ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 12, 2017

DC SIKONGE AKAA MEZA MOJA NA WAFUGAJI, AUNDA KAMATI KUMALIZA MALALAMIKO YAO

Na Mussa Mbeho, Sikonge

MKUU wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri ameingilia kati sakata la mgogoro wa wafugaji na maofisa maliasili wilayani humo baada ya wafugaji 4 kukamatwa na kuswekwa ndani huku mmoja akipigwa risasi na kuvunjwa miguu yake kwa madai ya kuingia katika eneo la hifadhi.

Sakata hilo ambalo limeibua hasira miongoni mwa wafugaji limemfanya DC huyo kukutana na wafugaji wote wa vijiji vilivyoko katika kata ya Ngoywa na Ipole wilayani humo na kusikiliza malalamiko yao huku akiahidi kuchangia gharama za matibabu kwa mfugaji aliyepigwa risasi.  

Awali alikutana na viongozi wa chama cha wafugaji wilayani humo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kanda ya Magharibi Kusundwa Wamalwa ambao walieleza kusikitishwa kwao na vitendo vya kamatakamata, udhalilishwaji, vipigo na uonevu wanavyofanyiwa na askari wa maliasili.


DC aliwaambia wafugaji hao kuwa serikali haina dhamira ya kumnyanyasa mwananchi wake na hata inapotokea kuna tatizo eneo fulani kiongozi anapaswa  kukutana na wahusika na kusikiliza malalamiko yao na kuyafanyia kazi.

Ili kubaini ukweli wa malalamiko yao ikiwemo vipigo, kukamatwa wafugaji na mifugo ndani au nje ya eneo la hifadhi, DC aliunda kamati itakayochunguza ukweli wake ikihusisha baadhi ya wafugaji ili kujiridhisha kama kuna vitendo vya uonevu vilivyofanywa na askari wa maliasili ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Alibainisha wazi kuwa baada ya kamati hiyo kukamilisha uchunguzi wake afisa yeyote wa maliasili atakayebainika kutumia wadhifa wake vibaya dhidi ya wafugaji hao atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha aliwataka kufuata taratibu punde mifugo yao inapokamatwa na sio kutozwa mamilioni ya faini na askari hao pasipo kufuata mwongozo au utaratibu unaokubalika wa ulipaji faini, ambapo aliwataka maafisa wote wa maliasili kuacha mara moja tabia za kutoza mamilioni ya fedha kinyume cha taratibu.

Kuhusiana na ukosefu wa malisho, DC alieleza kuwa tayari alishaunda timu maalumu ya kuzunguka kila kijiji kubaini maeneo yaliyopo ili kutenga eneo maalumu la kilimo na wafugaji,  aliwataka kuwa na subira na kuendelea kutii sheria za nchi kwa kutoingiza mifugo yao katika eneo lisilostahilia.

Alitaja viwango vya faini vinavyopaswa kutozwa kwa mifugo inayokamatwa, kuwa kila kundi la ng’ombe 2-10 faini ni sh laki 2 na fidia milioni 1 (jumla mil 1.2), kundi la ng’ombe 11-50 faini ni laki 5 na fidia 2.5 (jumla mil 3) na ng’ombe 51-100 faini ni laki 7 na fidia million 3.5 (jumla mil 4.2) na sio vinginevyo.

Aliongeza kuwa ng’ombe kuanzia 100 na kuendelea faini yake inakuwa milioni 1 na fidia milioni 5 jumla mil.6, aidha alisema afisa wanyama pori yeyote atakayebainika kutoza faini na fidia zaidi ya kiwango kilichowekwa sheria itachukua mkondo wake.

Wakitoa kilio chao mbele ya DC wafugaji hao walisema mara nyingi mifugo yao imekuwa ikikamatwa nje ya eneo la hifadhi na kuswagwa hadi ndani ya hifadhi inayozunguka kijiji chao ili mradi wapigwe faini tu.

Walisema suala la kutozwa faini zaidi ya kiwango kilichowekwa ikiwemo vipigo na dhuluma limekuwa la kawaida sana na hakuna hatua zozote ambazo zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya maafisa hao.

Shiga Lubinza (70) alihoji watapata wapi malisho ya mifugo kama zaidi ya robo tatu ya eneo lote la wilaya hiyo limefanywa kuwa hifadhi ya serikali, kwa nini kunyanyaswa kiasi hicho, na kuongeza kuwa kama wao siyo Watanzania basi waambiwe ili wahamie nchi jirani inayohitaji wafugaji wenye mifugo mingi.

Diwani wa kata ya Ngoywa Lucas Kiberenge (CHADEMA) alimshukuru DC Magiri kwa dhamira yake nzuri ya kumaliza kero za wafugaji ikiwemo agizo lake la  kuachiliwa kwa mifugo iliyokamatwa kwa kulipiwa faini ya kawaida tu, alibainisha wazi kuwa DC huyo ni mfano wa kuigwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Simon Ngatunga alisema wafugaji ni wadau muhimu sana kwa maendeleo ya halmashauri yake, kwani wamekuwa wakichangia fedha nyingi kwa shughuli za maendeleo ya wilaya hiyo.

Alimwagiza Mtendaji wa Kata na Wenyeviti wa serikali za vijiji kukaa meza moja na wafugaji hao na kusikiliza kero zao na kama kuna tatizo kubwa walilete ofisini kwake haraka ili lishukughulikiwe kuliko kusubiri hadi mtu apigwe risasi au akamatwe.

No comments: