MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetoa amri kuzuia Polisi wasimkamate Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe hadi maombi yake ya kupinga asikamatwe, yatakaposikilizwa Alhamisi wiki hii.
Jopo la majaji watatu likiongozwa na Sekieti Kihiyo, Lugano Mwandambo na Pellagia Kaday limetoa zuio hilo leo. Hata hivyo majaji hao wameruhusu Polisi kumuita Mbowe kwa mahojiano watakapomuhitaji.
Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2017, Mbowe anapinga mamlaka ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO) Camilius Wambura, ya kutaka kumkamata hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.
Maombi ya kesi hiyo yataanza kusikilizwa Februari 23, mwaka huu saa 7:30 mchana katika chumba cha wazi cha mahakama ili kuruhusu watu kusikiliza.
Kesi hiyo leo imesikilizwa kwa vipindi vitatu kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana.
Mahakama imeamuru upande wa wadai ulioongozwa na Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, kurekebisha maombi yao kwa kuwa hawakumuingiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) licha ya kuishitaki serikali.
No comments:
Post a Comment