ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 19, 2017

MBOWE ASAKWA NA POLISI KILA KONA, APEWA MASAA 48 AJISALIMISHE MWENYEWE KWA SIRRO. MASOGANGE, CHID BENZ MAHAKAMANI KESHO

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro amesema endapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hataripoti kituoni kesho (saa 48 tangu jana), atatafutwa kwa namna ambayo jeshi hilo litaona inafaa.

Mbowe ni miongoni mwa watu mashuhuri waliotajwa hivi karibuni katika orodha ya watu 65 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wanaodaiwa kujua taarifa za wanaojihusisha na dawa za kulevya. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna Siro alisema Mbowe kupitia kwa baadhi ya viongozi aliwajulisha angeripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Jumatano ya Februari 15, lakini alikuwa hajaripoti hadi jana 

“Jumatatu asiporipoti kutakuwa hakuna namna ya kulizuia tena Jeshi la Polisi kutafuta namna ya kumuhoji,” alisema. 

“Mheshimiwa Mbowe tunamheshimu sana kama kiongozi wa chama kikubwa cha siasa na hata akiwa bungeni ameonekana akipinga kwa nguvu suala la dawa za kulevya na anasikitika kuona vijana wa Kitanzania wanateketea. 

"Asitafute namna nyingine, tunamuhitaji kwa ajili ya kumuhoji kutokana na hizi tuhuma za dawa za kulevya,” alisema Siro. 

Alisema kiongozi kama Mbowe hatakiwi kuwa mtu wa kuta- futwa. ”Jeshi la Polisi lisingependa kuwa na mvutano na yeye, najua anajua kuwa tunamtafuta. 

"Jana (juzi) tumejitahidi kumtafuta kwa simu hajapatikana, tumekwenda nyumbani kwake hatujampata na hata tulipokwenda mahali ambapo inasemekana anaishi sasa hatukumpata,” alisema. 

Kamanda Siro alisema hafahamu ni kwanini Mbowe haja- ripoti wakati yeye mwenyewe anapinga biashara ya dawa za kulevya, hivyo baada ya taarifa yake ya jana, anamuomba ajitahidi aende waonane, tofauti na hapo ni lazima atakamatwa na kuhojiwa kwa kuwa ndiyo wajibu wa jeshi hilo.

 Hata hivyo, Februari 10 akiwa mjini Dodoma, Mbowe alise- ma hatafika polisi kwa kuitwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda lakini yupo tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola endapo utaratibu wa kisheria utafuatwa. 

Wengine kortini 
Katika hatua nyingine, Kamishna Siro alisema operesheni ya dawa za kulevya inaendelea vizuri na kesho watuhumiwa Agnes Gerald ‘Masogange’, Rashid Said ‘Chid Mapenzi’ na Walid Nasher watapelekwa mahakamani. 

Hata hivyo, Kamanda Siro alitoa kauli mbili zinazokinzana, mwanzo alisema watuhumiwa hao watashtakiwa kwa kutumia dawa za kulevya, lakini baadaye akasema walipatikana na dawa hizo. 

Alisema operesheni inayoendelea tangu Februari 16 imewezesha kukamatwa watuhumiwa 73 wa makosa mbalimbali, yakiwamo ya wizi wa kutumia nguvu. 

Pia, ilikamatwa mitambo mitano ya kutengeneza pombe haramu aina ya gongo na puli 250 za bangi. Kamishna Siro alisema juzi walimkamata mtuhumiwa anayejifanya askari magereza akiwa na sare za jeshi hilo.

Alisema mtuhumiwa huyo, Elias Msingwa aliwahi kuwa askari wa jeshi hilo kabla ya kuachishwa kazi Desemba mwaka jana, akiwa na cheo cha Koplo lakini amekamatwa akiwa na sare zikiwa na cheo cha Sajenti. 

Akizungumzia tukio hilo katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, akiwa na pingu mkononi, Msingwa alisema alikuwa askari katika Gereza la Keko jijini Dar es Salaam na alifanya kitendo hicho baada ya kukosa nauli ya daladala. 

“Ninakaa Kivule jana (juzi) nilikuwa sina nauli ya kuja mjini ndiyo maana nikavaa sare hizi ili niweze kusafiri bure, ninaomba radhi kwa Watanzania na kuwashauri wenzangu wasije wakafanya hivi na baada ya hapa nitazirudisha sare hizi,” alisema Msingwa. 

Kamishna Siro alisema sare hizo zilivaliwa kinyume na sheria, huku zikitumika kuwababaisha wananchi hivyo upelelezi unaendelea utakapokamilika jalada lake litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.

No comments: