RAIS John Magufuli na mgeni wake Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wamekubaliana kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kuongeza biashara kati ya nchi hizo ili kukuza uchumi wa nchi hizo mbili. Rais Museveni yupo nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili, ambapo jana alikuwa na mazungumzo ya kina na Rais Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Magufuli alibainisha kuwa mazungumzo yao pia yalilenga suala la kusaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA) na nchi za Jumuia ya Ulaya (EU).
Rais Magufuli alisisitiza kuwa Tanzania haitasaini mkataba wa EPA na kubainisha kuwa hiyo ni njia nyingine ya ukoloni.
“Tumezungumza kwa kina na Rais Museveni na tumekubaliana kuendelea kulizungumza. Nimemueleza kuwa sisi Tanzania tunaona EPA haina faida na ni ukoloni mwingine, ambao unaletwa kwa sababu ya mambo mengi.
“Hatuwezi kuzungumzia kujenga viwanda wakati huohuo tunashindana na watu wenye viwanda vikubwa.
“Hili tumelizungumza kwa kina na tumekubaliana na Rais Museveni na jopo la wataalamu litakwenda Uganda Machi 18, kutoa maelezo ya kina. Na yeye Rais Museveni amesema kimsingi anapenda kufanya kitu chenye faida.” Rais Magufuli aliongeza:
“Rais Museveni ni ndugu yetu na alibebwa na Watanzania na kwa sababu Nyerere (Baba wa Taifa Julius Nyerere) hayupo basi anibebe mimi kwa kufanya mambo ambayo nafikiri ni kwa faida ya Watanzania.”
Rais Museveni alisema kutokana na msimamo wa Tanzania katika suala la EPA, ameamua kuja kufanya mazangumzo na Rais Magufuli ili kuwa na msimamo wa pamoja.
“Nimekuja ili kufanya mazungumzo na Rais Magufuli na kujumuisha mawazo yetu na kuwa na msimamo mmoja.
“Kama jambo dogo la EPA limekuja, mmoja anakwenda kushoto mwingine kulia tunaweza kushughulikia. Nimesema ngoja niende maana hili si juu ya EPA ni juu yetu sisi,” alisema na kuongeza kuwa ameshafanya mazungumzo na Kenya ili kuwa na msimamo mmoja.
Aidha, Rais Magufuli amesisitiza haja ya kuongeza biashara kati ya nchi hizo mbili na kuwa tayari serikali imeshafanya juhudi mbalimbali za kuwezesha kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili. Mwaka 2015 biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili ulikuwa na thamani ya Sh bilioni 178.19 na kwa mwaka 2016 imeongezeka hadi kufukia Sh bilioni 193.59 wakati uwekezaji wa Uganda kwa Tanzania ni dola za Marekani milioni 46.05 uliotoa ajira 1,447.
“Lakini uwekezaji huu wa biashara bado uko chini ukilinganisha na undugu halisi wa Tanzania na Uganda, kwa hiyo Rais tumekubali kuwa sasa biashara lazima ikue zaidi.”
Rais Magufuli alisema Tanzania kwa sasa inajenga reli ya kisasa, sambamba na ukarabati wa mv Umoja na kujenga bandari kavu itakayohudumia mizigo ya Uganda pekee mkoani Mwanza ambayo itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi Kampala, Uganda.
Aidha, Rais Museveni alishukuru serikali ya Tanzania kwa hatua za kuboresha miundombinu ya usafiri na kusema;
”Nashukuru kwa ujenzi wa reli ya kisasa na huu ni mchango wa mara ya pili kwa ukombozi wa Uganda.
“Tunajenga bandari kavu Mwanza ili mfanyabiashara wa Uganda asihangaike kuja Dar es Salaam atafanya taratibu zote za kutoa mizigo pele pale Mwanza.”
Rais Magufuli alisema pia Serikali imeondoa urasimu uliokuwa ukiwakatisha tamaa wafanyabiashara na kupunguza vituo vya ukaguzi ambapo kwa sasa vitakuwa vitatu kutoka Dar es Salaam hadi Mtukula.
Aidha, Magufuli ameomba Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kufanya safari zake katika miji ya Entebbe na mingine jambo ambalo Rais Museveni amekubaliana nalo huku akiwaahidi Waganda kuwa wakati wa maombolezo ya kifo la Shirika la Ndege la Uganda umefika mwisho na kuwa atalifufua shirika hilo.
No comments:
Post a Comment