Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Philip Mpango akiongea na watakwimu (hawapo pichani) katika mkutano wa kujadili matumizi ya takwimu za umaskini na namna bora ya kupima hali ya umaskini Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akiongea na watakwimu katika mkutano wa kujadili matumizi ya takwimu za umaskini na namna bora ya kupima hali ya umaskini Afrika
Mtafiti Mwandamizi kutoka REPOA Dkt. Blandina Kilama akichangia mada katika mkutano wa kujadili matumizi ya takwimu za umaskini na namna bora ya kupima hali ya umaskini Afrika.
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Roeland Van De Geer akiongea na watakwimu (hawapo pichani) katika mkutano wa kujadili matumizi ya takwimu za umaskini na namna bora ya kupima hali ya umaskini Afrika. (Picha na Benjamin Sawe-Maelezo)
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia saba kwa mwaka umepelekea kiwango cha umaskini kupungua kutoka asilimia 36.8 hadi 28.2.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kitaifa wa kujadili matumizi ya takwimu za umaskini na namna bora ya kupima hali ya umaskini afrika leo jijini Dar es salaam.
Waziri Dkt. Mpango alisema kuwa fursa za ukuaji wa uchumi uliopo umetufikisha hapa tulipo, hivyo amewataka wananchi kutumia fuirsa zilizopo kwa maendeleo ya nchi.
Aidha, Dkt. Mpango ametoa wito kwa mabingwa wa takwimu kuangalia upya moduli mbalimbali zinazotumika kupima umaskini nchini ili kuweza kuja na mikakati ya kupambana na hali hiyo.
“Takwimu za umaskini na upimaji wa umaskini katika nchi zinazoendelea hasa kusini mwa nchi za Jangwa la Sahara bado ni changamoto, hivyo Serikali ya tanzania ya awamu ya tano imejikita katika kupambana na umaskini” alisisitiza Waziri Dkt. Mpango.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa mkutano huo unalengo la kujadili kwa kina matumizi ya takwimu za hali ya umaskini katika sera zinazolenga ama kupunguza au kuondokana na umaskini hususani katika nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Afrika.
Alisema kuwa matumizi ya takwimu katika kupanga maendeleo ya wananchi katika nchi zinazoendelea hayaendani na kasi inayotakiwa kimataifa hivyo Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeona umuhimu wa kuwa na mkutano huo kwa kuwakutanisha watakwimu na wachumi na fani nyingine za kitaaluma kujadili kwa kina matumizi ya takwimu na hali ya umaskini.
Hata hivyo Dkt. Chuwa amewataka watunga sera nchini kutumia takwimu hizo katika kupanga maendeleo ya nchi, na kuwataka baadhi ya watu kutotumia takwimu hizo kupotosha umma kuhusu hali ya umaskini nchini.
Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Roeland Van De Geer alisema kuwa wao kama wadau wa maendeleo wataendelea kutumia takwimu hizo kwa ajili ya maendeleo ya nchi husika.
Alisema kuwa Ofisi yake imeandaa Euro Milioni 200 kwa ajili ya sekta ya Nishati ikiwa katika juhudi za kumuunga Waziri Muhongo endapo watapata takwimu za mahitaji ya umeme nchini.
Mbali na hayo, Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bella Bird alisema kuwa takwimu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi au bara lolote duniani, hivyo ni jambo la umuhimu kuboresha upatikanaji wa takwimu.
“katika sekta ya kilimo tunahitaji takwimu kwani kumekuwa na changamoto kadha wa kadha katika upimaji katika sekta hiyo” alifafanua Bella Bird.
Mkutano huo wa siku mbili wa kimataifa wa kujadili matumizi ya takwimu za umaskini na namna bora ya kupima hali ya umaskini afrika umeshirikisha takribani washiriki 150 kutoka ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment