Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemueleza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu kuwa ameponea chupuchupu kutumbuliwa baada ya kukataa maagizo ya watu ambao hakuwataja, kuhusu sakata la dawa za kulevya.
Akizungumza wakati wa kuwaapisha viongozi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jana, Rais alimpongeza IGP Mangu kwa hatua hiyo na kuwataka viongozi wengine kuunga mkono jitihada hizo.
“Ndiyo maana nampongeza IGP kwa kuwachukulia hatua watendaji walio chini yake ili uchunguzi ufanyike na ninataka kukuhakikishia umefanya vizuri na umetoa heshima kwa Jeshi la Polisi.
“Tembea kifua mbele katika vita hii ya dawa za kulevya, hakuna mtu maarufu, hakuna mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri, au mtoto wa fulani ambaye alijihusisha aachwe. Hata angekuwa mke wangu Janeth, shika tu kwa sababu dawa za kulevya kwa Taifa letu sasa hivi zimefikia mahali pabaya,” alisema Rais alipozungumzia uamuzi wa IGP kuwasimamisha kazi askari waliotajwa kuhusika na tuhuma za dawa za kulevya.
Alimweleza IGP Mangu kuwa ana bahati watu waliompigia simu hakuwasikiliza, na iwapo angefanya hivyo, angekuwa ameshatimuliwa.
“Ninajua mtapata vipingamizi vingi, hata IGP najua umepigiwa simu, wanakupa advice (ushauri) fulani, ninajua. Nashukuru hukuwasikiliza, ungewasikiliza ningejua na wewe unahusika na leo usingekuwa IGP,” alisema.
No comments:
Post a Comment