Arusha. Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Arusha imependekeza makada wake 1,575 kuvuliwa uanachama kwa madai ya usaliti katika Uchaguzi Mkuu uliopita kwa kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa.
Miongoni mwa wanachama hao yumo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dk Wilfred Soileli na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambao wamechukuliwa hatua mbalimbali.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika kikao cha halmashauri hiyo ambacho kilipokea taarifa ya hali ya chama mkoani hapa hususan uchaguzi huo ambao kilipoteza majimbo sita kati ya saba na halmashauri tano.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer alikiri kufanyika kikao hicho na kufikia uamuzi mzito wa kukijenga upya chama, lakini akasema taarifa hizo zingetolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shabani Mdoe.
“Ni kweli tulikuwa na kikao lakini hayo ni mambo ya kiofisi, naomba uwasiliane na katibu wa uenezi atawapa taarifa,” alisema.
Mdoe alipotafutwa, licha ya kukiri kuwapo kikao hicho na kufikia uamuzi mzito wa kuwang’oa wasaliti, alisema taarifa kamili zitatolewa leo.
“Ni kweli tulikuwa na hicho kikao lakini muda huu nipo hospitali ila kesho tutatoa taarifa rasmi saa sita mchana,” alisema.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho, alisema licha ya kupendekezwa mwenyekiti huyo wa CCM kufukuzwa, pia kikao hicho kimependekeza kusimamishwa kwa Mjumbe wa NEC kutoka Wilaya ya Arusha, Mathias Manga na mwenzake wa wilaya ya kichama Meru, Julius Mungure.
Pia imependekezwa Mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Karatu, Awaki Awakii apewe barua ya onyo kali kutokana na tuhuma za usaliti.
Manga ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini jijini hapa pamoja na viongozi wengine, hivi karibuni waliitwa Makao Makuu ya CCM Dodoma kujieleza.
Hata hivyo, akizungumza na mwananchi jana, Soileli alisema hajui kilichoendelea katika kikao hicho baada ya kutakiwa kutoka nje ili wajumbe wamjadili.
“Sina hizo taarifa kama wameamua nifukuzwe au la. Mimi bado ni mwanaCCM halali na sijapewa barua yoyote,” alisema.
Awakii pia alisema hajui lolote kwa kuwa alikuwa Dodoma na alirejea Karatu jana, “Nasikia tu hayo maneno lakini naomba uwasiliane na katibu mwenezi atakupa taarifa kamili.”
Juhudi za kumpata Manga na Mungule, hazikufanikiwa baada ya kutopatikana kwa simu jana.
Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015, CCM ilitangaza kupambana na wasaliti ndani ya chama hicho tawala.
Katika uchaguzi huo, makada zaidi ya 50 wakiwamo viongozi wa chama hicho, walihamia Chadema wakimuunga mkono Lowassa ambaye alikuwa ameenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwa urais ndani ya CCM. Waliohama alikuwamo pia Mwenyekiti wa Mkoa, Onesmo ole Nangole na Katibu wa Uenezi, Joseph Isack.
No comments:
Post a Comment