By James Magai, Mwananchi jmagai@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Sheria ya Huduma za Vyombo Habari iliyopitishwa mwishoni mwa mwaka jana imefikishwa mahakamani na wadau, wakipinga baadhi ya vifungu vyake.
Wadau hao ni Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambao wamefungua kesi kupinga.
Katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Masijala ndogo Dar es Salaam, iliyoko katika Mahakama ya Rufani Tanzania, hati ya madai waliyoiwasilisha mahakamani, wadau wanapinga vifungu 18 vya sheria hiyo.
Vifungu hivyo ni pamoja na 7 (3) (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i), (j); 13, 14, 19, 20, 21, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 52, 53, 54, 58 na 59.
Kesi hiyo itaendeshwa na jopo la mawakili sita, akiwamo Mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu, Fulgence Massawe, Jebra Kambole, Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla, Mpale Mpoki na Donald Deya.
Wakizungumza baada ya kufungua kesi hiyo, walalamikaji hao wamesema wamefikia uamuzi huo kwa kuwa baadhi ya vifungu vya sheria hiyo vinakandamiza uhuru wa habari na wa kujieleza.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema vifungu hivyo vinakiuka matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao unazitaka nchi wanachama kuzingatia na kulinda haki ambazo zimeelezwa katika mkataba huo kwenye Ibara ya 6(d) na ya 7(2), ambao Tanzania iliridhia Julai 7, 2000.
No comments:
Post a Comment