ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 23, 2017

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete Akutana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika jijini Abidjan, Ivory Coast



 Rais Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya ELimu, Dkt. Jakaya Kikwete akikaribishwa kwa furaha na mwenyeji wake Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina ofisini kwake jijini  Abidjan, Ivory Coast
 Rais Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu  Dkt. Jakaya Kikwete akiwasilisha ripoti ya Kizazi cha Elimu kwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Adesina
 Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Adesina katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano.
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akibadilishana mawazo na  Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia  Dkt, Makthar Diop pembezoni mwa mkutano huo.

Rais Mstaafu na  Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya Kupendekeza Namna Bora ya Kugharamia Fursa za ELimu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi Adesina alipomtembelea katika Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Abidjan, Ivory Coast.
Katika mazungumzo yao, Rais Mstaafu Kikwete amewasilisha kwa Rais Adesina ripoti ya Kamisheni ya Elimu na kuwasilisha rai ya Kamisheni hiyo ya kuiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika kusaidia nchi za Afrika kugharamia miradi na mageuzi ya sekta ya elimu katika nchi zao. Rai hiyo ya Kamisheni inatokana na ripoti kubaini kuwa misaada na mikopo inayotolewa kwa sekta ya elimu imekuwa ikishuka ikilinganisha na zile zinazotolewa kwa miradi ya afya na miundombinu. Kamisheni inaamini kuwa bila kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu, watoto wapatao milioni 223 duniani (takribani milioni 160 wakiwa Afrika) watakosa fursa ya kupata elimu ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake, Rais Adesina ameupokea ujumbe huo na kusema kuwa takwimu zilizoibuliwa na Ripoti ya Kamisheni 'zinakatisha tamaa na pia zinatoa changamoto'. Rais Adesina ameahidi kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika itaitizama Ripoti hiyo na mapendekezo yake na iko tayari kufanya kazi kwa karibu na Kamisheni katika kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo katika elimu barani Afrika. Amesema kuwa Benki yake inatambua kuwa kuwekeza katika vijana na nguvu kazi ya Afrika ndio jawabu la maendeleo ya uhakika huko mbeleni.
Katika hatua nyingine, Rais Mstaafu amekutana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Makhtar Diop pembezoni mwa mkutano wake na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Ziara ya Rais Mstaafu nchini Ivory Coast itahitimishwa kwa kukutana na Rais wa Ivory Coast Mhe. Alassane Ouattara.

No comments: