutano ya ndani. Hata hivyo, aliachiwa jana jioni. 

Akiwa ameongozana na viongozi na makada wa Chadema, Lowassa aliingia Geita saa 9:30 alasiri na kupokewa na umati wa wananchi waliojitokeza eneo la Nyankumbu, tayari kwa safari ya kwenda kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Nkome. 

Viongozi wengine waliokuwamo kwenye msafara huo ni Profesa Mwesiga Baregu, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Hamis Mgeja, ambaye ni kada wa chama hicho. 


Msafara huo uliokuwa wa magari matano, ukisindikizwa na pikipiki na wafuasi kadhaa wa chama hicho, ulipitia makutano ya barabara mjini Geita na kukutana na magari ya polisi yaliyosheheni askari wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD), Ally Kitumbo. 

Bila kuingilia msafara huo, magari ya polisi yaliufuatilia kwa nyuma ulipokuwa ukielekea Kata ya Nkome. 

Hali ya hewa ilichafuka baada ya msafara kufika eneo la Soko Kuu wakati wananchi walipouzuia wakitaka kumsalimia Lowassa, ambaye aligombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita. 

Kiongozi huyo alilazimika kujitokeza juu ya gari lake kuwapungia na baada ya kelele za ‘njaa, njaa, njaa’ kusikika eneo hilo, Lowassa alitumia kipaza sauti kuwaomba wananchi wawe watulivu na wawaruhusu waendelee na safari yao kuwahi mkutano wa kampeni. 

“Ndugu zangu wana-Geita, natamani kuzungumza nanyi lakini sheria inanibana. Naomba muwe watulivu na mturuhusu tuendelee na msafara kuwahi mkutano wa kampeni Nkome,” alisema Lowassa. 

Askari hao wakiongozwa na OCD, walimfuata Lowassa na kumuamuru yeye na msafara wake kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano. Wakati wa kuelekea kituoni, gari lake lilitanguliwa mbele na la polisi na nyuma kulikuwa na jingine la jeshi hilo. 

Kitendo hicho kiliwafanya wananchi waliokuwa na hamu ya kumsikiliza kiongozi huyo kuongozana kwenda kituoni, jambo lililoibua taharuki na polisi kuwatawanya kwa kufyatua mabomu ya machozi.

Waandishi wapigwa
Pamoja na kuwatawanya wananchi kwa mabomu, askari hao pia waliwapiga kwa mikanda na fimbo waandishi wa habari waliokuwa wakifanya kazi yao eneo hilo. 

Hali ilivyokuwa kituoni 
Baada ya kuwasili kituoni huku polisi wakiendelea kuwazuia wananchi, Lowassa alisalia ndani ya gari lake hadi hali ilipotulia na kutakiwa kuingia kituoni. 

Ni magari mawili pekee; la Lowassa na la Profesa Baregu, yaliyoruhusiwa kuingia eneo la polisi huku viongozi wengine kama Singo Benson ambaye ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, na Upendo Peneza (Mbunge wa Viti Maalumu), wakitakiwa kusubiri nje. 

Kitendo cha wananchi kuzidi kufurika kituoni hapo, kiliwafanya polisi kuimarisha ulinzi, wakizuia mtu yeyote kukatiza wala kusogelea eneo hilo. Licha ya kuzingira kituo cha polisi, askari walitanda barabara inayoelekea ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita ambako pia wananchi walizuiwa kukatiza. 

Lowassa apitishwa uani
Baada ya kuona wananchi wanazidi kujaa kituoni, polisi waliamua kumtoa Lowassa kupitia mlango wa nyuma na kumhamishia ofisini kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Mponjoli Mwabulambo.

 Kama ilivyokuwa Kituo cha Kikuu cha Polisi, ulinzi pia uliimarishwa eneo lote la ofisi ya RPC baada ya Lowassa kuhamishiwa huko na wananchi kupata taarifa. 

Kiongozi huyo aliyehamia Chadema akitokea CCM mwaka 2015 aliachiwa jana jioni. Kamanda Mwabulambo alisema hawakumkamata bali walizuia msafara huo kwa ajili ya usalama wake. 

Akizungumzia suala hilo, Peneza alisema huo ni muendelezo wa ukandamizaji dhidi ya viongozi wa Chadema unaofanywa na polisi mkoani Geita, akitoa mfano kitendo cha yeye kuhojiwa kwa saa kadhaa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa madai ya uchochezi alipohutubia mkutano wa hadhara na kusema nchi inakabiliwa na njaa. 

1 comment:

Unknown said...

Katiba ya nchi iheshimiwe.