ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 24, 2017

MKE WA BILIONEA MSUYA ASHITAKIWA TENA

KWA mara ya pili, mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Mariam Mrita (41) na mfanyabiashara Revocatus Muyela (40), wamesomewa mashitaka ya mauaji. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam juzi iliwaachia huru kwa kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kurekebisha hati ya mashitaka.

Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi amedai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na kosa moja la mauaji mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Kuna madai ya kuwepo utata kuhusiana na uamuzi huo wa upande wa mashitaka.

Akiwasomea mashitaka, Kishenyi amedai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na kosa moja la mauaji ambalo walilitenda Mei 25, mwaka jana.

Amedai kuwa washitakiwa hao walimuua dada wa bilionea Msuya, Aneth ambaye walimchinja nyumbani kwake Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasomea kosa hilo, Hakimu Simba alisema kuwa washitakiwa hawapaswi kujibu kitu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kishenyi aliiomba Mahakama iahirishe kesi hadi siku nyingine kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Utata ulitokea baada ya Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kudai kuwa hati ya mashitaka ipo kinyume na sheria na kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Alidai kuwa kesi hiyo imefunguliwa kinyume na sheria kwa sababu ilishatolewa uamuzi Februari 23, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa ambapo aliwaachia huru washitakiwa wote.

Alidai kuwa, alimsikia Hakimu Mwambapa aliyetoa uamuzi huo akisema washitakiwa wameachiwa huru na si kwamba wamefutiwa mashitaka.

"Maneno aliyoyatumia Hakimu katika uamuzi wake ni amewa-set free washitakiwa na si kuwa-discharge, hivyo hawa washitakiwa wapo huru na hawakupaswa kukamatwa na kuletwa mahakamani kusomewa kosa hilo la mauaji," alidai Kibatala.

Pia alibainisha kuwa hatua ya Mahakama hiyo kukosa mamlaka inatokana na kosa ambalo wamesomewa washitakiwa tayari limeshatolewa uamuzi.

Alidai kuwa kitendo cha upande wa mashtaka kuwakamata washtakiwa hao na kuwasomea kosa lile lile la mauaji ni sawa na uchonganishi baina ya Hakimu mmoja na mwingine.

Alieleza kuwa awali kabla ya washtakiwa hao kuachiwa huru upande wa mashtaka ulipewa nafasi zaidi ya tatu na Mahakama ili kubadilisha hati ya mashtaka lakini walishindwa.

Akijibu, Kishenyi amedai kuwa washitakiwa hao wamepandishwa kizimbani jana na kusomewa kosa hilo kwa mujibu wa sheria.

Amedai kuwa uamuzi uliotolewa juzi na Mahakama hiyo ilikuwa ni kuwafutia mashitaka ambapo Jamhuri ina uwezo wa kuwakamata tena washitakiwa na kuwasomea kosa hilo la mauaji.

Alieleza kuwa kwa namna yeyote ile uamuzi uliotolewa mahakamani hapo, ulikuwa na athari za kuwafutia mashtaka washtakiwa, ndio maana wamekamatwa tena.

Amebainisha kuwa haoni sehemu yeyote ambayo inaonesha kosa walilosemewa washitakiwa lipo kimakosa mahakamani hapo.

Kutokana na mvutano huo wa kisheria, Hakimu Simba amesem, anajua mzizi wa fitina wa kuibuka kwa hoja hizo ni uamuzi uliotolewa juzi mahakamani hapo.

"Ili kukata mzizi huo wa fitina na kuondoa utata, itabidi uamuzi huo uletwe kwa ajili ya kuuangalia sehemu ambazo mnabishania, tena kwa vile umetolewa na mahakama hii...hakuna kitakachoharibika," amesema Hakimu Simba.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 7, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi kama washtakiwa waliachiwa huru ama walifutiwa mashtaka. ends

HABARI LEO

No comments: